Fidia zisikwamishe miradi ya barabara Zanzibar - Hemed
Ujenzi wa Daraja na Barabara ya Amani-Biziredi Mkoa wa mjini Ukoendelea. Picha na Jesse Mikofu
Muktasari:
- Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla amesema hakuna sababu kuchelewa kulipa fidia na wananchi ili wapishe miradi itekelezwe kama ilivyopangwa
Unguja. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah amesema Serikali haipo tayari kuona miradi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara ikikwama au kuchelewa kutokana na changamoto za ulipaji fidia.
Hemed ametoa kauli hiyo leo Jumamosi, Julai 4, 2026, wakati wa ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya ujenzi wa barabara katika maeneo tofauti ya Zanzibar.
Amesema Serikali imeweka utaratibu mzuri wa kushughulikia fidia, hivyo hakuna sababu ya miradi kusimama wakati taratibu za tathmini na ulipaji zinaweza kukamilishwa kwa wakati.
"Hatuna sababu ya kukwamisha miradi hii kisa fidia. Naagiza tathmini ifanyike kwa maeneo yote ambayo bado hayajalipwa na wananchi walipwe ili wapishe miradi iendelee," amesema.
Ameziagiza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuhakikisha hakuna kikwazo chochote kinachosababisha kuchelewa utekelezaji wa miradi ya barabara nchini.
Miradi hiyo ya barabara ni sehemu ya ujenzi wa kilomita 100.9 kwa thamani ya dola za Marekani 130 milioni, inayotekelezwa na wakandarasi mbalimbali katika Jiji la Unguja.
Hemed pia amewataka wananchi wanaopokea fidia kuhama mara moja katika maeneo husika, akisema Serikali haitasita kuchukua hatua kwa wale watakaokaidi, wakiwemo wanaojenga upya vibanda katika maeneo yaliyolipiwa fidia.
"Wizara tuondoe muhali katika hili. Mtu kama amelipwa aondoke. Kuna baadhi wamekuwa wakaidi au kurejea kujenga vibanda, hilo halikubaliki," amesema.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa Serikali haitamdhalilisha au kumdhulumu mtu yeyote anayestahili kulipwa fidia, na malipo yote yatafanyika kwa mujibu wa tathmini rasmi.
"Tutawalipa wananchi wote kwa mujibu wa tathmini ilivyo na kila mmoja atalipwa haki yake kama walivyolipwa wengine," amesema.
Aidha, amemwagiza mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi kuhakikisha kuwa baada ya ulipaji wa fidia kukamilika, nyumba na majengo yote yanayopaswa kuondolewa yanabomolewa mara moja ili kuruhusu ujenzi kuendelea bila vikwazo.
Amesema lengo la Serikali ni kuimarisha miundombinu kwa masilahi ya wananchi wa sasa na vizazi vijavyo.
Katika hatua nyingine, akiwa katika Bandari ya Mpigaduri Maruhubi, Hemed ameagiza Wizara ya Maji na Nishati kuangalia uwezekano wa kutoa vibali vya mchanga ili kuruhusu ujenzi wa awamu ya pili ya bandari hiyo kuendelea bila kuchelewa.
"Hatuwezi kusitisha miradi mikubwa ya kimkakati kwa kusubiri vibali vya mchanga," amesisitiza.
Pia ameiagiza Wizara ya Uchumi wa Bluu na Uvuvi pamoja na Mamlaka ya Usafiri Baharini (ZMA) kutafuta eneo maalumu litakalowekwa kwa ajili ya shughuli za wavuvi ili kurahisisha shughuli zao.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Ali Said Bakar amesema baadhi ya miradi hukwama kutokana na kuchelewa kukamilika kwa ulipaji wa fidia kwa wananchi.
Naye Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk Khalid Mohammed Salum amemhakikishia Makamu wa Pili wa Rais kuwa wizara itaendelea kusimamia kikamilifu miradi hiyo ili ikamilike kwa wakati na kuwa barabara nyingi zinatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu.
Katika ziara hiyo, Hemed alikagua miradi ya barabara ya Kwamchina Mwanzo (Othman Maalim), Magomeni hadi Mwanakwerekwe Makaburini, Flyover ya Amani, barabara ya Amani hadi Mikunguni, ya Mpigaduri hadi Kinazini, Darajani–Cric Road na barabara ya ZRA hadi Fumba.