Zanzibar mbioni kufumua mfumo wa elimu

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Unguja. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inakusudia kufumua mfumo wa elimu visiwani hapa ili uendane na mahitaji ya soko la ajira.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Leila Mohamed Mussa alisema hayo jana, alipozungumza na waandishi wa habari kueleza mafanikio ya wizara hiyo kuelekea kilele cha miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Alisema kwa kutambua umuhimu wa sekta ya elimu katika kufanikisha Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050, Serikali imedhamiria kufanya mageuzi makubwa nchini kuendana na uhalisia uliopo sasa.

“Mfumo wa elimu utafumuliwa, ili uendane na mahitaji ya sasa kutokana na mabadiliko ya kidunia,” alisema.

Alisema bajeti ya sekta ya elimu inazidi kuongezeka kutoka Sh265 bilioni mwaka 2021/22 hadi kufikia Sh457.2 bilioni mwaka 2022/23, sawa na ongezeko la asilimia 72.2.

Alieleza baada ya Serikali kutangaza elimu bure Septemba mwaka 1964 baada ya Mapinduzi, mpaka sasa gharama zote za elimu zinafidiwa na Serikali, zikiwemo, kuwapatia madaftari wanafunzi, malipo ya mitihani ya taifa, vitabu na kuhakikisha mazingira mazuri ya kujifunzia na kufundishia yanayokidhi mahitaji ya kila mtoto.

Alisema kuwapo mazingira hayo kumesababisha kila mtoto hata wale wanaotoka familia duni kupata haki yao ya elimu bila ubaguzi wowote.

Hatua hiyo imeongeza uandikishaji kutoka wanafunzi 25,432 kabla ya Mapinduzi na kufikia wanafunzi 593,591 mwaka 2023 baada ya miaka 60 ya Mapinduzi.

Waziri Lela alisema kwa kipindi cha miaka mitatu Serikali imejenga madarasa 2,273, kati ya hayo tayari 1,131 yameanza kutumika na mengine yatafunguliwa mwaka huu wa fedha.

“Shule 18 kati ya 25 za ghorofa zinazojengwa mwaka huu wa fedha zimeingia katika miradi ya uwekaji wa mawe ya msingi katika sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi Zanzibar,” alisema.

Alisema shabaha ya Serikali ni kuhakikisha wanafunzi wote wanasoma shule kwa shifti moja na idadi ya wanafunzi isiyozidi 45 kwa darasa.

Ripoti ya Mageuzi ya Elimu ilionyesha jumla ya madarasa 5,600 yalikuwa yanahitajika kufikia shabaha hiyo, na kwa sasa idadi imepungua na kufikia madarasa 3,327 kutokana na ujenzi wa madarasa 2,273.

Mdau wa elimu, Yassir Jumbe alisema ujenzi wa miundombinu uende sambamba na kuwa na walimu wenye ujuzi watakaowasaidia watoto kupata elimu yenye ushindani duniani.