Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwinyi: Tumeweka kipaumbele kuhifadhi maeneo ya kihistoria

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi (kulia), akizungumza na Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Marjo Crompvotes, alipofika Ikulu ya Zanzibar kwa mazungumzo maalumu Aprili, 2026.

Muktasari:

  • Uhifadhi huo unaenda sambamba na kukarabati majengo ya kihistoria katika eneo la Mji Mkongwe Unguja, Zanzibar

Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema imeweka kipaumbele katika kuimarisha na kuhifadhi maeneo ya kihistoria kwa kuzingatia umuhimu wake katika uchumi na uhifadhi wa utamaduni wa Zanzibar.

Kauli hiyo imetolewa leo Aprili Mosi 2026 na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alipokutana na Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania, Marjo Crompvoet, aliyefika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo maalumu.

Akizungumzia hatua hiyo, Rais Mwinyi ameeleza kuwa ukarabati mkubwa unaoendelea katika jengo la Sinema ya Majestic lililopo Vuga unafanyika chini ya ushirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Japan, ukiwa na lengo la kulibakisha katika mwonekano wake wa asili na kulifanya kuwa endelevu.

"Kukamilika kwake kutachochea kufanyika kwa matamasha mbalimbali ndani ya jengo hilo," amesema.

Rais Mwinyi ameeleza kuwa Serikali ina mipango endelevu ya uhifadhi wa majengo muhimu yenye historia ya muda mrefu, ambayo ni nyenzo muhimu katika kuitangaza Zanzibar na kuimarisha sekta ya utalii, kwani wageni wengi huyatembelea maeneo wanapokuja nchini.

Ameishukuru Uholanzi kwa kuimarisha uhusiano na ushirikiano na Tanzania, ikiwemo Zanzibar katika nyanja mbalimbali pamoja na misaada inayotolewa kuendeleza miradi ya maendeleo nchini.

Ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka Uholanzi kuwekeza nchini, hususani katika sekta za kipaumbele za utalii na uchumi wa buluu kwa ujumla.

Hatua hiyo kwa mujibu wa kiongozi huyo mkuu wa nchi, itachochea ongezeko la watalii kutoka nchi hiyo na kubainisha kuwa Zanzibar bado inahitaji wawekezaji zaidi katika sekta za viwanda, uvuvi na kilimo.

Naye Crompvoet, ameihakikishia Zanzibar kuendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano pamoja na misaada katika sekta mbalimbali.

Ameeleza kufarijika na hatua kubwa za maendeleo ya kiuchumi yanayofikiwa na Zanzibar, ikiwemo ujenzi wa miundombinu mbalimbali, huku akiahidi ongezeko la wawekezaji kutoka nchi hiyo kuja kuwekeza Zanzibar.

Wakati huohuo, Rais Mwinyi amekutana na Balozi wa Slovakia nchini, Ivan Lančarič, aliyefika Ikulu kujitambulisha, akiambatana na Balozi mdogo wa nchi hiyo ambaye kituo chake rasmi cha kazi kitakuwa Zanzibar, Mustafa Khataw.

Katika mazungumzo hayo, Mwinyi ameihakikishia Slovakia kuwa Zanzibar iko tayari kufungua milango ya ushirikiano na kufanya kazi na nchi hiyo katika maeneo mbalimbali ya kiuchumi, uwekezaji, biashara na utalii, pamoja na kuishauri kuitangaza Zanzibar katika soko la utalii la nchi hiyo.

Balozi Lančarič amesema nchi hiyo inatarajia kufungua ofisi ya ubalozi wake nchini Tanzania mapema Juni mwaka huu, hatua itakayokwenda sambamba na ufunguzi wa ofisi ndogo ya ubalozi wake Zanzibar, kwa lengo la kuendeleza ushirikiano.

"Slovakia ina maendeleo makubwa katika uchumi wa viwanda, teknolojia ya utengenezaji wa magari, biashara na uwekezaji," amesema.