SMZ yatangaza vitalu vya utafutaji, uchimbaji mafuta na gesi asilia nchi kavu
Muktasari:
- Machi 20, 2024 na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alizindua duru ya kwanza ya kuvitangaza vitalu vinane vya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia baharini.
Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imetangaza vitalu viwili vya uchimbaji wa mafuta na gesi asilia nchi kavu.
SMZ imezikaribisha kampuni za ndani na nje ya nchi zenye nia ya kuwekeza katika sekta hiyo kuwasilisha maombi.
Hatua hiyo imefikiwa ikiwa imepita miezi sita tangu izinduliwe duru ya kwanza ya kuvitangaza vitalu vinane vya utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia baharini. Uzinduzi huo ulifanywa Machi 20, 2024 na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.
Taarifa iliyotolewa na Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Shaaban Ali Othman kwa vyombo vya habari Septemba 27, 2024 imesema vitalu hivyo vilitokana na kitalu cha Pemba-Zanzibar baada ya Kampuni ya RAKGAS kumaliza muda wa leseni yake na kukirejesha serikalini.
“Hivyo eneo hilo lililokuwa la kitalu cha Pemba-Zanzibar limegawanywa katika vitalu viwili ambavyo ni kitalu cha Zanzibar 1 chenye ukubwa wa kilomita za mraba 6,572 na kitalu cha Zanzibar 2 chenye ukubwa wa kilomita za mraba 6,242,” imeeleza taarifa hiyo.
Amesema uamuzi wa kuvitoa vitalu hivyo kwa njia ya majadiliano unaenda sambamba na dira ya kimkakati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuvutia uwekezaji katika shughuli za mafuta na gesi asilia na kuendeleza rasilimali zake.
"Mpango wa Maendeleo wa Zanzibar (ZADEP 2021/26), na Sera ya Uchumi wa Buluu 2022, kwa pamoja zinaelekeza kuendeleza shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia kwa maeneo ya Zanzibar na kushirikiana na kampuni za kimataifa za mafuta na gesi asilia (IOCs) katika uendelezaji wa shughuli hizo," amesema.
Kuhusu vitalu vinane vya baharini vilivyotangazwa tangu Machi, 2024 Waziri Shaaban amesema bado wanaendelea kupokea maombi na mwitikio umekuwa mzuri kwani kampuni za kimataifa za mafuta na gesi zinaendelea kujitokeza.
Hata hivyo, hakutaja ni kampuni ngapi zimeshajitokeza mpaka sasa.
Mwisho wa kupokea maombi katika vitalu hivyo awali ilipangwa kuwa Septemba mwaka huu lakini baadaye uliongezwa hadi Desemba, 2024.
“Tumefungua mlango mpya yeyote aliye tayari sisi Serikali tunakaribisha kukaa naye kuangalia namna ya uwekezaji katika sekta hii upande wa nchi kavu,” amesema.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Hamad Bakari Hamad amesema wizara imejipanga kuhakikisha sekta hiyo inatumika kikamilifu na kuleta tija kwa Taifa na wananchi wake.
Fahamu zaidi
Tofauti katika uchimbaji wa mafuta baharini na nchi kavu ni kwamba, kampuni kubwa zinapendelea nchi kavu kwani ni rahisi ikilinganishwa na baharini.
Uwekezaji wa baharini unahitaji mitaji mikubwa na uwezo mkubwa wa kifedha lakini nchi kavu kampuni zenye uwezo wa kati zinaweza kufanya vizuri.