Wanawake wenye uwezo nchini watakiwa kujitokeza kugombea nafasi za uongozi


Wanawake wenye uwezo nchini watakiwa kujitokeza kugombea nafasi za uongozi

"Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk John Pombe Magufuli imechukua hatua kadhaa ili kuondoa  vizingiti vinavyowazuia wanawake wasishiriki kikamilifu katika uongozi na meza ya maamuzi. Changamoto ninayoiona kwenye suala hili ni ya uchache wa wanawake wanaogombea nafasi mbalimbali iwe kwenye uongozi wa kisiasa, biashara, asasi za kiraia na hata sekta binafsi. Ni jukumu lenu kuwashawishi wanawake wenye uwezo kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi hizo,  washawishini wajitokeze," Makamu wa Rais.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, amewataka wanawake walio mstari wa mbele kutetea haki za wanawake kuwashawishi wanawake wenye uwezo kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Makamu wa Rais alisema hayo siku ya Jumatano wakati alipokuwa akifungua kongamano kusherekea Siku ya Wanawake Duniani (International Women’s Day) na miaka 25 baada ya Mkutano wa wanawake Duniani uliofanyika Beijing, China mwaka 1995.

Kongamano hilo lilifanyika Hyatt Regency (zamani Kilimanjaro Hotel) na kuhudhuriwa na wanawake zaidi ya 150.

‘’Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk John Pombe Magufuli imechukua hatua kadhaa ili kuondoa  vizingiti vinavyowazuia wanawake wasishiriki kikamilifu katika uongozi na meza ya maamuzi. Changamoto ninayoiona kwenye suala hili ni ya uchache wa wanawake wanaogombea nafasi mbalimbali iwe kwenye uongozi wa kisiasa, biashara, asasi za kiraia na hata sekta binafsi. Ni jukumu lenu kuwashawishi wanawake wenye uwezo kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi hizo,  washawishini wajitokeze,’’ alisisitiza Makamu wa Rais.

Katika mihimili mitatu ya dola, kumekuwa na mabadiliko makubwa ya uwiano wa kijinsia. Katika Bunge, wanawake ni asilimia 36.7 na Baraza la Wawakilishi Zanzibar, wanawake ni alisimia 38.  Kwenye Mahakama ya Rufaa ambayo ni Mahakama ya juu kabisa nchini wanawake ni asilimia 38.  Aidha katika Baraza la Mawaziri ( Serikali ya Awamu ya Tano) wanawake ni asilimia 18 wakati Naibu Mawaziri ni asilimia 33, jambo la kutia moyo hata hivyo ni kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mwanamke.

Wakati akitoa mwongozo wa kongamano hilo, kabla ya Makamu wa Rais kulifungua rasmi, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Women Fund Tanzania- Trust (WFT), Profesa Ruth Meena alisema ingawaje ukilinganisha na nchi nyingine barani Afrika, Tanzania inaonekana iko juu kwenye kuondoa ubaguzi wa jinsia kwenye uongozi, lakini hali halisi kwenye ushiriki wa wanawake kwenye maamuzi mbalimbali ya uongozi wa Taifa bado ni kidogo sana. Wanawake wanaoshinda uchaguzi ni wachache na uwanja wa kushindana (kati ya wanaume na wanawake) haujarekebishwa ama kusawazishwa.

‘’ Ingawaje tunashangilia ongezeko la idadi ya wanawake bungeni  kwa kuwepo viti maalum, mkondo huu una athari zake. Wanaoingia bungeni kwa kutumia mfumo huu, wanabaguliwa katika kupewa fedha za jimbo. Vilevile kuna nafasi za uongozi kama vile nafasi ya Waziri Mkuu hawawezi kuteuliwa. Aidha kwenye vyama vya siasa, hakuna mifumo iliyo wazi ya jinsi wagombea hao wa viti maalum walichaguliwa, jambo ambalo limeleta tafakuri zisizofaa kwa mfano utumiaji wa rushwa na hata upendeleo,’’ aliongeza Profesa Meena.

