Rais Mwinyi: Ujenzi barabara, hoteli umeongeza thamani ya ardhi Z'bar
Rais wa Zanzibar wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi akizungumza wakati wa kilele cha wiki ya ardhi Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja
Muktasari:
- Hivyo amesema zinahitajika jitihada za makusudi kushughulikia changamoto hizo na kuzuia ujenzi holela katika maeneo ambayo hayahusiki.
Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema ujenzi wa barabara na hoteli unaoendelea kisiwani humo vinachangia ongezeko la mahitaji makubwa ya ardhi hatua inayoweza kuchochea migogoro ya ardhi zisipochukuliwa hatua.
Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Jumapili Juni 28, 2026 wakati akihitimisha kilele cha wiki ya ardhi awamu ya pili tangu ilivyoanzishwa programu hiyo mwaka jana.
Amesema ardhi ya Zanzibar inazidi kuongezeka thamani na kupungua kutokana na ujenzi mkubwa unaoendelea.
"Kwa hiyo msipokuwa waangalifu, migogoro hii itazidi mno. Mimi nafurahi kwamba sasa tunakuja na mfumo mkubwa wa Laris ambao ndio utakuwa ufumbuzi wa matatizo yaliyokuwa miaka mingi yaliyopita," amesema.
Amesema katika mazingira yaliyokuwapo eneo moja linatolewa haki zaidi ya moja, kuna maeneo yana hati mpaka tatu, eneo hilohilo moja, kwa sababu ya kukosekana mfumo.
"Sasa mfumo huu, ukishatoa hati moja, hautaweza kutoa nyingine. Mifumo hii itahakikisha kila mwenye kustahili kupimiwa na kupata haki yake, ili ajiendeleza kimaisha na kiuchumi," amesema.
Amesema hatua zinazopaswa kuchukuliwa ni kudhibiti ujenzi holela na maeneo ambayo hayaruhusiwi; Watu wasijenge viwanda kwenye maeneo ya makazi, kilimo, wasijenge hovyo kwenye maeneo ya viwanda, pembezoni kwenye hifadhi ya barabara, hayo yote yatawezekana kupitia mradi huu.
Hata hivyo amepongeza kamisheni ya ardhi na Shirika la Nyumba kutokana na jitihada wanazofanya kuhakikisha Zanzibar inaondokana na migogoro ya ardhi na makazi bora.
"Haijawahi kutokea katika historia ya Zanzibar, ujenzi wa nyumba nyingi za makazi kama inavyoendelea hivi sasa. Bila shaka baada ya muda mfupi ujao, tutaweka utaratibu mzuri wa kuwawezesha wafanyakazi wote wa Serikali kumiliki nyumba zao kupitia hatua hizi," amesema.
Amesema idadi ya watu Zanzibar inaongezeka ambapo kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, kuna watu 1.8 milioni huku ikikadiriwa kufika mwaka 2050 watakuwa wamefikia watu 3.6 milioni.
Amesema ardhi inazidi kupungua hivyo kutaka kuendeleza mipango ya kujenga nyumba na kuwauzia wananchi na kuacha na mpango wa kujenga nyumba kwa muda mrefu.
Matumizi bora ya ardhi kwa mujibu wa Dk Mwinyi yanatokana na kuwa na mipango bora na endelevu ambayo itabainisha kupata na umiliki kulingana na aina ya matumizi kwa kila eneo.
"Kwa muktadha huo, Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi ina jukumu kubwa la kusimamia serikali na kuhakikisha ardhi zote zinaratibia, zinapimwa, zinapangwa, na zinasajiliwa pamoja na kutoa kadi za hati ya matumizi ya ardhi kwa wanao stahiki," amesema.
Mapema Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Rahma Kassim Ali amesema licha ya changamoto kubwa za ardhi, lakini sekta hiyo imepiga hatua ikilinganishwa na kipindi cha miaka mitano nyuma.
Amesema kuna ongezeko la mapato, kwani wakati Dk Mwinyi anaingia madarakani walikuwa wanakusanya Sh5 bilioni kwa mwaka lakini sasa wanakusanya Sh25 bilioni.
"Imani yetu tutaendelea kufanya vizuri mpaka kufikia kukusanya Sh50 bilioni kwa mwaka kulingana na jinsi tunavyokwenda,' amesema Rahma.
Pia amesema wakati Rais Mwinyi anaingia madarakani asilimia 20 ya ardhi ndio ilikuwa imepimwa lakini sasa wamefikia asilimia 20 lakini wanaamini hatua hiyo asilimia 80 iliyobaki itapimwa kwa muda mfupi.