Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mvua sabababisha adha ya usafiri wananchi Zanzibar

Baadhi ya abiria katika kituo cha daladala Bububu Kwanyanya wakiwania usafiri, hali iliyosababishwa na kuendelea kwa mvua iliyochangia  uhaba wa daladala kila sehemu. Picha na Zuleikha Fatawi

Muktasari:

  • Kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini imekuwa changamoto kubwa ya kuharibika miundombinu na shida ya usafiri.

Unguja. Kufuatia mvua zinazoendela kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini zimeendelea kuwaathiri wananchi kwa kuwaumiza na kuwatia hofu hususani katika suala la usafiri kwani imekuwa changamoto kubwa na inayoliliwa kila sehemu kipindi hichi.

Wakizungumza na Mwananchi Digital leo, Novemba 14, 2023 kwa nyakati tofauti wamesema kipindi hichi cha mvua usafiri umekuwa wa mateso kwao kwa sababu ni mgumu hasa nyakati za asubuhi na jioni.

Akizungumzia adha hiyo, mkazi wa Magogoni Kidatu, Fat-hiya Ameir amesema usafiri umekuwa changamoto kwao husuani nyakati za asubuhi ambapo muda huo wengi wanajiandaa kuelekea kazini kutekeleza majukumu ya kitaifa.

"Umejiandaa kwenda kazini unafika kituo cha daladala hamna usafiri hapo  inakupasa usubirie na unaweza kuchukuwa saa mbili au tatu hakuna daladala inayotokea hadi unafanya maamuzi ya kutembea kwa miguu," amesema Fat-hiya.

Pia, amesema muda wa jioni kwa upande wao imekuwa shida kwani wanakuwa wametoka kazini wanataka kuelekea nyumbani pia inakuwa kikwazo na kuwafanya kusubiria kwa muda mrefu.

Mkazi wa Mangapwani, Khattabi Khamis ameeleza kuwa kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha zimesababisha ugumu wa upatikanaji wa usafiri hasa kutoka shamba kuja mjini kwani barabara nyingi zimekuwa na mashimo kiasi ambacho gari kufika sehemu husika inachukua muda.

"Mvua zinasababisha msongamano wa magari barabarani kwa sababu maji yanakaa katika maeneo hayo ambayo  yanachelewesha usafiri kufika katika vituo vyao na wengine kuondosha usumbufu huo mara nyingi wanaishia njiani na kuona bora walaze magari," amesema Khattabi.

Ameongezea kuwa, baadhi ya makonda na madereva wanalichukulia suala hili la mvua kama fursa kwao kwa kukatisha ruti huku mvua ikiwa ndiyo kisingizio cha kutofika katika vituo vyao.

Amesema hili nalo linawaumiza abiria wengi kwani ni kawaida yao hata siku ambazo hakuna mvua kuwa na mtindo huo na abiria yeyote atayeguswa na hili basi anaishia matusi kutoka kwa makonda na madereva.

"Hii ya kukatisha ruti wanafanya hata kama sio kipindi cha mvua saivi wamepata sababu, hii inatokana na kukosa huruma pamoja na nidhamu ya kazi yao, ukinyanyua mdomo kuzungumzia hili basi kauli mbovu Ndio jawabu analopewa abiria," amesema Khattabi.

"Hii changamoto kubwa kwani inasababisha abiria kuchelewa kazini, wakati mwengine unamshusha mtu ni mgonjwa anapata shida ya kutembea umbali kuchukua usafiri mwengine ili kuwahi sehemu husika," amesema.

Khattabi ametoa wito kwa mamlaka husika kuchukua hatua na jitihada za dharura ikiwemo kutia vifusi vizito katika maeneo yenye mashimo barabarani kwa ajili ya kuzuia uharibifu usiendelee kuongezeka.

Dereve wa daladala za Nungwi, Ali Juma amesema mvua zinazonyesha zinawaathiri zaidi wao wenye daladala za shamba kwani abiria wanapatikana kwa shida kwa hiyo inawabidi wakubali kupata hasara kwa kuchukua wachache waliopo au walaze gari kuepusha hasara.

Dereve huyo amesema Licha ya kuwa abiria hawaonekani vituoni lakini foleni hasa njia ya Bububu ndio kilio kikubwa kwao kwani inatoa ari na nguvu ya utendaji kazi.

"Natoka Nungwi shamba mtu unajipa moyo kupiga zaidi kwa siku ila ukifika Bububu Skuli ile ari yote inaishia na kipindi  hiki cha mvua imezidi na madereva ndiyo tunaoumia kwa kweli unang'ang'ana kubana breki mara ufunge, serikali wangeangalia barabara hii," amesema Ali.

Amesema ubovu wa miundombinu ya barabara inachangia kwa kiasi kikubwa kuathirika kwa gari kwani kawaida matope yanaganda katika gari hivyo inatakiwa kila baada ya siku tatu ioshwe.

Dereve wa Kinuni, Abdul-Wahid  Ali Hassan amesema changamoto kubwa inakuja kwenye barabara, mashimo ni mengi na ukizingatia zinafanyiwa matengenezo kwa hiyo hilo linachangia foleni.

Dereve huyo ameiomba Serikali kuboresha miundombinu hususani barabara zilizokaribu na mabwawa kwa kuwekewa uzio maalumu ili mvua zinaponyesha maji yasitoke kwenye mabwawa na kukatiza barabarani.