Makamu wa Rais alibainisha kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) na Katiba ya Zanzibar (1984) ambazo ndio ’sheria mama’ hapa nchini zinatamka bayana kuhusu usawa wa binadamu na kukataza ubaguzi wa kijinsia. Ndiyo sababu, aliongeza, mipango ya Serikali kwenye kuondoa umaskini na kukuza uchumi ina upana mkubwa na linganifu (broad-based and inclusive) ili iweze kuwanufaisha wanaume na wanawake, watoto wa kiume na wa kike, bila ubaguzi wowote.

Akatoa mfano wa jinsi Halmashauri zote nchini zinatakiwa kwa mujibu wa sheria kutenga asilimia 10 ya mapato yake ili kuwakopesha wanawake, bila riba, asilimia 4, vijana asilimia 4 na watu wenye ulemavu asilimia 2 ili waweze kutekeleza miradi yao vizuri.

Aidha alisema juhudi za kupeleka umeme vijijini, kupeleka miradi ya maji, kupunguza changamoto za mama wajawazito, kukomesha ukatili kwa wanawake na watoto, kupambana na rushwa ya ngono ni jitihada za makusudi kuboresha maisha ya wakina mama, na akawaomba wanamtandao kuunga mkono juhudi hizo za Serikali.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Zainabu Chaula alisema tangu Azimio la ulingo wa wanawake Beijing mwaka 1995, Serikali imejitahidi kutekeleza kwa dhati maeneo sita ya kipaumbele. Maeneo hayo ni uwezeshaji wanawake kiuchumi, kutoa elimu kwa usawa kati ya wavulana na wasichana, kutokomeza vitendo vya ukatili kwa wanawake, kuwawezesha wanawake kushiriki kwa usawa kwenye uongozi na masuala ya afya na maendeleo ya jamii.

Balozi wa Ireland, Paul Sherlock na Balozi wa Canada, Pamela O’ Donnell wote waliipongeza Women Fund Tanzania – Trust (WFT) kwa kushirikiana na wanamtandao wengine kuandaa kongamano hilo. Walisisitiza kuwa wasiwatenge na kuwaacha wanaume kando wakati wa kupigania usawa wa kijinsia, kwani hilo litakuwa kosa, wahakikishe wanawaelimisha wanaume juu ya mapambano haya.

Naye Mwakilishi wa UN Women nchini, Hodan Addou aliisifu Tanzania kwa kuwa na sheria nyingi zinazozuia ukandamizaji wa wanawake, lakini akasisitiza kuwa usawa wa kijamii ni jambo la kupiganiwa kwa nguvu zote na sio jambo la kulala na kusubiri matokeo. Akasema hata nchi nyingine nyingi zilizoendelea, bado hazijapata usawa wa asilimia 50 kwa 50 wa kijinsia, kwa hiyo mapambano yanaendelea.

Jopo la wanaharakati wanne nao walitoa mapendekezo yao mbalimbali kwenye kongamano hilo ambalo kauli mbiu yake ilikuwa ‘’ Uwajibikaji wa Uongozi katika kujenga kizazi cha Usawa wa Kijinsia (Accountable leadership for a generation of gender equality)’’.

Mkurugenzi Mtendaji wa mtandao wa msichana Initiative, Rebecca Gumi aliiomba Serikali itoe pedi za bure kwa wasichana wanaosoma shule, kwani wengi wao hawaendi shule kwa wastani wa siku 5 ama 6 kila mwezi, wakiwa kwenye hedhi. Pia akasema tuelimishe jamii kuwa na mabadiliko ya kifikra kwani watu wengi hujificha kwenye kichaka cha mila na desturi wanapotaka kumnyima mwanamke haki yake.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi alidai wizara zote ziwe na bajeti yenye mrengo wa kijinsia na pia kuwe na mfumo wa utoaji taarifa kuhusu maendeleo ya kijinsia kwenye wizara zao, kwani kwa hivi sasa hakuna mrejesho huo.

