Wawakilishi wanawake wakomaa na udhalilishaji

Muktasari:

  • Kati ya wawakilishi 10 waliochangia mjadala kwa kuzungumza, tisa walikuwa wanawake waliozungumzia kadhia wanayopata wanawake na watoto kutokana na vitendo vya udhalilishaji.

Unguja. Wawakilishi wanawake wameng’aka kwenye Baraza la Wawakilishi wakielezea kadhia wanazopitia wanawake na watoto kutokana na  ukatili, udhalilishaji.

Wawakilishi hao walikuwa wakichangia mjadala  wa ukatili na udhalilishaji wa watoto na wanawake ambapo kati ya 10 waliochangia mjadala huo kwa kuzungumzia, tisa walikuwa wanawake.

 Hayo yalijitokeza wawakilishi walipojadili hotuba ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa mwaka 2024/25.

Waziri mwenye dhamana na wizara hiyo, Riziki Pembe Juma alisoma hotuba hiyo akiomba Baraza liidhinishe bajeti ya Sh23.315 bilioni. Baraza limepitisha bajeti hiyo.

Mwakilishi wa Mahonda, Asha Abdalla Mussa amesema vitendo vya ukatili vinaendelea kutokea, hivyo wizara ihakikishe inaweka mikakati mizuri kuvidhibiti.

Mwakilishi Saada Ramadhani Mwendwa (Viti maalumu) amesema watoto wanateseka kwa kubakwa, kulawitiwa na kutelekezwa.

“Nini hasa mwarobaini wa suala hili kwa sababu kila siku yanasemwa lakini hayaishi basi kama hayaishi yapungue,” amesema.

Hata hivyo, amewataka wazazi kuwafuatilia watoto wao wanapotoka kwenda shule na wanaporudi wawachunguze.

Kwa upande wake, Fatma Ramadhan Mohamed, maarufu Mandomba mwakilishi wa viti maalumu amesema jamii ina wajibu wa kuhakikisha malezi ya watoto na wanawake, akieleza wanaume wanakimbia majukumu na wengine wakitaka wagawane na wanawake.

“Wizara iunde kitengo cha familia, wanawake wanadhalilika sokoni, anafanyiwa vitendo vya udhalilishaji, tunataka kujua nini majibu. Uchungu tulionao wa kutelekezewa familia, bado tunadhalilishwa kwenye masoko,” amesema Mandomba.

“Tatizo la udhalilishaji bado ni kubwa tushirikiane kulitokomeza ili kufika mwaka 2025 tusisikie tukio hata moja la udhalilishaji,” amesema.

Mwakilishi Bihindi Hamad Khamis (Viti maalumu) amesema wanawake wawe tayari kutoa ushahidi kukomesha vitendo hivyo badala ya kukaa kwenye familia na kuelewana jambo linalochangia kurejea kwa vitendo hivyo.

Salma Mussa Bilali (Viti Maalumu) amesema kuna taarifa nyingi hazitolewi za udhalilishaji, hivyo kuwa na uwezekano wa kuwapo matukio zaidi ya yanayosikika.

Ametaka kuboreshwa masilahi ya waratibu katika ngazi ya shehia ambao wamekuwa msaada katika kufuatilia masuala ya udhalilishaji.

Naibu Waziri wa wizara hiyo, Anna Atanas Paul amesema bado jamii haijazingatia malezi kwa watoto ndiyo maana wanakutana na vitendo hivyo, ikiwamo kuwaachia watumie vitu ambavyo umri wao bado haujafikia ikiwemo matumizi ya simu.

“Kwa hiyo tuwe makini watoto wanaangalia katuni gani, familia bora ndiyo Taifa imara na familia bora inaanzia kwa mama na baba, lakini kwa sasa cha kusikitisha watu wanatelekeza watoto,” amesema.

Akihitimisha hoja, Waziri Pembe amesema bado hali ni mbaya, hivyo wanatakiwa kushirikiana kupambana na vitendo hivyo.

“Niwaombe sana, hata ninyi wawakilishi kwenye ziara zenu hatusikii mkisema masuala haya, tunaomba iwe ajenda yetu sote lisiwe la mmoja, tukemee kabisa kutokomeza matendo haya,” amesema.

Amesema wizara itahakikisha huduma zinaendelea kuimarishwa na kutia nguvu zaidi kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia na kustawisha jamii.