Rais Mwinyi amueleza Tony Blair kipaumbele cha Serikali yake

Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema licha ya uchumi wa buluu kujumuisha sekta tano, utalii ni kipaumbele chake cha kwanza kwenye mnyororo wa sekta hizo kwani unachangia asilimia 30 ya pato la taifa tofauti na sekta nyingine za maendeleo.
Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Oktoba 5, 2023 Ikulu, Zanzibar alipozungumza na Waziri Mkuu wa Zamani wa Uingereza, Tony Blair aliyefika na ujumbe wake.
Dk Mwinyi alimueleza Blair kwamba Zanzibar ina utalii wa asili wa fukwe na urithi lakini kwa sasa inahitaji kwenda mbali kuboresha utalii wake kwa kuangalia zaidi utalii wa mikutano na michezo.
Sekta nyingine za uchumi wa buluu ni Bandari ambayo inamchango mkubwa wa uchumi wa Zanzibar na ina mahitaji ya uwekezaji kwenye eneo hilo hasa bandari jumuishi itakayotoa huduma zote ikiwemo kuruhusu meli kubwa kushusha na kupakia mizigo mingi ya vyakula, nafaka, mafuta na mahitaji mengine ya uchumi.
Dk Mwinyi amesema kwakuwa Zanzibar imezungukwa na bahari, sekta ya usafirishaji ni muhimu kwa uchumi wake hivyo inahitaji uwekezaji mkubwa ili kuimarisha usafiri wa majini kwa abiria na mizigo.
Kuhusu sekta ya Mafuta na gesi, Rais Dk Mwinyi alimueleza Waziri Mkuu huyo wa Zamani wa Uingereza kwamba Zanzibar inahitaji uwekezaji mkubwa ili kuimarisha sekta ya biashara na uchumi kupitia bandari.
Dk Mwinyi alieleza, ushirikiano uliopo baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na taasisi ya Tony Blair hasa kwenye miradi mbalimbali ya huduma za jamii ikiwemo elimu na afya.
Naye Blair ambaye pia ni Mwenyekiti wa taasisi ta Tony Blair (TBI) alisifia uzuri kisiwa cha Zanzibar kilivyobarikiwa kuwa na haiba na mwambao mzuri wa kumvutia kila mgeni na kwamba Zanzibar imejijengea sifa duniani ya kuwa na vivutia vizuri vya utalii.
Pia aliishauri Serikali kuongeza mvuto zaidi kuendelea kukipatia sifa nzuri kisiwa cha Pemba kwani ni bahati kubwa kwa Zanzibar kuwa na kisiwa kizuri kama hicho ambacho ni mfano mzuri wa kivutio cha utalii duniani.
Tony Blair ni mwanasiasa mkongwe nchini Uingereza aliyehudumu nafasi ya Uwaziri mkuu tangu mwaka 1997 hadi 2007 anakua Waziri Mkuu wa pili kuongoza nafasi hiyo kwa muda mrefu Uingereza baada ya Magret Thatcher aliyehudumu nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka 11.