Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais Mwinyi azialika benki za ndani kukopesha miradi Zanzibar

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Obedi Laiser (kushoto), akimkabidhi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi, tuzo ya kumbukumbu kama ishara ya kuthamini ushirikiano imara kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na sekta ya fedha pamoja na mageuzi makubwa ya kiuchumi visiwani humo. Na Mpiga Picha maalumu.

Muktasari:

  • Serikali iko tayari kuimarisha ushirikiano na benki za ndani zinazodhihirisha dhamira ya kuunga mkono jitihada za maendeleo, hususan katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya kiuchumi na kijamii katika sekta mbalimbali.

Zanzibar. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema kuna fursa nyingi kwa taasisi za kifedha za ndani kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayolenga kukuza uchumi na ustawi wa wananchi.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo leo Alhamisi, Juni 25, 2026 alipokutana na ujumbe wa Absa Bank Tanzania, ulioongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Obeid Laiser, katika ziara ya heshima iliyofanyika Ikulu Zanzibar.

Rais Mwinyi amesema Serikali iko tayari kuimarisha ushirikiano na benki za ndani zinazodhihirisha dhamira ya kuunga mkono jitihada za maendeleo, hususan katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya kiuchumi na kijamii katika sekta mbalimbali.

“Hata hivyo, niwapongeze sana ninyi Absa Bank Tanzania kwa utayari wenu wa kushirikiana na Serikali katika kuchangia maendeleo ya Zanzibar, Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya ufadhili wa miradi ya maendeleo kwa kupanua vyanzo vya fedha nje ya bajeti yetu ya kawaida,” amesema Rais Mwinyi.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi, akizungumza na ujumbe kutoka Benki ya Absa Tanzania, ulioongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wake, Obedi Laiser (wa tano kushoto) ulipomtembelea Ikulu, Zanzibar. Na Mpiga Picha maalumu

Amesema hatua hiyo inalenga kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Aidha, amewaahidi viongozi wa benki hiyo, kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za kifedha katika kurahisisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo kupitia mikopo na mifumo mingine ya kifedha.

Kwa upande wake, Laiser ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano wake wa muda mrefu na benki hiyo, akimpongeza Dk Mwinyi kwa uongozi ambao amesema unachochea maendeleo makubwa Zanzibar.

Amesisitiza dhamira ya Absa Bank Tanzania kuendelea kushirikiana na Serikali katika kusaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi na uchumi wa Zanzibar.

Laiser pia amesema benki hiyo inao mchango mkubwa katika uchumi wa Zanzibar kupitia utoaji wa huduma za kifedha kwa watu binafsi, wafanyabiashara na taasisi mbalimbali.

Amesema Absa inathamini mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji yaliyowekwa na Serikali ya Zanzibar.

“Tunajivunia kupata fursa ya kukutana na Mheshimiwa Rais Hussein Ali Mwinyi na kujadili safari ya maendeleo ya kipekee ya Zanzibar. Kama mshirika wa kifedha anayeaminika, Absa itaendelea kujitolea kusaidia matarajio ya wananchi wa Zanzibar kupitia upatikanaji wa fedha, urahisishaji wa uwekezaji, ukuzaji wa ujasiriamali na suluhisho bunifu za kibenki zinazochangia ukuaji endelevu wa uchumi,” amesema Laiser.

Amesema mbali na huduma za kifedha, benki hiyo inaendelea kushiriki katika miradi ya uwajibikaji kwa jamii, ikiwamo mpango wa Uzazi ni Maisha unaotekelezwa kwa ushirikiano na AMREF Health Africa pamoja na Wizara ya Afya Zanzibar.

Amesema kupitia mpango huo, Absa imechangia kuboresha upatikanaji wa vifaa muhimu vya kitabibu na kuimarisha huduma salama za uzazi kwa akina mama na watoto wachanga Zanzibar.

Hivyo, amesema benki hiyo itaendelea kutekeleza dhima yake ya kuimarisha kesho ya Afrika, kwa kusaidia ustawi wa muda mrefu wa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.