Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zanzibar yajipanga kuwa kinara wa matumizi ya teknolojia na ubunifu Afrika

Wahitimu wa shahada ya pili katika sayansi ya data na akili mnemba na shahada ya pili katika Teknolojia na Mfumo wa bahari katika Taasisi ya IITMZ Unguja Zanzibar.

Muktasari:

  • Vipaumbele vya Serikali ni kubadilisha huduma za umma kuwa kidijitali, kujenga uchumi imara wa kidijitali, kuwekeza katika akili bandia na kutumia vipaji vya vijana.

Unguja. Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu, Mudrik Ramadhan Soraga, amesema Zanzibar imeanza safari ya mabadiliko ya kidijitali, huku jukumu kubwa likiwa kuhakikisha inaongoza katika matumizi ya teknolojia katika ukanda wa Afrika.

Mudrik ametoa kauli hiyo leo, Julai 5, 2026 katika mahafali ya pili ya wahitimu wa shahada ya pili katika Sayansi ya Data na Akili Mnemba (Master of Technology in Data Science and Artificial Intelligence) na Shahada ya pili katika Teknolojia ya Muundo wa Bahari (Master of Technology Ocean Structure) katika Taasisi ya Teknolojia ya India, Kampasi ya Zanzibar (IITMZ).

“Vipaumbele vyetu ni wazi: kubadilisha huduma za umma kuwa kidijitali, kujenga uchumi imara wa kidijitali, kuwekeza katika akili bandia na kutumia vipaji vya vijana wetu,” amesema Soraga.

Amesema Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu imeanza safari ya mabadiliko ya kidijitali na Zanzibar inataka kujitangaza kama kituo cha ubunifu na startups katika ukanda huo.

Amesema Zanzibar ina vipaji vya kutosha, isipokuwa kilichokuwa kinakosekana ni jukwaa kama IIT Madras, hivyo kupitia jukwaa hilo wanaamini kuna fursa za kutosha kwa kila Mzanzibari kustawi.

Akizungumza kuhusu uwepo wa chuo hicho, Soraga amesema kitachochea ubunifu katika nyanja mbalimbali kisiwani humo.

“Kwa Zanzibar, kuwa na chuo cha IIT Madras ni neema kubwa. Hiki ndicho chuo pekee cha IIT Madras kinachofanya kazi nje ya Chennai, India. Duniani kote kuna viwili tu, na kimoja kipo hapa Zanzibar,” amesema Soraga.

Amesema kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar elimu ndio nguzo kuu ya maono yao, akibainisha kuwa Zanzibar ni kisiwa kidogo, haina mashamba makubwa ya kilimo wala madini mengi, bali rasilimali yake kubwa zaidi ni watu wake.

Amesema kwa kuwekeza katika mtaji wa binadamu, wanahakikisha maendeleo endelevu ya uchumi na mustakabali wa nchi. Ameongeza kuwa ushirikiano kama huo na IIT Madras unahusiana moja kwa moja na lengo la kujenga uchumi unaotegemea maarifa.

Amewasihi wahitimu kuangalia mazingira yao, kutambua matatizo na kujiuliza namna wanaweza kuchangia kubuni suluhisho litakaloiweka Zanzibar kwenye ramani kama kituo cha ubunifu Afrika Mashariki.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi IITMZ, Profesa Mohamed Sheikh, amesema India na Zanzibar zilipofikia makubaliano, lengo halikuwa kuuza elimu tu, bali kujenga mfumo wa kimataifa wa ubunifu Zanzibar.

“Leo nyinyi hamtunukiwi shahada tu, bali pia mnachukua hatua moja zaidi kutimiza maono ya viongozi wa nchi zetu zote mbili,” amesema.

Amesema kwa kuleta urithi mkubwa na wa hali ya juu wa kitaaluma wa IIT Madras kwenye pwani za Zanzibar, wanawekeza katika rasilimali yenye nguvu zaidi ya ukanda huu.

Naye Mkurugenzi Msimamizi wa IITMZ, Profesa Prabhu Rajagopal, amesema siri ya mafanikio ya IIT imekuwa ushirikiano wa kimataifa, ushirikiano mkubwa na sekta binafsi na utamaduni wa kubadilisha utafiti kuwa bidhaa na suluhisho.

“Tunajivunia kampasi ya IIT Madras Zanzibar, chuo chetu cha kwanza cha kimataifa. Utamaduni wetu wa ubora unaonekana kwa takwimu, vituo vya ukuzaji wa biashara na zaidi ya startups 565. Tunataka kuunda startups 100 kutoka hapa Zanzibar,” amesema.

Amesema katika miaka michache tu, wanafunzi wamefikia 129, ambapo karibu asilimia 50 wanatoka Afrika Mashariki; Tanzania, Kenya, Uganda, Zambia na Ethiopia, huku asilimia 30 wakiwa wanawake.

Akizungumza kwa niaba ya wahitimu, Aisha Hamad Hassan amesema wametoka sehemu tofauti za dunia lakini wamejifunza, kuishi na kufanya kazi kwa pamoja.

“Kama darasa la pili la wahitimu, tumeendelea kuandika historia na kutengeneza njia kwa wale watakaofuata. Tujivunie si shahada zetu tu, bali pia jamii tuliyojenga na mustakabali tuliosaidia kuubuni,” amesema.