Zanzibar, Singapore zafikia makubaliano ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi
Rais wa Singapore, Tharman Shanmugaratnam (kushoto) wakati akisalimiana na mwenyeji wake ambaye ni Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, leo Juni 10, 2026 Ikulu Zanzibar
Muktasari:
- Maeneo hayo ni katika sekta za uchumi wa buluu, mafuta na gesi, umeme, teknolojia na mazao ya baharini.
Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi na mwenzake wa Singapore, Tharman Shanmugaratnam wamefikia makubaliano ya pamoja ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kiuchumi katika sekta za kimkakati.
Sekta hizo za uchumi wa buluu, nishati, teknolojia, biashara na uwekezaji, hatua inayolenga kufungua fursa mpya za maendeleo kwa pande zote mbili.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa, makubaliano hayo yanalenga kuimarisha mazingira ya biashara na kuongeza ushirikiano wa kiuwekezaji kati ya pande hizo mbili, huku yakitarajiwa kuchochea ukuaji wa sekta muhimu za uchumi na kuleta manufaa kwa wananchi wa Zanzibar na Singapore.
Makubaliano hayo yamefikiwa leo Juni 10, 2026, Ikulu Zanzibar, baada ya mazungumzo rasmi kati ya Dk Mwinyi, na Shanmugaratnam, ambaye yupo nchini kwa ziara ya siku tatu.
Rais Mwinyi amesema Zanzibar inakusudia kuendeleza ushirikiano wa muda mrefu kwa kuuimarisha katika maeneo ya kiuchumi yatakayosaidia kuongeza tija kwa wananchi wa pande zote mbili.
Amesema maeneo hayo ni pamoja na uchumi wa buluu, mafuta na gesi, umeme, teknolojia pamoja na usindikaji wa mazao ya baharini.
Rais wa Singapore, Tharman Shanmugaratnam wakati akisaini kitabu cha wageni Ikulu Zanzibar pembeni kulia ni Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi
Dk Mwinyi amesema Zanzibar inatarajia kuimarisha ushirikiano huo katika maeneo mbalimbali, ikiwemo kubadilishana uzoefu, ujuzi, elimu, teknolojia, maarifa mapya, kujenga uwezo wa nguvu kazi na kufanya kazi kwa pamoja katika sekta za kimkakati za biashara na uwekezaji.
"Tutaimarisha ushirikiano katika sekta za kimkakati na kukuza biashara na uwekezaji," amesema.
Rais Mwinyi ameihakikishia Singapore kuwa Zanzibar itaendelea kudumisha uhusiano wa kidugu uliopo baina ya pande hizo mbili, aliouelezea kuwa ni nyenzo muhimu ya kuwaleta pamoja wananchi wa Zanzibar na Singapore.
Ametumia fursa hiyo kuzikaribisha kampuni za uwekezaji na wafanyabiashara wa Singapore kuwekeza Zanzibar katika sekta kuu za uchumi wa buluu na utalii.
Katika mazungumzo hayo, Dk Mwinyi amewakaribisha Zanzibar wawekezaji wa Singapore, hususan katika sekta za uvuvi wa bahari kuu, viwanda vya kuongeza thamani mazao ya mwani na miradi ya nishati inayokwenda sambamba na ukuaji wa sekta ya utalii na hoteli.
Kuhusu sekta ya teknolojia, Rais Mwinyi amesema Zanzibar inahitaji ushirikiano wa karibu katika mageuzi ya kidigitali, ikiwa ni pamoja na kuboresha mifumo ya utoaji huduma za umma, kujenga uwezo wa watendaji na kuongeza fursa za mafunzo kwa wataalamu.
Ameongeza kuwa utafiti wa awali umeonyesha viashiria vya rasilimali za nishati katika baadhi ya maeneo ya Zanzibar, jambo linalofungua milango ya uwekezaji mpya katika sekta ya mafuta na gesi.
Ameielezea ziara ya Rais Shanmugaratnam hapa Zanzibar kuwa ni kielelezo cha kuanza kwa awamu mpya ya uhusiano na ushirikiano, pamoja na kuibua fursa mpya za maendeleo kwa manufaa ya pande zote mbili.
Kwa upande wake Rais Shanmugaratnam, amesema nchi yake iko tayari kuimarisha zaidi ushirikiano na Zanzibar na kusaidia katika kukuza uwekezaji na mageuzi ya kiuchumi.
Ameipongeza Zanzibar kwa hatua inazochukua katika maendeleo na kuahidi kuhamasisha wawekezaji kutoka Singapore kuja kushirikiana katika sekta mbalimbali za uchumi.