Vituo vya afya 300 Zanzibar vyafanyiwa tathmini viwango vya ubora
Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dk Amour Suleiman (kulia), akimkabidhi Mulhat Ali Mussa cheti cha kuhitimu mafunzo ya usimamizi wa ubora wa huduma za afya Zanzibar
Muktasari:
- Ufuatiliaji wa tathmini ya ubora katika vituo vya afya unalenga kuboresha huduma za afya Zanzibar kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na zinazotakiwa kama miongozo ya afya inavyotaka.
Unguja. Wakati vituo vya afya 300 vya Serikali na binafsi vikifanyiwa tathmini ya ubora, wataalamu waliohitimu mafunzo ya usimamizi wa ubora wa huduma za afya wametakiwa kutumia elimu hiyo kuboresha huduma kwa wananchi na kupunguza malalamiko katika vituo hivyo.
Hayo yamebainika wakati wa utoaji wa vyeti kwa wataalamu hao ambao wamepewa mafunzo na Pharm Access kwa kushirikiana na Wizara ya Afya.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, leo Juni 6, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dk Amour Suleiman amesema ubora wa huduma ni jukumu la kila mfanyakazi wa afya kuanzia mlinzi hadi viongozi wa hospitali.
“Lengo ni kuhakikisha tunafikia maeneo yote yanayotoa huduma katika sekta ya afya, kwa hiyo niwapongeze walioshiriki kuona tunafanya tathmini jumuishi na kuimarisha sekta ya afya na utoaji huduma katika maeneo tofauti,” amesema.
Ameipongeza Pharm Access katika jitihada zao za kusaidia na kuwataka waendelee kushirkiana na wizara mpaka watakapoona mifumo ya sekta ya afya imekuwa imara na endelevu.
Amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Hussein Mwinyi imeendelea kuipa kipaumbele sekta ya afya kwa kuongeza bajeti na kuboresha mazingira ya kazi kwa wataalamu wa afya ili watekeleze majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Kwa upande wake, Meneja Mradi kutoka Pharm Access, Dk Faiza Abasi amesema mafunzo hayo yataimarisha uwezo wa wataalamu wa afya na kuongeza ufanisi wa huduma kwa wananchi.
Dk Faiza amesema Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika ujenzi wa miundombinu ya afya, hivyo ni wajibu wa wahudumu kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora zinazostahili.
“Huduma bora za afya ni haki ya msingi ya kila mwananchi na mifumo ya kidijitali inayozidi kuimarishwa itasaidia kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma,” amesema Dk Faiza.
Naye, Kiongozi wa Kitengo cha Ubora kutoka Wizara ya Afya Zanzibar, Hafsa Haji amesema zaidi ya vituo 300 vya afya vimefanyiwa tathmini ya ubora huku wahitimu hao wakitarajiwa kusaidia kusimamia viwango vya huduma.
“Wizara imeanzisha kitengo na ikaona ni bora tujijue tupo wapi katika huduma zetu za afya, na ndio Pharm Access wakaingia kusaidia wizara kwa sababu ni wataalamu na wana weledi, vituo 300 vya serikali na binafsi vimefanyiwa tathmni ya ubora,” amesema.
Awali, Mkurugenzi Idara ya Uuguzi na Ukunga, Mwanaisha Juma Fakih amesema kuongezeka kwa wataalamu hao wa tathmini kutasaidia kuimarisha ubora wa huduma za afya na kupunguza malalamiko ya wananchi Zanzibar.
Kwa upande wake, mhitimu wa mafunzo hayo, Fatma Suleima Daud ameahidi kuyafanyia kazi mafunzo hayo ili kuweza kuboresha huduma za afya katika hospital na vituo vya afya.
Ameipongeza Wizara ya Afya Zanzibar na Pharm Acces kwa kuendelea kuwajengea uwezo wahudumu wa afya.