Huu hapa wosia wa Mzee Mwinyi kwa familia

Muktasari:

  • Dk Hussein Mwinyi aeleza baba yake alipolia baada ya kutembelewa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, amesema kabla ya kifo cha baba yao, aliwaita familia yote akawaeleza wanatakiwa kuwa wamoja, akimchagua asimamie familia.

Dk Mwinyi amesema hayo leo, Machi 3, 2024 wakati wa hitma ya hayati Ali Hassan Mwinyi iliyoandaliwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika viwanja vya maonyesho Nyamanzi Fumba, Unguja.

Mzee Mwinyi alifariki dunia Februari 29, 2024 katika Hospitali ya Mzena, jijini Dar es Salaam na maziko yamefanyika jana, Machi 2, eneo la Mangapwani, Zanzibar ambako alikulia na kupata elimu ya msingi na kati.

“Aliniita kwa jina, akaniambia nakuagiza wewe si kwa ukubwa wako, bali kwa nafasi uliyonayo, uwe msimamizi wa familia yangu,” amesema Dk Mwinyi.

Huku akionekana mwenye majonzi, Dk Mwinyi amesema ana mambo mengi ya kuzungumza, lakini akaishia kueleza: “Nimezidiwa naomba niishie hapa."

Kabla ya kueleza hayo, Dk Mwinyi amesema alijizuia kuzungumza, lakini akahisi ana deni kubwa, hivyo asipofanya hivyo ataendelea kubaki na deni hilo.

Dk Mwinyi amemshukuru Rais Samia akisema amewafanyia wema tangu Mzee Mwinyi alipopelekwa nchini Uingereza kwa matibabu, kwamba alikuwa karibu nao akiwauliza kila hatua inayoendelea hata aliporudi nyumbani aliendelea kuwa nao karibu.

“Alipokuja (Rais Samia) kumtembelea nyumbani Mikocheni, Mzee wetu alilia kwa furaha kumuona Rais wetu,” amesema.

Amewashukuru madaktari wa Hospitali ya Mzena alikokuwa amelazwa Mzee Mwinyi akisema walimhudumia kwa upendo mkubwa kwa saa 24.

“Mimi ni daktari, nimefanya kazi nje ya nchi na hapa nchini, katika maisha yangu sijawahi kuona watu waliojitolea kumsaidia mzee wetu kama madaktari wa Hospitali ya Mzena, huduma ilikuwa ya saa 24, walikuwa hawabanduki. Mara nyingi mzee wetu hali yake ilikuwa ikibadilika, lakini tulikuwa nao wakati wote,” amesema.

Dk Mwinyi amewashukuru watu wote walivyojitoa kabla na wakati wa kifo cha Mzee Mwinyi na kwamba alikuwa akipokea simu nyingi kutoka kila upande wakimueleza jinsi wanavyomuombea dua mzee wao.

Hitma ya Mzee Mwinyi

Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kabi amesema kulingana na wema aliofanya Mzee Mwinyi duniani, inawezekana ameenda peponi moja kwa moja.

Mufti Kabi ametoa kauli hiyo baada ya kusoma hitma ya Mzee Mwinyi, akieleza alikuwa mtu wa kusamehe na mwenye uadilifu mkubwa.

“Huyu mzee alikuwa ni mtu mwema na amefanya mengi mazuri na inaweza akawa ameepushwa motoni na kuingizwa peponi, wasiwasi upo kwetu sisi, tufuate matendo yake, alikuwa mtu kivitendo, uongozi wake, alikuwa ni mtu wa kusamehe na muadilifu,” amesema.

Amesema uadilifu wake umetajwa mara nyingin lakini pia alikuwa na huruma kwa watu anaowaongoza, alijishusha kwa watu na kuwaheshimu masheikh wenzake.

Amesema wakati wa uhai wake alifanya mambo mengi ikiwa ni pamoja na ujenzi wa misikiti na nyumba za ibada.

Wakati wa uongozi wake, amesema aliufungua uchumi na Zanzibar, watu walianza kwenda kisiwani hapo kutoka nchi mbalimbali kufanya biashara.

Katibu wa Mufti, Khalid Ali Mfaume amesema wazee wenye hekima wanaondoka, lakini ni lazima kuendeleza waliyoyatenda.

“Jana (Machi 2) tumezika elimu, busara na hekima. Huyu alikuwa sheikh, alikuwa mwalimu, alipomaliza kazi ya urais alikuwa akisalisha misikiti mbalimbali, katika sifa zake zote, basi alikuwa mpenzi wa Mtume Muhamad (S.A.W)” amesema.

Khalid amesema, “Maisha ya binadamu ni hadithi, kila mmoja anatamani azungumzwe hivihivi kama anavyozungumzwa mzee wetu, na hapa ndipo tunaposema waandaliwe watoto wetu katika malezi mema.”

Amesema kila mmoja ana nafasi ya kubadilisha hadithi yake, ili baadaye akiondoka aweze kuzungumzwa vizuri.

