Wasafirishaji walia makali bei ya mafuta Zanzibar

Muktasari:

  • Wamesema kupanda kwa bei ya mafuta kumesababisha pia kupanda bei ya bidhaa nyingi zikiwemo za chakula na kupelekea kuongezaka kwa ukali wa maisha,na kuiomba Serikali ingilie kati kunusuru wananchi wake na makali hayo.

Unguja. Siku moja baada ya Mamlaka ya Udhibiti Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (Zura), kutangaza bei mpya ya mafuta ambayo imeanza kutumika leo, wadau mbali mbali visiwani hapa wamesema kuna haja Serikali kuingilia kati kupunguza ukali wa maisha kwa wananchi wa kawaida.

Wameyasema hayo kwa nyakati tofauti walipokua wakizungumza na mwananchi visiwani hapa na kueleza kuwa bei hiyo ni kubwa ukilinganisha na kipato cha kawaida kwa wananchi walio wengi.

Said Abdalla, dereva wa dalala kutoka Darajani Unguna na Bububu amesema bei hiyo haiendani na gharama za uendeshaji.

Amesema kikawaida kila mwezi bei za mafuta hupanda lakini bei za nauli kwenye daladala hubaki hapo hapo kwa miaka kadhaa huku akisema kuendelea kubaki hivyo kunawasababishia mazingira magumu kazini.

Omar Silima dereva wa boda boda anaefanya kazi hiyo kwa mkataba amesema kupanda kwa bei mpya ya mafuta kutamlazimu kufanya kazi muda mwingi zaidi ya mwanzo.

‘’Bosi anataka elfu kumi yake kila siku na pikipiki nayo inahitaji kuwekwa mafuta ili niweze kuanzia kazi kesho sasa ukitazama kwa gharama hii ya mafuta ilivyopanda kuna haja hata kiwango cha kumpelekea boss kipungue vinginevyo itakua nikuumizana tu,’’ amesema.

Kwa mujibu wa mamlaka ya udhibiti huduma za maji na nishati Zanzibar (ZURA) kwa kipindi cha miezi sita kutoka mwezi Mei hadi Novemba kumekua na bei tofauti huku zikitajwa sababu mbali mbali zinazopelekea hali hiyo.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Dk Stela Ngoma Hassan ni Mkuu wa Kitivo cha Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar amesema kupanga na kushuka kwa bei ya mafuta ulimwenguni kote ni jambo lisiloweza kuepukika.

Amesema pamoja uwepo wa vita na migogoro ya kiuchumi lakini pia baadhi ya nchi zinazotoa mafuta kwa wingi ikiwemo Saudi Arabi kupunguza uzalishaji.

Pamoja na hayo amesema kuna uwezekano wa Serikali kuwapunguzia wananchi makali wa kufidia sehemu ya gharama hizo za mafuta hata kama ni kiasi kidogo kinaweza kusaidia.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hamza Hassan Juma amesema Serikali inatambua hali ambayo wananchi wanakabiliana nayo hasa kwenye upatikanaji wa nishati hiyo.

‘’Lazima watu wafahamu kuwa mafuta ya Zanzibar yanaingizwa kutokea Dar es Salaam, kuna gharama ambazo zilitakiwa kuzidi zaid lakini tunafidia gharama hizo tukijua hali ya wananchi wetu,’’ ameongeza.

Akitaja mikakati zaidi ya kukabiliana na hali hiyo amesema lengo la Serikali ni kujenga eneo maalumu ambalo litatumika kama bandari ya mafuta huko Mangapwani, na kwamba meli kutoka nje zitatia naga hapo na hivyo kuifanya Zanzibar kuwa kituo kikubwa cha kuhifadhi na hata kuziuzia mafuta, nchi nyengine.