Zanzibar yainadi Pemba ikiita uwekezaji katika sekta ya utalii, viwanda
Muktasari:
- Eneo la uwekezaji la Micheweni, Pemba, lina ukubwa wa zaidi ya ekari 800 na tayari limewekewa mpango mkuu wa matumizi ya ardhi.
Dar es Salaam. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imewaita wawekezaji kutoka sekta ya utalii, maendeleo ya majengo, viwanda vya usindikaji na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kuwekeza katika eneo la Micheweni, Pemba.
Eneo hilo, ambalo sasa linatarajiwa kufunguliwa rasmi, linatajwa kuwa kitovu kipya cha fursa za biashara na uwekezaji, kikilenga kuzalisha ajira na kuongeza fursa za biashara.
Akizungumza jana, Julai 12, 2026, Mkurugenzi wa Kitengo cha Uhamasishaji Uwekezaji katika Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (Zipa), Khamis Dunia, amesema eneo hilo lenye ukubwa wa zaidi ya ekari 800 tayari limewekewa mpango mkuu wa matumizi ya ardhi.
“Eneo hili pia linaendelea kuwekewa miundombinu muhimu, ikiwemo barabara, umeme na huduma za maji, ili kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi,” amesema.
Akizungumza katika jukwaa la uwekezaji, mwakilishi wa Zipa amesema eneo hilo limegawanywa katika vitalu viwili; Block A yenye takribani hekta 200 na Block B yenye karibu hekta 600, huku maendeleo ya awali yakianza katika Block A kwa kujengwa mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 13.5.
“Eneo hili limepangwa kwa matumizi mchanganyiko, hivyo linatoa fursa kwa uwekezaji katika sekta mbalimbali kulingana na mahitaji ya soko na mazingira ya eneo husika,” amesema.
Mbali na uwekezaji wa hoteli na majengo ya biashara, Serikali pia inalenga kuvutia viwanda vya usindikaji wa samaki na miradi ya Tehama, ikiwemo uwezekano wa kuanzisha kituo cha kuhifadhi na kurejesha taarifa (Data Recovery Centre), kutokana na eneo hilo kuwa karibu na bandari na miundombinu mingine muhimu ya usafirishaji.
Kwa mujibu wa Zipa, ukaribu wa Micheweni na bandari pamoja na uwanja wa ndege unaifanya kuwa sehemu yenye ushindani mkubwa kwa uwekezaji katika uzalishaji wa bidhaa, huduma na shughuli nyingine za kiuchumi.
Mkurugenzi wa Property International, Abdulhalim Salim, amesema bado watu wengi ndani na nje ya Zanzibar hawajafahamu kwa kina jitihada zilizofanywa na Serikali kuandaa eneo hilo kwa uwekezaji, ikiwemo kupeleka miundombinu muhimu.
Amesema bado kuna dhana kwamba maeneo ya Pemba hayafikiki na hayana huduma za msingi, jambo ambalo si sahihi kutokana na maboresho makubwa yaliyofanyika katika miaka ya karibuni.
“Bado Pemba ni eneo ambalo halijaendelezwa kwa kiwango kikubwa, na hilo linaifanya kuwa fursa adhimu kwa wawekezaji. Watu wengi duniani wanatafuta maeneo yaliyopangwa vizuri yenye huduma zote muhimu,” amesema.
Amewataka wadau, hususan taasisi za fedha, kushirikiana katika kutoa taarifa sahihi kuhusu fursa zilizopo ili kuwahamasisha wawekezaji wengi zaidi kuwekeza katika eneo hilo.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Chama cha Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TNCC), Fatma Khamis, amewataka wafanyabiashara kutumia fursa za uwekezaji zilizopo Zanzibar, akisema Tanzania ina soko kubwa la ndani na pia inanufaika na masoko ya kikanda kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Soko Huru la Afrika (AfCFTA).
“Wawekezaji watakaowekeza Zanzibar watanufaika na fursa za kuuza bidhaa katika masoko hayo makubwa, huku TNCC na Chama cha Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo Zanzibar (ZNCC) vikiendelea kuwasaidia wawekezaji kupata vivutio mbalimbali vya kibiashara,” amesema.