Taasisi za masuala ya haki zapewa angalizo

Mwenyekiti wa Kamati ya kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa kitaifa ya Baraza la wawakilishi, Machano Othman Said akizungumza na watendaji wa Ofisi ya Rais Katiba Sheria Utumishi na Utawala Bora, baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Ofisi hiyo kwa kipindi cha Januari hadi Machi.

Muktasari:

  • Ni zile zinazobeba dhamana ya wananchi, ikiwemo haki za watu na maisha yao.


Unguja. Mwenyekiti wa Kamati ya Kusimamia ofisi za viongozi wakuu wa kitaifa ya Baraza la Wawakilishi, Machano Othman Said amezitaka taasisi zinazojihusisha na masuala ya haki kuhakikisha zinashirikiana ili kuleta ufanisi katika utendaji kazi.

Taasisi hizo ni Ofisi ya Mwendesha Mshtaka, Mahakama, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Kupambana na Uhujumu Uchumi (Zaeca).

Alitoa kauli hiyo baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Rais Katiba Sheria Utumishi na Utawala Bora kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2024 katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Wilaya ya Magharibi B, Zanzibar.

Machano alisema taasisi hizo zinabeba dhamana kubwa ya wananchi ikiwemo haki za watu na maisha yao, hivyo iwapo zitashirikiana na kufanya kazi kwa pamoja zitaweza kufikia malengo ya kutoa huduma bora kwa wananchi.

“Wakati mwingine kuna malalamiko kutoka kwa wananchi kuwa kesi zinachelewa na kesi zikichelewa ndio unamnyima mtu haki yake, au uchunguzi wa kesi unachelewa kwa hiyo huu ni mnyororo, ni vyema mnyororo huu kushirikiana zaidi ili kufikia malengo yaliyokisudiwa,” alisema.

Kwa mujibu wa Machano, licha ya taasisi hizo kila moja kuwa na majukumu yake tofauti na ofisi tofauti, lakini kazi zake zinaelekeana na zinahitaji muunganiko wa pamoja ili kuleta ufanisi kati ya taasisi moja na nyingine, kwani iwapo kuna moja ikipwaya inaweza kusababisha nyingine kupwaya pia.

Alizishukuru taasisi za kidini ikiwemo Ofisi ya Mufti wa Zanzibar na Kadhi Mkuu wa Zanzibar kutokana na mabadiliko yao makubwa katika utendaji na amewaomba waendelee kufanya kazi kwa pamoja na kuwataka kumaliza changamoto za wakfu, ikiwemo mashamba, majengo na mambo mengine ili kuondosha migogoro katika jamii.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Ali Suleiman alisema katika kipindi cha Januari hadi Machi 2024, ofisi hiyo imesimamia na kutekeleza shughuli mbalimbali za sekta ya sheria.

Moja ya kazi kubwa zilizofanyika alisema ni kuendelea na uratibu wa mradi wa uwezeshaji na upatikanaji wa haki awamu ya pili kwa mwaka 2024, imani yao ni kwamba utasaidia kupunguza changamoto za upatikanaji wa haki kisiwani humo kupitia misaada ya kisheria kwa wananchi.

Waziri Haroun alisema Wizara ya Katiba na Sheria inaendelea kutoa mafunzo maalumu ya kuwajengea uwezo, wapelelezi na waendesha mashtaka ili waweze kupeleleza na kuendesha kesi mahakamani.

“Ili kutatua changamoto ya uhaba wa wataaluma na ujuzi mahususi kwa waendesha mashtaka na wapelelezi wa makosa ya udhalilishaji na uhalifu wa kupangwa wa kiuchumi,” alisema Waziri Haroun

Alisema Ofisi ya Rais inawapatia mafunzo ya uchunguzi na vifaa watendaji wa mamlaka kwa ajili ya kuwajengea uwezo wa kuendesha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali za rushwa na uhujumu uchumi.

Alisema Ofisi ya Rais imejipanga kuimarisha upatikanaji wa haki na utawala wa sheria, kusikiliza kesi na kutoa maamuzi ya haraka na kwa wakati na kuhakikisha upatikanaji wa msaada wa kisheria katika maeneo yote ya kijamii unakuwapo.

Moja ya changamoto ambazo zimekuwa zikiwakumba wananchi ni kukosa uelewa wa kisheria, ili kuondokana na changamoto hiyo, Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na wadau wengine wameanzisha utaratibu wa kutoa huduma hizo kwa wananchi bure ili wanapopata matatizo yanayohusu sheria angalau wawe na msingi wa jambo linalowakwaza.

Ofisi ya Mufti Zanzibar ilitakiwa kuongeza utoaji elimu kwa walimu wa madrasa ili kuondoa wimbi la vitendo vya udhalilishaji vinavyoonekana kuongezeka kila mara, huku baadhi yake vikitokea katika vyuo vya madrasa.

Nassor Ahmed, mjumbe wa kikao hicho alisema kwa mazingira na hali ilivyo kwa sasa si nzuri kwani kumekuwapo na wimbi la vitendo vya udhalilishaji kwa hiyo jitihada kubwa zinahitajika kuanzia kwenye jamii, si tu kwenye vyombo vinavyosimamia kesi hizo.