Profesa Bertha Koda wa Idara ya Jinsia, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema kuna haja ya kutazama sheria zetu kwani zinagongana, moja ikisema hivi na nyingine ikisema vingine na kufanya maamuzi ya usawa wa kijinsia yasifikiwe haraka, akatoa mfano wa Sheria za Ndoa na Ardhi.

Naye Profesa Ruth Meena alisisitiza kuwa mfumo mzima wa uzalishaji kwenye kilimo una mapungufu mengi, na ambao unabebesha mwanamke sura ya umaskini, licha ya kufanya kazi nyingi kwenye sekta hiyo.

Alisema pamoja na takwimu zinazotolewa kila mara kuwa uchumi wa Taifa letu umekuwa kwa wastani wa asilimia 7 ambao ni wastani mzuri, hali hii haiendani na kupungua kwa umaskini  na kwamba kwa kiasi kikubwa wanawake ndiyo wako hatarini kutumbukia kwenye umaskini zaidi ukilinganisha na wanaume. Akataka hali hiyo irekebishwe, na hasa kwa wanawake waishio vijijini ambao ukilinganisha na wale wa mijini wana hali mbaya sana ya kipato. Kulikuwa na majadiliano marefu baada ya jopo hilo kutoa tathimini yao.

Mkurugenzi Mtendaji wa WFT, Mary Rusimbi alimpa tuzo maalum Makamu wa Rais kwa kutambua mchango wake mkubwa kwa maendeleo ya wanawake hapa nchini. Tuzo hii maalum iliandaliwa na mtandao wa wanawake unaojumuisha zaidi ya vikundi 60.

Kongamano hilo pia lilihudhuriwa na Balozi Getrude Mongella ambaye mwaka 1995 ndiye alikuwa Mwenyekiti wa Mkutano wa Beijing na kuiletea sifa nchi yetu kwenye harakati za kumkomboa mwanamke na wasichana kimapinduzi barani Afrika.

Kwa wale ambao hawakumbuki kwa nini kuna maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani (ambayo huadhimishwa tarehe 8 Machi kila mwaka) ikumbukwe kuwa ilitokana na  harakati za wanawake wafanyakazi waliokuwa wakidai haki ya kufanya kazi katika mazingira mazuri na kulipwa maslahi stahiki.

Mwaka 1912, takriban wafanyakazi 15, 000 wengi wao wanawake kutoka viwanda vya nguo huko New York waliandamana kudai haki zao ambapo mmiliki wa kiwanda hicho aliwaua takriban wafanyakazi 146. Jambo hili liliwasha moto na kuhamasisha utetezi wa haki za wanawake duniani.  Mwaka 1975 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitangaza rasmi kuwa siku ya Machi 8 iadhimishwe na mataifa yote kama Siku ya Wanawake Duniani.

Kwa mujibu wa Profesa Ruth Meena, maadhimisho ya siku hii mwaka 2020 yamebeba kauli mbiu ‘Mimi ni kizazi cha usawa’ na pia ‘Kizazi cha usawa kwa maendeleo ya Tanzania, sasa na baadae’.

Kongamano lililozinduliwa na Makamu wa Rais lilijumuisha wadau mbalimbali watokao katika TAPO ya wanawake, wasichana na wapenda haki, na pia watetezi wa haki za binadamu.

Pia, vyama vya siasa vimeombwa kuanzia Siku ya Wanawake Duniani wafuatilie kwa makini matamko na ilani zitakazotolewa na wanaharakati wa mtandao ili wajifunze mengi yatakayowasaidia watakapofanya kampeni wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Madiwani , wabunge na Rais mwezi Oktoba,2020.