Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nini kimeituliza Zanzibar?

Dar es Salaam. Ukiona vyaelea jua vimeundwa, ndivyo unavyoweza kuutumia msemo huu kuelezea maendeleo kwenye sekta mbalimbali visiwani Zanzibar, chini ya utawala wa Rais Dk Hussein Ali Mwinyi, anayetimiza miaka mitatu madarakani siku chache zijazo.

Dk Mwinyi alishinda urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, 2020 baada ya kupata kura 380,402 sawa na asilimia 76.72 dhidi ya mpinzani wake, Maalim Seif Sharif Hamad, aliyepata 99,103, sawa asilimia 19.87.

Dk Mwinyi, ambaye ni mtoto wa Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, aliapishwa kuwa Rais Novemba 2, 2020 akichukua nafasi ya Dk Ali Mohamed Shein, aliyemaliza muda wake wa utawala miaka kumi mfululizo kwa mujibu wa Katiba.

Nani asiyejua miaka saba iliyopita hali ya kisiasa Zanzibar haikuwa ya kuridhisha kama ilivyo hivi sasa licha ya kuwapo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK)?

Wakati Dk Mwinyi anatimiza miaka mitatu madarakani, si jambo la siri kuwa, chini ya uongozi wake kuna maboresho makubwa kwenye uboreshaji wa miundombinu ya barabara, afya, elimu na bandari.

Hata hivyo, kwenye mafanikio pia hapakosi changamoto; ugumu wa maisha unaowakabili Wazanzibari ndilo jambo linalopaswa kuwekewa nguvu kubwa na Rais Mwinyi, viongozi na watendaji wa taasisi za umma.

Katika mahojiano na Mwananchi kuhusu miaka mitatu ya Rais Mwinyi, wachambuzi wa masuala ya kijamii na kisiasa wanamuona kiongozi huyo amejipambanua kujenga umoja, amani na mshikamano kwa wananchi wa kisiwa hicho bila kujali tofauti za itikadi za vyama vyao.

Hata hivyo, wanasema SUK bado inaonekana haijapewa uzito unaostahili kama baadhi ya watu walivyotamani.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM (Zanzibar), Khamis Mbeto anasema katika kipindi cha miaka mitatu Dk Mwinyi ‘ameupiga mwingi’ (amefanya mambo makubwa), katika utekelezaji wa majukumu yake ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Pemba na Unguja.

Mbeto anasema wakati Dk Mwinyi anaingia madaraka Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) walikuwa wanakusanya Sh170 bilioni kwa mwaka, lakini sasa hivi wamefikia hadi Sh449 bilioni kwa mwaka.


Vipi kuhusu siasa

Kuhusu siasa, Mbeto anasema hali ya siasa visiwani humo imeimarika kutokana na utendaji kazi bora wa Dk Mwinyi, aliyewahi kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa nyakati tofauti.

Anasema kinachofanywa na Rais Mwinyi kinaonekana, kilichobaki ni upinzani wa kumwandama yeye binafsi.

“Kazi nzuri inafanyika, ikiwamo uboreshaji ya miundombinu, sasa hivi upinzani umebaki ni kumwandama yeye binafsi, lakini tunaamini Serikali ya Umoja wa Kitaifa ndio suluhisho, sasa hivi Zanzibar imetulia,” anasema Mbeto.


Ilichokisema ACT- Wazalendo

Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo, Juma Duni Haji anasema chama hicho hakiwezi kuzungumza kwa undani kuhusu miaka mitatu ya Rais Mwinyi, bali wanamuachia kiongozi huyo wa Zanzibar azungumze suala hilo, maana ndiye Rais.

“Tumsubiri yeye atazungumza nini, hatutaki tutangulie...lakini matumaini madogo, tulitarajia ndani ya miaka mitatu awe amejenga uhusiano mzuri kwa Wazanzibari, ila imekuwa kinyume tu,” anasema Duni, aliyewahi kuwa Waziri wa Afya Zanzibar.

Kuhusu hali ya maisha Zanzibar, Duni anasema hairidhishi kwa kuwa, wananchi wanaishi katika mazingira magumu, sio Unguja wala Pemba.

Anasema vyakula vimepanda bei na watu wanashindwa kumudu kupata mlo wa mara tatu kwa siku.

“Hapa Zanzibar siasa ni chakula, mchele, unga na sukari, sasa kama mchele wa mapembe unaopendwa na watu wa hali ya chini umepanda bei itakuwaje...,” anasema Duni.

Kuhusu suala la maridhiano, Duni anasema anayestahiki kufanya maridhiano ni yule mtu mwenye nguvu au madaraka ili amridhishe yule asiyekuwa na nguvu.

“Kama hajataka Samia (Rais Samia Suluhu Hassan) na Dk Mwinyi (Hussein) maridhiano yatakuwa yanatamkwa tu, wao ndio wa kuamua, sio sisi (upinzani). Lakini imekuwa sisi kama tunawalazimisha, maridhiano hayaji kwa kulazimisha, bali maelewano na kutekeleza makubaliano,” anasema Duni.

