Rais Mwinyi: Mapambano ya rushwa yasiangalie taasisi
Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Sulaiman Abdulla akizungumza kwa niaba ya Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi katika maadhimisho ya kupambana na rushwa Afrika yaliyofanyika Unguja Zanzibar
Muktasari:
- Katika mapambano dhidi ya rushwa na uhujumu uchumi nchini, hatua mbalimbali zimechukuliwa, ikiwamo kuanzishwa kwa Tume za Maadili ya Viongozi wa Umma, kuanzishwa kwa taasisi maalumu za kupambana na rushwa pamoja na kuimarisha sheria
Unguja. Serikali imesema pamoja na kuimarisha mifumo ya kisheria na kitaasisi ili kukuza uadilifu na kupambana na rushwa nchini, jukumu hilo linapaswa kusimamiwa na kila mmoja badala ya kuziachia taasisi zinazohusika.
Hayo yameelezwa leo Jumamosi Julai 11, 2026 na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, kupitia hotuba yake iliyosomwa na Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla, katika hafla ya maadhimisho ya Siku ya Mapambano Dhidi ya Rushwa Barani Afrika, yaliyofanyika Unguja, Zanzibar.
Amesema katika mapambano dhidi ya rushwa na uhujumu uchumi nchini, hatua mbalimbali zimechukuliwa, ikiwamo kuanzishwa kwa Tume za Maadili ya Viongozi wa Umma, kuanzishwa kwa taasisi maalumu za kupambana na rushwa pamoja na kuimarisha sheria.
Miongoni mwa sheria hizo ni Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sura ya 398 ya Tanzania Bara, na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 4 ya mwaka 2015 ya Zanzibar.
"Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya mwaka 2007 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar Na. 5 ya mwaka 2025 zimeimarishwa sambamba na Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 2 ya mwaka 2025 na Sheria ya Ukaguzi wa Umma Na. 7 ya mwaka 2025," amesema.
Amesema Tanzania inaendelea kuhakikisha mikataba yote ya kikanda na kimataifa inayohusu mapambano dhidi ya rushwa inatekelezwa ipasavyo kwa manufaa ya wananchi na maendeleo ya Taifa.
Amesema kupitia uimara huo, Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (Zaeca) imeokoa na kurejesha hazina ya Sh5 bilioni pamoja na Dola 398 za Marekani kuanzia Julai 2025 hadi Mei 2026, zilizopatikana kutokana na kudhibiti ubadhirifu, ukwepaji wa kodi na matumizi mabaya ya madaraka.
Pamoja na hayo, Rais Mwinyi amesema mapambano dhidi ya rushwa si jukumu la Zaeca na Takukuru pekee, bali ni wajibu wa kila mmoja kusimamia uadilifu, uwazi na uwajibikaji katika kutekeleza majukumu yake kulingana na nafasi aliyonayo.
Amesema ushirikiano kati ya wananchi, viongozi, sekta binafsi na taasisi za kiraia utawezesha kushinda vita dhidi ya rushwa.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (Zaeca), Ali Abdalla Ali, amesema katika kufikia adhima ya Dira ya Maendeleo ya Zanzibar katika kudhibiti rushwa na uhujumu uchumi, nguvu za pamoja zinahitajika ili kuwa na Taifa salama lisilo na mianya ya rushwa na uhujumu uchumi.
Ali amesema Zaeca kwa kushirikiana na Takukuru wanafanya kazi kwa pamoja ili kuendelea kutoa huduma bora zisizo na malalamiko ya uwepo wa rushwa na uhujumu uchumi nchini.
Akitoa salamu za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Crispian Chalamila, amesema rushwa na uhujumu uchumi vimekuwa vikwazo vikubwa katika jamii na vimesababisha athari mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
"Hivyo, juhudi za pamoja zinahitajika katika mapambano dhidi ya rushwa," amesema.
Mapema, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Umoja wa Afrika ya Kupinga Rushwa, Ivona Achibia, amesema wakati umefika kwa taasisi za kupambana na rushwa kutoa elimu zaidi kuhusu mapambano dhidi ya rushwa kuanzia ngazi za chini na kuifikia jamii moja kwa moja ili iwe na uelewa mpana kuhusu athari za kutoa na kupokea rushwa.