Zanzibar yadhibiti wafanyakazi hewa kidijitali

Muktasari:
- Mifumo mbalimbali ya kidijitali imeundwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa lengo la kurahisisha huduma ili kuendana na kasi ya kiuchumi, iliyosaidia katika maeneo mengi ikiwemo udhibiti wa mianya ya rushwa na ubadhirifu.
Dar es Salaam. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetaja faida mojawapo ya mifumo ya Serikali ni kuzuia uwapo wa watumishi hewa na kudhibiti mapato na matumizi ya Serikali.
Faida hiyo imetokana na mifumo mbalimbali ya kidijitali iliyoundwa ukiwemo mfumo huo uitwao ‘HR Payroll’ ambao umeweza kudhibiti mianya yote ya malipo hewa Serikalini na kudhibiti rushwa na ubadhirifu.
Hayo yamesemwa leo Jumapili Oktoba 15, 2023 na Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Serikali Mtandao Zanzibar, Said Seif Said katika kipindi maalum kinachorushwa na runinga ya ZBC kwa kushirikiana na Mwananchi Communications Limited (MCL) kuelekea Jukwaa la Fikra litakalojadili miaka mitatu ya Rais wa Zanzibar, Hussein Ali Mwinyi.
“Hapa kulikuwa na watumishi hewa, lakini utawagundua vipi mfumo unajua na umeanza kutupa suluhisho tukipitisha huko inaonyesha huyu analipwa mara mbili, huyu hayupo kwa sasa kuna mabadiliko makubwa,” amesema.
Amesema mfumo huo umeisaidia Serikali kwani unarahisisha pia ukaguzi, “Tunapokuja kwenye ukaguzi mifumo ya zamani ilikuwa shida, unapofika baadhi ya sehemu mtaalamu hakupi taarifa zile zinazohitajika zote.”
Said amesema hata wanapotengeneza mifumo yote wanahakikisha kunakuwa na usalama wa hali ya juu kama ilivyo katika mfumo wa Zan Ajira ambao unamlazimu kila Mzanzibar anayehitaji ajira ajiandikishe huko.
“Mfumo huu upo na manufaa yake tumeyaona kwani kila kitu kipo wazi na uwazi ndiyo utatufikisha pale tunapopataka,” amesema Said na kuongeza kuwa taasisi yoyote inapotaka kufanya mabadiliko ya kidijitali inashirikiana na serikali na kwamba tayari mifumo mingi imeanzishwa ikiwemo Zan-Malipo kwa ajili ya kukusanya mapato yote ya Serikali ukiwemo na ule wa E-procurement.
Katika hatua nyingine amesema ili kuendana na kasi ya kiuchumi haiwezi kukwepa maendeleo ya kidijitali, hivyo inakusudia kuja na mfumo wa malipo mtandao wa Serikali yaani National QR Code.
Amesema utatuzi huo unafuatia changamoto kubwa ya Zanzibar kuwa na watalii wengi wanaotoka katika nchi zilizoendelea kidijitali.
“Mtalii anakuja ana kadi, Mzanzibar anauza vitu vizuri mtalii anataka kununua inakua shughuli pale anapotaka kulipa akimpa kadi, anamwambia nenda kanitafutie fedha taslimu hayo mambo tunataka kuyaacha.
“Tunataka sehemu yoyote inayofanya hivyo tuwawezeshe hawa wenzetu wapate kipato kupitia National QR Code mtalii anakuja analipa wamemalizana, mwananchi amefanya biashara yake huo ni ushirikishwaji wa kifedha, tunakuja hivyo ili kila mmoja aweze kupata faida ya haya mabadiliko ambayo Serikali ya awamu ya nane inayaleta Zanzibar,” amesema Said.
Amesema mabadiliko mengi yamefanywa kulingana na utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi CCM ambayo ilinadiwa na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.
Amesema lengo la Wakala wa Serikali mtandao ni kuhakikisha inaleta mabadiliko kwa kutumia Tehama katika kuleta huduma kwa jamii ipatikane kwa urahisi ili mwananchi aweze kufanya shughuli zote kwa urahisi ziwe za kiserikali au kijamii.
“Lengo jingine kuu ilikuwa ni kuhakikisha mapato yanapatikana kwa ajili kuleta maendeleo kwa kutumia ubunifu na kuja na vyanzo vya mapato ambavyo ni vipya na kwa ubunifu, kwa kuangalia mwananchi ana shida na kero gani anayo, tutatue kwa kuleta suluhisho,” amesema.
Amesema mifumo hiyo imeleta tija katika kila mfumo kuanzia katika ofisi za Serikali, kijamii na katika huduma za walimu na masuala ya afya kwamba kwa sasa hakunamafaili ya makaratasi na kumbukumbu za wagonjwa zinatunzwa kidijitali.
Hata hivyo amesema jukumu lililo mbele ni kuhakikisha mifumo hiyo inakuwa endelevu, “Ili kuleta mabadiliko lazima kuwe na uendelevu isiwe leo imefanya kazi, kesho haijafanya kazi hasa pale inamfanya mwananchi arudi kulekule kwa zamani.”
Amesema ili kuhakikisha hilo linawezekana ni kuhakikisha mifumo hiyo inajaribiwa wakati wote na pale kutakapokuwa na changamoto basi itatuliwe, “Lazima uwe na timu imara wakati wote kunapokuwa na changamoto yoyote au tushirikiane na timu husika kama kosa limefanyika kuhakikisha halirudiwi tena.”