Prime
Safari ya siku 1,096 za Dk Mwinyi madarakani
Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi akiapa kushika nyadhifa hiyo. Picha na Maktaba
Dar es Salaam. Novemba 02, 2020 baada ya kuapishwa na Jaji Mkuu wa Zanzibar Othman Omar Makungu, Rais Hussein Mwinyi ambaye alitumia dakika mbili kuapa, alitoa mwelekeo wa itakayokuwa Serikali yake.
Hotuba ya Dk Mwinyi aliyoitoa siku hiyo katika Uwanja wa Amani Zanzibar, ilikuwa ya dakika 14, aliahidi kushirikiana na watu wote kuijenga Zanzibar na kuunda Serikali ya uwazi, inayowajibika na yenye usawa.
"Nawapongeza wagombea wenzangu kwa nafasi ya urais kwa kuyapokea matokeo na kuyakubali na ninaahidi kushirikiana nao katika Serikali nitakayoiunda ili kujenga Zanzibar mpya," alisema Rais Mwinyi aliyezaliwa tarehe 23 Desemba 1966.
Alisema lengo ni kuijenga Zanzibar mpya ambayo sanjari na kuenzi na kuendeleza pale alipoisha mtangulizi wake (Dk Ali Mohammed Shein), pia ataendeleza maridhiano ya mshikamano wa Wazanzibari.
“Serikali nitakayoiunda itakuwa ya uwazi, uwajibikaji na usawa bila kubagua mtu kwa rangi au eneo analotoka, ambayo itazingatia "nidhamu kwa watumishi, itakayokuwa na kazi kwa kuimarisha huduma za kijamii,” alisema.
Hotuba yake hiyo haikuwa na ujumbe tofauti na vipaumbele alivyokuwa akivitaja katika kampeni zake kwani wakati akiomba kura kwa wananchi aliahidi kupambana na rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma.
Vilevile alieleza kuwa akipewa ridhaa ataboresha mazingira ya sekta ya utalii ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Zanzibar pamoja na kuwanyanyua wajasiriamali na wanawake visiwani humo.
Dk Mwinyi ambaye kitaaluma ni daktari wa binadamu alitangazwa mshindi wa nafasi ya urais Zanzibar kwa asilimia 76. 27 huku mpinzani wake, Maalim Seif akiwa mshindi wa pili kwa asilimia 19.87.
Maisha yake ya uongozi kabla ya urais na pengine sasa watu walikuwa wakimwelezea Dk Mwinyi kama mwanasiasa msiri, mkimya na wakati akiomba ridhaa ya kuiongoza Zanzibar alitumia kaulimbiu "Yajayo ni neema tupu."
Novemba 2, Dk Mwinyi atatimiza miaka mitatu madarakani tangu aanze kuiongoza Zanzibar, kueleka jubilee hiyo Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa kushirikiana na Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) wameandaa kongamano la kuangazia hali ya mambo ilivyo kipindi hicho cha siku 1,096.
Kongamano hilo linatarajiwa kufanyika Oktoba 31, 2023 katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Zanzibar Airport kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa sita mchana, mada itakuwa Miaka mitatu ya Dk Hussein Mwinyi; Mafanikio, fursa na changamoto.
Mwananchi itatumia chapa yake ya Mwananchi Jukwaa la Fikra (MTLF) na hilo litakuwa ni kongamano lake la 14 kufanyika tangu kuanzishwa kwake lakini la kwanza kufanyika Zanzibar.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Oktoba 9, 2023 kuhusu tukio hilo, Mkurugenzi Mkuu wa MCL, Bakari Machumu alisema kongamano hilo litawaleta pamoja wadau, wanazuoni na jamii kwa ujumla ili kufurahia mageuzi ya serikali hiyo.
"Pia tutatafuta ufumbuzi wa pamoja wa changamoto mbalimbali zinazojitokeza. Katika hili tumejipanga kuwawezesha wananchi kushiriki katika majadiliano hayo yanayolenga kuainisha mafanikio yaliyo dhahiri katika nyanja mbalimbali,” alisema.
Baadaye akihojiwa na ZBC, Machumu alisema lengo la kuandaa kongamano la miaka mitatu ya Rais Mwinyi ni kuleta uelewa kwa wananchi ili wajue nini Serikali yao inafanya, washiriki ili waweze kuziona fursa na wasiwe mabingwa wa kuelezea changamoto.
Machumu alisema MCL inaamini wananchi wakijua fursa zilizopo itakuwa ni rahisi kwao kufahamu wanapata nini katika kile kinachofanyika na mabadiliko mengi yameshuhudiwa.
"Ukizungumza na watu wanasema tunaona Zanzibar imezungushiwa mabati, ikatupa sisi hamu ya kutaka kujua ni nini kinaendelea, tukielezee katika eneo hilo la maendeleo, ndiyo dhima yetu kwamba tulete makundi hayo mbalimbali yajadili kwa undani," amesema Machumu.
Alisema Serikali ya Dk Mwinyi itaelezea ilikuwa na ndoto gani na wamefanya nini, wako wapi, wamekwama wapi na nini wanakwenda kufanya baadaye.
"Wananchi waulize mbona katika vitu mnavyofanya mbona hapa hamjatupa kipaumbele, mbona hapa pameachwa, hapa hapajafanywa vizuri, mwisho wa siku kunakuwa na mjadala ambao watunga sera na watekelezaji wanapata mrejesho wa moja kwa moja kutoka kwa wananchi na wadau wote ili kuboresha kwa manufaa ya kila mtu," alisema Machumu.
Katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Zanzibar ambaye pia ni Msemaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Charles Hilary alisema waandishi wa habari wana jukumu kubwa kueleza mafanikio yaliyopatikana kwa kipindi kifupi cha utawala wa Rais Mwinyi.
Mkurugenzi huyo alisema ipo haja vyombo vingine vya habari kubuni na kuendelea kutangaza, akisema Serikali ya Mapinduzi ipo tayari kukosolewa ikiwa kuna nia ya kutaka kujenga.
Aliwataka kuendelea kuwa macho na masikio ya wananchi wa Zanzibar na duniani kueleza yanayofanyika na mengine yanayoendelea kufanyika Zanzibar.
Mkurugenzi wa ZBC, Ramadhan Bukini alisema kuelekea maadhimisho ya miezi 36 ya Dk Mwinyi watatoa fursa kwa mashirika na wizara za Zanzibar kila Jumapili kuzungumzia mafanikio yaliyofikiwa katika kipindi hicho.
“Tunafanya hivyo kwa sababu kuna vitu vingi vimefanyika na kuna watu wengi watashiriki, kwa hiyo watapewa nafasi kuzungumza na pia tutaandaa makala mbalimbali kwenye redio na televisheni na kwenye magazeti kwa kushirikiana na Mwananchi na pia tutaandaa vipindi maalumu,” alisema.
Upande wa MCL kuanzia leo kupitia magazeti yake ya Mwananchi, The Citizen, Mwanaspoti, YouTube Mwananchi Digital ya mitandao yake ya kijamii itakuwa ikichapisha maudhui yahusuyo safari ya Dk Mwinyi ikiangazia fursa, mafanikio na changamoto.
Usikose kufuatilia kila siku mfululizo wa Makala zihusuzo miaka ya mitatu ya Rais Mwinyi katika nyanja za kijamii, kiuchumi, kisiasa, kitamaduni, sanaa na kimichezo. MCL tunaliwezesha Taifa.