Wawakilishi wataka hatua za wazi mifugo kuvamia mashamba ya wakulima

Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Shamata Shaame Khamis akijibu maswali barazani
Muktasari:
- Serikali imekiri kuwa changamoto ya mifugo kuingia kwenye mashamba imekuwa ikitokea kwa muda mrefu na kuwataka wakulima kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama ili hatua stahiki zichukuliwe.
Unguja. Licha ya Serikali kueleza mipango yake ya kuimarisha kilimo, ikiwemo kuotesha miche na kuwagawia wakulima, wawakilishi wameibua changamoto kubwa inayowakumba wakulima, ikihusisha mazao yao kuharibiwa na mifugo, jambo linalosababisha hasara kubwa na kuzuia maendeleo ya kilimo cha maeneo hayo.
Akichangia katika kipindi cha maswali na majibu leo Mei 24, 2025, Mwakilishi wa nafasi za Wanawake, Shadya Mohamed Suleiman amesema kumekuwapo na kilio cha muda mrefu cha wafugaji kuweka mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima na kuwafanya washindwe kufikia malengo yao, akitaka kujua jitihada za wazi zinazochukuliwa na Serikali.
Akijibu swali hilo, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Shamata Shaame Khamis amekiri kwamba wamekuwa wakipata malalamiko kuhusu changamoto hiyo ya jinsi wafugaji wanavyoharibu mazao ya wakulima.
Kwa mujibu wa waziri huyo, si tu kulisha mifugo kwenye mashamba, lakini pia wanapokea malalamiko ya wizi wa mazao, vitu ambavyo vinarejesha nyuma jitihada za kukuza kilimo licha ya tatizo la wizi kupungua kwa sasa.
“Natoa wito kwa wananchi lazima watambue kwamba hakuna mtu aliye na thamani au zaidi ya mwingine. Wote tuna haki sawa, mfugaji ana haki ya kufuga na mkulima ana haki ya kulima, kwa hiyo wafugaji waache kuingiza mifugo yao kwenye mashamba,” amesema.
Ametumia fursa hiyo kuwataka wakulima wanaokumbana na kadhia hiyo watoe taarifa kwenye vyombo vya ulinzi na usalama ili hatua zichukuliwe, na wizara itakuwa mstari wa mbele kuhakikisha inasimamia haki hizo.
“Tutahakikisha tunalinda wakulima wetu kwa wivu mkubwa sana,” amesema Waziri Shamata.
Awali, katika swali la msingi, Mwakilishi wa nafasi za wanawake, Chumu Kombo Khamis alitaka kujua mipango ya wizara ya kuhakikisha inapatikana miche ya miti mbalimbali na utaratibu wa wizara wa kutoa miche kwa wananchi muda wa mvua unapofika.
Katika majibu yake, Waziri Shamata amesema wizara imekuwa ikiendelea na jitihada za kuotesha miche ya aina mbalimbali kupitia vitalu vya Serikali Unguja na Pemba.
Pia, Wizara inaendelea na utaratibu wa kujenga hamasa na kuelimisha wananchi kwa kuwapatia vifaa na utaalamu katika kuanzisha na kuzalisha miche katika vitalu binafsi ili kukidhi mahitaji yaliyopo.
“Vilevile, nawahakikishia wananchi kwamba kupitia vitalu vya Serikali na binafsi, upatikanaji wa miche kwa msimu wa mvua za Masika 2025 upo vizuri,” amesema.
Kuhusu upatikanaji wake, amesema baada ya kukamilisha utaratibu wa kuotesha, wizara hutoa taarifa kupitia vyombo vya habari kuhusu utaratibu wa upatikanaji na upandaji wa miche hiyo.
Amesema kwa msimu wa Masika wa mwaka 2025, wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, imeandaa ratiba ya upandaji miti katika maeneo mbalimbali kupitia programu yake ya Urithi wa Kijani (Green Legacy).
Hata hivyo, wizara inapokea maombi mbalimbali ya kupatiwa miche kupitia taasisi za Serikali na kiraia pamoja na wananchi, huku utoaji wa miche unazingatia ukubwa wa eneo, hali ya eneo, aina na idadi ya miche.