Hemed: Sitaki mawaziri wa mafaili, nendeni kwa wananchi
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla akisikiliza maelezo kutoka kwa Mhandisi Emanuel Holehole kuhusu maendeleo ya ujenzi wa kituo cha biashara na jengo la Abiria la Terminal Two yanayojengwa katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume (AAKIA) Unguja Zanzibar.
Muktasari:
- Mtendaji Mkuu huyo wa Serikali amesema wananchi wanakabiliwa na changamoto ni wajibu wa viongozi wakuu kwenda kusikiliza kero zao na kuzipatia ufumbuzi badala ya kusubiri taarifa ofisini.
Unguja. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema hataki kuona mawaziri wa ‘ma-file’ badala yake watoke maofisini kwenda kwa wananchi kusikiliza na kutatua changamoto zao.
Hemed ametoa kauli hiyo leo Jumapili, Julai 5, 2026 katika mwendelezo wa ziara yake ya kutembelea miradi mbalimbali, ambapo ametembelea ujenzi wa jengo la Terminal 2 Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abel Aman Karume, eneo la uchujishaji mafuta bandari Jumuishi Mangapwani na barabara.
"Nimeshatoa maagizo, nikiwa mtendaji mkuu wa Serikali, sitaki kuona mawaziri wa ma-file, nataka waende ‘site’ wakasikilize kero zinazowakabili wananchi," amesema
Hemed amesema kiongozi anayekwenda kwa wananchi anajua changamoto zao na namna ya kuzipatia ufumbuzi tofauti na anayesubiri kuletewa taarifa ofisini.
"Ukisubiri taarifa ofisini unaweza kudanganywa, kiongozi wetu ameshasema na maelekezo yangu twende ‘site’," amesema.
Hata hivyo, ameupongeza uongozi wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi akisema wanafanya kazi kubwa katika kusimamia miradi.
Akizungumza kuhusu ujenzi wa jengo la terminal 2 na kituo cha biashara katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume, Hemed amesema hilo ni eneo muhimu hivyo ukikamilika unakwenda kuleta mageuzi makubwa kwenye uchumi na kuchochea utalii.
"Hili ni eneo moja muhimu sana katika michezo inayokuja mbeleni ya Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon)
na itakuwa kigezo muhimu cha kusababisha tufanikiwe zaidi katika mashindano hayo maana moja ya maeneo watakayopitia ni lango hili la ndege.
Amesema inakwenda kuongeza kasi ya ukuaji uchumi ndani ya nchi kwani mlango wa ndege na bandari hata ajira zitaongezeka na huduma zitaboreka.
Naye Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk Khalid Mohamed Salum amesema terminal 2 itakuwa na uwezo wa kuchukua abiria milioni 1.4 kwa mwaka huku Terminal 3 ikiwa na uwezo wa kuchukua abiria milioni 1.6 kwa mwaka.
"Kwa hiyo tutakapokamilisha majengo yetu haya uwanja wetu utakuwa na uwezo wa kuchukua abiria milioni 3.6 kwa mwaka ambapo kwa sasa wana abiria takribani 2.6 milioni kwa hiyo uwezo wetu umepanda," amesema.
Akiwa katika bandari ya kushusha mafuta Mangapwani, Hemed amesema ipo haja kutoa zabuni au kuzipa kampuni za kizawa zenye uwezo kushiriki katika kujenga miradi au kuwekeza kwenye maeneo tofauti.
Akizungumza kuhusu miundombinu hiyo, Hemed amesema inakwenda kupunguza kwa kiasi kikubwa hali ya upatikanaji wa mafuta kwa Zanzibar.
Mbali na upatikanaji wa nishati kwa haraka, pia amesema hali hiyo inaweza kusababisha pia kushuka bei kwani gharama zitapungua kutoka na mizunguko iliyokuwapo awali ya ushushaji wa mafuta katika visiwa hivyo.
Akitoa taarifa ya kitaalamu, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC), Akif Khamis amesema Serikali imewekeza hapo kwa kushirikiana na kampuni ya ndani ya UP Ltd kwa takribani Dola milioni 15 sawa na Sh39.4 bilioni.
Amesema awali miundombinu hiyo ya kushusha mafuta ilikuwa katika eneo la Mtoni ikiwa na uwezo wa kupokea meli yenye uzito wa tani 2,000 pekee hivyo kusababisha mafuta kupungua mara kwa mara kisiwani humo.
Amesema kwa sasa meli zinakuja na mafuta kutoka Saudi Arabia moja kwa moja na kushusha mafuta Zanzibar tofauti na ilivyokuwa awali ambapo ililazimika kutegemea bandari za Dar es Salaam na Mombasa.
"Tayari zimeshawasili meli mbili, ya kwanza iliwasili Mei 31, 2026 na hii nyingine imewasilia Juni 26, 2026 zote zikiwa na mafuta ya petroli, dizeli, na ya ndege zaidi ya lita milioni 35 zote zikitokea Saudi Arabia.
Amesema miundombinu imezingatia mahitaji yote yanayotakiwa ikiwemo kuhakikisha meli kubwa zinakuja na zinaweza kuhudumia meli hata zenye lita milioni 100.
Amesema kuna vifaa vya kisasa kupima mafuta na ujazo wake kupitia mfumo.