Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ZFDA yateketeza tani 82 za bidhaa za vyakula

Muktasari:

  • Bidhaa hizo zikiwemo mahindi, mchele na pipi na bidhaa nyingine zimekutwa hazina sifa kwa matumizi ya binadamu.

Unguja. Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi Zanzibar (ZFDA) imeteketeza tani 82 za bidhaa zilizobainika hazifai kwa matumizi ya binadamu.

Kati ya shehena hiyo, tani 78 ni mahindi ya bisi (popcorn) yaliyoharibika, na tani nne ni bidhaa mbalimbali zilizokwisha muda wa matumizi, zikiwemo pipi na mchele.

Ofisa Uhusiano wa ZFDA, Fatma Makame Juma, amesema uteketezaji huo umefanyika jana, Juni 28, 2026 katika jaa (dampo) la Kibele, Mkoa wa Kusini Unguja.

Amesema mahindi hayo yaliharibika baada ya kukaa muda mrefu katika eneo la bandari kutokana na kutokukamilishwa kwa taratibu za forodha kwa wakati.

“Kuchelewa huko kulisababisha bidhaa hizo kushambuliwa na wadudu, hali iliyochangia kupungua kwa ubora wake na hivyo kutofaa tena kwa matumizi ya binadamu,” amesema na kuongeza:

“Bidhaa zinapobainika kuwa zimeharibika au zimekwisha muda wa matumizi haziwezi kuruhusiwa kuingia sokoni kwa sababu zinaweza kuhatarisha afya ya wananchi, na ZFDA inapopata taarifa basi hufanya ukaguzi na ikigundulika haifai tuna jukumu la kuiteketeza kwa kufuata taratibu zote za kitaalamu.”

Hivyo, ametumia fursa hiyo kuwataka waingizaji wa bidhaa nchini kuhakikisha wanakamilisha taratibu zote za forodha kwa wakati ili kuepusha bidhaa zao kukaa muda mrefu bandarini na kuathiri ubora wake.

Amesema ucheleweshaji wa taratibu unaweza kusababisha hasara kwa wafanyabiashara na kuhatarisha usalama wa chakula iwapo bidhaa hizo zitaingia sokoni bila ukaguzi stahiki.

Hata hivyo, amewahimiza wafanyabiashara kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa bidhaa walizonazo katika maghala na maduka yao ili kubaini mapema bidhaa zinazokaribia kuisha muda wa matumizi au zilizoharibika.

Hatua hiyo itasaidia kulinda afya ya walaji na kuimarisha uaminifu wa wafanyabiashara kwa wateja wao.

“Ni wajibu wa kila mfanyabiashara kuhakikisha bidhaa anazouza ni salama kwa matumizi ya binadamu. Tunawataka kuzingatia masharti yote ya uhifadhi na kufuatilia tarehe za mwisho wa matumizi ya bidhaa zao,” amesisitiza.

Naye Msaidizi Mkuu wa Karantini ya Mazao kutoka Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar, Othman Khatibu Vuai, amesema wizara ilifanya ukaguzi wa bidhaa za mahindi na kubaini kuwa yameharibika na si salama kwa matumizi ya binadamu na viumbe wengine.

Amewataka wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa za kilimo nchini kuhakikisha wanajisajili mara tu zinapowasili bandarini ili kurahisisha ukaguzi na ufuatiliaji wa ubora wake.

Amesema usajili wa bidhaa ni hatua muhimu katika kuimarisha usalama wa mazao ya kilimo na kuzuia kuingia kwa bidhaa zinazoweza kuwa na wadudu, maradhi au changamoto nyingine zinazoweza kuhatarisha sekta ya kilimo na afya ya walaji.

“Ushirikiano kati ya wafanyabiashara na mamlaka husika utasaidia kuongeza ufanisi katika usimamizi wa bidhaa zinazoingia nchini na kupunguza hasara zinazotokana na kuchelewa kwa taratibu za uingizaji wa bidhaa,” amesema.