Waliokufa kwa kula kasa wafikia tisa

Pemba. Vifo vya watu wanaodaiwa kula nyama ya kasa eneo la Kisiwapanza Wilaya ya Mkoani, Kusini Pemba vimefikia tisa, huku wengine 98 wakilazwa kutokana na tatizo hilo.

 Tukio la watu kudaiwa kula nyama hiyo lilitokea Machi 5, mwaka huu na taarifa za awali zilieleza kuwa waliokufa ni watoto wanane wa chini ya miaka 10 katika familia sita, huku familia moja ikipoteza watoto wawili.

Kwa mujibu wa Mganga wa Wilaya ya Mkoani, Bakar Haji, mmoja kati ya watu waliolazwa naye alifariki dunia juzi wakati akiendelea kupatiwa matibabu.

"Mtu mwingine msichana, Sabrina Makame Khamis (22) pia alifariki dunia, huku wagonjwa 98 wakiwa bado wamelazwa hospitali,” alisema Haji.

Alisema wataalamu wameweka kambi ya dharura kwa ajili kutoa huduma kwa mtu atakayebainika na dalili za kuathirika.

Alisema ingawa wagonjwa wameongezeka, hali zao zinaendelea vizuri tofauti na siku za mwanzo, huku wakiendelea kufanya uchunguzi na kusubiri majibu ya sampuli kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali.

Mkuu wa Wilaya ya ChakeChake anayekaimu nafasi ya Mkuu wa Wilaya ya Mkoani, Abdalla Rashid Ali, alisema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuongeza madaktari katika Kituo cha Afya Kisiwapanza.

Alisema kwa sasa hali inaendelea vizuri kwani wagonjwa walioongezeka wamesharejea nyumbani, huku wengine wakizuiliwa mpaka wataalamu watakapojiridhisha hakuna tena tatizo.

Alisema wagonjwa wanaofika kituoni hapo ni wale ambao waliwarejesha baada ya hali zao kuwa nzuri, lakini wamerejea tena baada kujisikia kama wanaumwa na koo.

“Wagonjwa zaidi wanaokuja ni wale tuliowarejesha mwanzo nyumbani, wanasema wanapata maumivu kwenye koo wanapatiwa matibabu na kurejea kwao,” alisema Abdalla.

Hata hivyo Abdalla alisema Serikali ya wilaya hiyo inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kutoogopa, huku akisema anayeona dalili akimbilie kituoni hapo.