Sheikh Othman Maalim, amesema mtu mwenye hekima anajua azungumze vipi na wakati gani, sifa ambazo alikuwa nazo Mzee Mwinyi.

“Alibeba Tanzania katika hali ngumu kulikuwa na uchumi mgumu, Mzee Mwinyi anatajwa kwa mengi, ametengeneza historia na hatumtaji kwa sababu alikuwa Rais wetu, lakini tunamtaja kutokana na busara zake,” amesema.

Amesema hiyo ni mifano mizuri inayotakiwa kuzungumzwa na kufahamika kwa kila mmoja na watoto wadogo wajue.

Sheikh Othman amesema njia nzuri ya kumuenzi ni kuendelea kuyaenzi, kuyafanya na kuziiga tabia za Mzee Mwinyi; “tunajua kuvaa viatu vya mzee itakuwa ngumu lakini japo kwa kujifananisha naye kwa uchache.”

Kaulimbiu inayoishi

Katika hatua nyingine, kaulimbiu ya Mzee Mwinyi kwamba; "Zanzibar ni njema, kila atakaye na aje" ni moja ya mambo ambayo Wazanzibari wanayakumbuka kutoka kwa kiongozi huyo aliyekuwa Rais wa Zanzibar kwa miezi tisa tu kati ya mwaka 1984 hadi 1985.

Mzee Mwinyi aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 98, ndiye Rais wa Zanzibar aliyetawala kwa muda mfupi zaidi baada ya kujiuzulu aliyekuwa Rais wakati huo, Abdul Jumbe na alitoka mwaka 1985 baada ya kuteuliwa na CCM kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akiwa Rais wa Zanzibar, anakumbukwa kupitia kaulimbiu ya "Zanzibar ni njema, kila atakaye na aje" iliyokuwa na lengo la kufungua mipaka ya nchi hiyo kwa kukaribisha wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani hasa wafanyabiashara kutoka Bara.

Ni katika kipindi hicho Serikali yake iliondoa masharti ya matumizi ya pasi za kusafiria kwa watu wanaotoka Tanzania Bara, jambo ambalo liliongeza mwingiliano na hasa kwa wafanyabiashara.

Falsafa hiyo ya Mzee Mwinyi ilipata umaarufu zaidi baada ya msanii wa muziki visiwani hapa, Siti Binti Saad kutunga wimbo maalumu wa kukaribisha wageni Zanzibar kutokana na mabadiliko makubwa na fursa zilizopo.

Wazanzibari wamezungumzia hilo kama jambo kubwa ambalo Mzee Mwinyi aliwafanyia wakati wa uongozi wake na wanamkumbuka kwa kuanzisha mageuzi yaliyochochea ukuaji wa uchumi wa Zanzibar.

Mkazi wa Kiembe Samaki, Ashura Mohamed Sadik amesema Mzee Mwinyi ndiye alianza kuitangaza Zanzibar duniani kwa kuwaita wageni hadi leo inapokea watalii wengi na wafanyabiashara wanaokuja kuwekeza visiwani hapa.

"Nakumbuka wakati ule tulikuwa tunaomba 'Zanzibar ni njema atakaye na aje', hiyo ilikuwa maneno ya Rais wetu (Mwinyi) akihamasisha wageni kuitembelea Zanzibar. Na kweli mambo mengi yalibadilika wakati huo," amesema.

Amesema kiongozi huyo amejaliwa umri mrefu kutokana na mambo mema aliyoyafanya kwa wananchi wake na anaamini angepata muda mrefu wa kuiongoza Zanzibar angefanya mengi zaidi.

Mkazi wa Magomeni, Nurdin Ally Said amesema watamkumbuka Mzee Mwinyi kwa uwezo wake wa kufungua mipaka si tu Zanzibar, bali pia Tanzania kwa ujumla, jambo ambalo lilileta mafanikio makubwa katika Taifa.

"Wazee wametueleza mengi kuhusu mzee huyu, hasa alivyokaribisha wageni kutoka nje ya Zanzibar, na hiyo ilikuwa muhimu kwa sababu wanasema hali ya uchumi ilikuwa mbaya sana hapa Zanzibar," amesema Said.

Hussein Hassan Bilal, mkazi wa Mji Mkongwe, amesema Mzee Mwinyi amekuwa Rais wa Zanzibar kwa muda mfupi lakini aliweza kutatua tatizo sugu lililokuwa likiwakabili wananchi la kudorora kwa uchumi kulikotokana na nchi kujifungia kwa sera zake.

"Wimbo maarufu wa Siti Binti Saad wa 'Zanzibar ni Njema' uliakisi falsafa ya Mzee Mwinyi ambaye wakati huo alikuwa akiifungua Zanzibar kwa kuita wageni na kama mnavyojua, mgeni haji mikono mitupu, analeta kitu. Hapo ndipo Wazanzibari tulineemeka," amesema.