Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wawakilishi wachachamaa kupotea misingi ya utawala bora Zanzibar

Mwakilishi wa Ole, Seif Hamad Suleiman (ACT Wazalendo) akichangia katika mkutano wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Unguja Zanzibar

Muktasari:

  • Wameitaka Serikali kuimarisha uwazi, usawa na uwajibikaji, huku wakisisitiza elimu ya utawala bora ianze ndani ya taasisi za Serikali. Pia wamelalamikia upungufu wa majaji na kuchelewa kwa kesi.

Unguja. Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamesema misingi muhimu ya utawala bora imepotea Zanzibar na kuitaka Wizara ya Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuwajibika kuirejesha ili kuleta ufanisi katika utendaji kazi.

Pia, wamesema katika ofisi nyingi viongozi wametengeneza makundi na kusababisha kuporomoka kwa utendaji kazi kwa baadhi ya wafanyakazi, huku wakidai Mahakama, licha ya kuwa ni taasisi inayojitegemea, imekuwa ikiingiliwa na kupokea maagizo kutoka serikalini, jambo linaloathiri utendaji kazi wake.

Hayo yamejiri leo Mei 13, 2026 wakati wakichangia makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya wizara hiyo Chukwani, Unguja, Zanzibar, ambapo wamesema kuna ushahidi kwamba misingi ya utawala bora haipo Zanzibar, hivyo wizara inaposema inakwenda kutoa elimu ya utawala bora lazima ianzie kwenye taasisi na kubadilisha hali hiyo.

Akichangia mjadala huo, Mwakilishi wa Pandani, Profesa Omar Fakih Hamad (ACT Wazalendo), amesema licha ya wizara hiyo kutaja kwenye bajeti kwamba inakwenda kutoa elimu ya utawala bora, lakini katika taasisi zenyewe hakuna hali hiyo, huku akitaja maeneo makuu sita ambayo yanaonekana kutozingatiwa.

Akitaja mambo hayo ni pamoja na kukosa ushirikishwaji, ufanisi na ubora wa kazi, uwajibikaji, uwazi na usawa.

“Uwajibikaji nao ni kiashiria cha utawala bora na hakuna uwazi na usawa, kwa hiyo haya ni mambo yanayotakiwa wizara kuhakikisha yanapatikana,” amesema.

Naye Mwakilishi wa Chumbuni, Makame Mohamed Sufiani (CCM), amesema viongozi wa taasisi za Serikali wanatengeneza makundi na kuwagawa wafanyakazi, jambo linaloshusha utendaji kazi wa kitaasisi.

Amesema viongozi wengi hawapendi kuambiwa ukweli, hivyo watumishi wanaoonekana kusema ukweli wanapata wakati mgumu wa kazi, hivyo ipo haja ya kubadilika katika utendaji.

Kaimu Waziri Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Suleiman Masoud Makame akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya wizara hiyo mwaka 2026/27 Barazani Chukwani Unguja Zanzibar.

“Kuna makundi ya wafanyakazi yanatengenezwa kwenye taasisi za umma, viongozi wanawagawa wafanyakazi na hawapendi kuelezwa ukweli, kwa hiyo mtu akitaka kusema ukweli anaonekana hafai na kuwa na wakati mgumu kwenye kazi. Wizara ina kazi kubwa kuhakikisha jambo hili viongozi hawagawi wafanyakazi,” amesema.

Mwakilishi wa Ole, Seif Hamad Suleiman (ACT Wazalendo), amesema misingi ya utawala bora inapaswa kuanzia katika vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), akieleza kuwa vinapaswa kupewa elimu ya kutosha kuhusu misingi hiyo.

Amesema hali hiyo inatokana na ukweli kwamba wananchi kwa sasa wanaonekana kuelewa zaidi haki zao, tofauti na baadhi ya vikosi hivyo vinavyoonekana kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya utawala bora.

Naye Mwakilishi wa Mtambile, Alley Masoud Alley (ACT-Wazalendo), pamoja na Mwakilishi wa Paje, Jaku Hashim Ayoub, wamesema kuwa hakuna usawa katika utumishi wa umma pamoja na utoaji wa haki kwa wananchi.

“Usawa kwa watumishi wa umma taasisi zetu Zanzibar unakuta zinatofautiana katika maslahi kiasi kwamba msingi wa utumishi wa umma haupo,” amesema Alley.

Mwakilishi wa nafasi za wanawake (ACT Wazalendo), Moza Mohamed Khamis, amesema kuwa Mahakama licha ya kuwa ni chombo kinachojitegemea, kiuhalisia hakina nguvu ya kutosha.

Amesema badala yake chombo hicho kinaonekana kuingiliwa kiutendaji katika utekelezaji wa majukumu yake.

“Mahakama hii haionekani kama ina uwezo, licha ya kwamba ni chombo kinachojitegemea,” amesema.

Pia, amesema Mahakama Kuu bado ina majaji wachache ukilinganisha na ongezeko la idadi ya kesi, hali inayodhoofisha ufanisi wa utendaji wa chombo hicho.

Amesema kutokana na upungufu huo, kesi zimekuwa zikichukua muda mrefu bila kusikilizwa kwa wakati kutokana na uhaba wa majaji wa kutosha. Kwa sasa Zanzibar ina jumla ya majaji 15.

“Kumekuwapo na vimemo vingi vinavyotolewa mahakamani, hili linaonesha kuingiliwa kwa utendaji wake na kuifanya ikose uhuru wake,” amesema.

Awali, akiwasilisha bajeti hiyo Kaimu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Suleiman Masoud Makame, ametaja vipaumbele 10 vinavyokwenda kutekelezwa, akiomba baraza liidhinishe Sh123.682 bilioni kwa ajili ya kazi hizo.

Miongoni mwa vipaumbele hivyo ni pamoja na kuendeleza matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika utumishi wa umma na kusimamia misingi ya utawala bora, maadili na kuongeza mapambano dhidi ya rushwa pamoja na ukaguzi na udhibiti wa rasilimali za umma.