Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waibana Serikali kuhusu sheria ya habari, Waziri aeleza kilichoikwamisha

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Riziki Pembe Juma akifafanua baadhi ya hoja zilizotolewa na Wawakilishi wakati wa mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo barazani Chukwani Unguja Zanzibar.

Muktasari:

  • Ilikuwa ni katika mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo katika mkutano wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Unguja Zanzibar.

Unguja. Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wameihoji Serikali kuhusu kuchelewa mchakato wa marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari, wakisema suala hilo limekuwa likizungumzwa kwa muda mrefu bila kufikia hitimisho, licha ya umuhimu wa sekta hiyo kwa masilahi ya taifa.

Wakichangia mjadala huo, wajumbe hao walitaka kufahamu sababu za mkwamo wa mchakato huo na lini sheria hiyo itawasilishwa rasmi kwa ajili ya kujadiliwa.

Kwa upande wake, Serikali imewataka kuwa na subira, ikieleza kuwa muswada wa marekebisho ya sheria hiyo unatarajiwa kuwasilishwa katika Baraza la Wawakilishi kwa ajili ya kujadiliwa katika mwaka wa fedha 2026/27.

Kauli hizo zimetolewa leo, Juni 5, 2026, wakati wa mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo katika mkutano wa Baraza la Wawakilishi unaoendelea Chukwani, Unguja.

Akichangia mjadala huo, Mwakilishi wa Wete, Shafi Mohamed Shafi (ACT-Wazalendo) amesema imekuwa ni muda mrefu tangu marekebisho ya sheria hiyo yaanze kuzungumzwa bila kuwepo kwa maelezo ya wazi kuhusu hatua iliyofikiwa, na kusisitiza kuwa umefika wakati wa kuhitimisha mchakato huo.

"Bado tunaendelea na utaratibu na mifumo ya zamani kwa sababu ya sheria hii, imekuwa ikipigiwa kelele na haifai tena kwa mazingira tuliyonayo sasa, tubadilike tulete sheria tuondokane na mifumo hii inayotuletea changamoto kubwa sana," amesema.

Naye mwakilishi wa viti maalumu, Nassra Nassor Omar ametaka kujua ilipokwama sheria hiyo kwani ni muhimu katika sekta ya habari na maendeleo ya taifa kwa ujumla.

"Sheria hii tuelezwe mchakato wake umekwama wapi maana umekuwa muda mrefu na katika bajeti hii hatujaona waziri akitaja popote kuhusu sheria hiyo," amesema.

Mwakilishi wa Wawi, Bakar Hamad Bakar (CCM), amesema sekta ya habari ndio inasukuma juhudi na mipango ya Serikali katika kufikia maendeleo, lakini bado kuna changamoto mbalimbali zinazoikabili hivyo zifanyike jitihada kuhakikisha zinaondoka.

“Ni muda mrefu kuna ahadi za kurekebisha sheria ya habari na masilahi ya wanahabari katika vyombo vya habari vya Serikali na binafsi lni mafinyo ikilinganisha na kazi kubwa wanayoifanya katika taifa hili.

Naye Profesa Omar Fakih Hamad, mwakilishi wa Pandani (ACT Wazalendo), amesema kila mara zimekuwa zikitolewa kauli za mchakato wa sheria hiyo upo mahali pazuri, lakini haufiki mwisho, hivyo akaitaka Serikali kueleza ukweli wa jambo hilo.

Naibu Waziri wa wizara hiyo, Abdugulum Hussein amesema sheria hiyo itakuja barazani ili iweze kutetea masilahi ya habari hivyo wasiwe na wasiwasi.

Akihitimisha hoja za wawakilishi hao, Waziri Dk Riziki Pemba Juma amesema Serikali inamalizia hatua za mwisho za sheria hiyo ili baadaye iende katika kamati ya ustawi wa jamii, kamati ya sheria ya Baraza la Wawakilishi kisha iingie ndani ya baraza.

"Tunamalizia hatua za mwisho za mchakato wa sheria hii kwa sasa ipo katika ngazi za kamati na hatimaye itakuja.

Amesema sheria imechelewa kwa sababu Baraza lililopita lilimaliza mapema kutokana na shughuli za uchaguzi, hivyo sheria nyingi zilisimamishwa kusubiri uchaguzi.

“Kwa hiyo niwahakikishie sheria ya habari mwaka 2026/27 itaingia ndani ya viunga vya Baraza la Wawakilishi, kwa hiyo tuwe tayari kuipitisha kwa pamoja kwa masilahi ya waandishi wa habari,” amesema.

Amesema kuwa sheria hiyo itakapopitishwa, masuala ya masilahi ya wanahabari yatajadiliwa na kuzingatiwa kwa kina kwa kuwa yatakuwa yamejumuishwa ndani ya sheria hiyo.

Akifafanua zaidi kuhusu mchakato wa sheria hiyo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amesema kwa sasa muswada wake upo katika ngazi ya Baraza la Mapinduzi.

Amesema baada ya kukamilika hatua hiyo, muswada huo utapelekwa kwenye Kamati ya Sheria ya Baraza, ambayo yeye ndiye mwenyekiti wake.

"Kwa hiyo hii sheria itakuja ipo katika hatua hizo, tuvute subra italetwa," amesema.

Baraza limepitisha Sh243.3 bilioni kwa ajili ya wizara hiyo kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2026/27.