Duni anasema ndani ya miaka mitatu, Dk Mwinyi hajatekeleza maridhiano, hasa utekelezaji wa ahadi alizompa aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad (marehemu) ikiwamo kuachiwa huru na kupewa fidia watu wote waliokamatwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

“Tulimpelekea namna ya muundo wa maridhiano unavyopaswa kuwa lakini hajatejeleza hadi sasa...” anasema Duni.


Wachambuzi wa siasa

Mchambuzi wa siasa, Ali Makame anasema ni wazo zuri Serikali kujenga vituo vya afya kila wilaya, lakini baadhi ya watu wanahoji kama kweli kuna umuhimu wa kuvijenga kulingana na ukubwa na wingi wa watu visiwani humo.

“Lakini wananchi pia wana wasiwasi je, vipimo vitakuwepo kama zamani? Kwa sababu hadi sasa vituo vingi havijafunguliwa kutokana na vifaa. Jambo jingine ni ujenzi wa nyumba za makazi, zinazojengwa wananchi wa chini hawawezi kuzimudu kabisa kutokana na gharama kubwa za ununuzi.

“Ujenzi wa barabara za ndani ukikamilika utaleta taswira nzuri za miji, lakini bado kuna malalamiko kuhusu zabuni zilivyotolewa, hali inayodaiwa kumfanya Balozi Ali Karume kuvuliwa uanachama wa CCM. Lakini kumekuwa na malalamiko kuhusu ukarabati wa uwanja wa ndege wa Amani umetumia fedha nyingi.

“Wananchi wanasema hakukuwa na haja, bora ungejengwa uwanja mpya na ule ungebaki kama kumbukumbu. Lakini ukweli bado upo pale pale, mchakato huu umekuwa na malalamiko ikiwamo kwa Balozi Karume,” anasema Makame.

Hata hivyo, Makame anasema malengo aliyojiwekea Dk Mwinyi ya miaka mitano, ikiwamo kuboresha miundombinu ya Pemba na Unguja ikifanikiwa italeta picha na taswira nzuri ya visiwa hivyo.

Anasema pamoja na mipango hiyo mizuri, hali ya maisha sio nzuri kwa Wazanzibari.

“Kupanda kwa bei ya mafuta, ingawa kuna falsafa ya uchumi wa buluu, bado haujawafikia wananchi na kuona faida yake. Mlo wa mara mbili au mara tatu kwa siku kuupata wananchi wa Zanzibar ni kazi sana, kuna haja kwa Rais Mwinyi kuongeza na kuboresha suala la kilimo,” anasema Makame.

Katika hatua nyingine, Makame anasema SUK ni kama vile haipo, kwa kile alichodai Serikali ya Umoja wa Kitaifa haiwezi kuendeshwa kwa mawaziri wawili, akisema sheria haimzuii Dk Mwinyi kuchukua watu wengine kutoka vyama vya upinzani kuingia katika Serikali kama alivyofanya mtangulizi wake, Dk Ali Mohamed Shein.

“SUK ya sasa Makamu wa Kwanza wa Rais (Othman Masoud) anainadi Serikali, lakini watendaji wa ACT wakikaa kwenye majukwaa wanaiponda na kuilamu Serikali, hapa bado kizungumkuti,” anasema Makame.

Mawazo ya Makame hayana tofauti na Enzi Talib, akisema, “SUK inakwenda kama vile unafiki...viongozi wa ACT wanapokuwa ndani wanazungumza vingine na wanafuata sera zake, lakini wakiwa nje wanakuwa lugha tofauti na kuwachanganya Wazanzibari,” anasema Talib.

Talib, ambaye ni mchambuzi mwingine, anasema ndani ya miaka mitatu Dk Mwinyi amejitahidi kuipeleka mbele Pemba, iliyoonekana kama imesahaulika na ipo nyuma kimaendeleo.

Anasema Dk Mwinyi amejitahidi kuwaunganisha Wazanzibari, hasa falsafa yake ya kupita misikitini.

“Ingawa wengine wanaiponda wakisema kujikita na falsafa za misikiti ni kuwapa fursa wale wapinzani wa ndani yake kupiga vita kutumia nyumba hizo za ibada.Upande mmoja amefanikiwa, lakini anapata upinzani Unguja na sio Pemba,” anasema Talib.

“Katika SUK, Dk Mwinyi amejitahidi, lakini anakabiliana na upinzani ndani ya CCM, hasa wale wanaotoka Unguja. Nia ya Dk Mwinyi ni nzuri, lakini waliozoea kutotaka mabadiliko, hasa ndani ya CCM wanataka mambo yawe yaleyale ndio maana wanampinga kwenye maeneo hayo.”