Lowassa apinga urais wa Dk Magufuli

Aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana. Katikati ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia

Muktasari:

Lowassa, aliyeonekana kukasirishwa na matokeo yaliyokuwa yanatangazwa kwa kutokuwa na tabasamu kama ilivyo kawaida yake, alitaja malalamiko hayo kuwa ni kupunguzwa kwa kura zake, kuongezewa kura kwa mgombea wa CCM, kutangazwa matokeo batili na kutotoa nafasi ya kuulizwa maswali na wanahabari.

Dar es Salaam. Saa chache kabla ya Dk John Magufuli wa CCM kutangazwa mshindi wa kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jana, mgombea wa Chadema, Edward Lowassa aliwasilisha pingamizi lenye hoja tatu kuhusu mwenendo wa uchaguzi kwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva na kugonga mwamba.

Katika tamko hilo, Lowassa alikuwa akipinga matokeo ya kura za urais yaliyotangazwa na NEC akidai kuwa si halisi na kutaka yasitishwe, lakini tume hiyo haikueleza lolote badala yake iliendelea kutangaza matokeo ya majimbo na baadaye mshindi wa urais.

Ilivyokuwa

Mgombea mwenza wa Chadema, Duni Haji Duni akiambatana na mwanasheria wa chama hicho, John Mallya waliwasili na kuruhusiwa kuingia Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) saa 5:45 asubuhi.

Lengo la safari yao ilikuwa kuonana na viongozi waandamizi wa NEC, ambao walikuwa ukumbini hapo wakiendelea na upokeaji wa matokeo ya kura za wagombea urais kutoka majimbo 61 yaliyokuwa yamebaki na kuyatangaza.

Hata hivyo, baada ya kuingia ndani ya ukumbi huo, ugeni huo ulizuiwa kuonana na viongozi waliokuwa wanawahitaji, hivyo walielekezwa wabaki nje na kusubiri iwapo ridhaa ingetolewa, lakini haikuwa hivyo.

Waandishi wa habari waliokuwa eneo hilo walitaka kumuhoji, lakini wakazuiwa.

Kutokana na mwingiliano huo wa maslahi, watu wa usalama walilazimika kumwondoa Duni kutoka kwenye ukumbi huo uliopo Mtaa wa Shaaban Robert na kumtaka kwenda zilipo ofisi za NEC, Mtaa wa Ghana kuwasilisha barua aliyokuwa nayo.

“Nimekuja hapa na nikakaa kwa zaidi ya dakika 20 bila kuonana na niliokuwa nawahitaji. Nimeambiwa niende ofisi za Tume nikakabidhi barua yangu huko. Naelekea huko,” alisema Duni akiondoka pamoja na Mallya.

Baada ya kufika ofisi za NEC zilizoko jengo la Posta, ujumbe huo wa Chadema ulipokelewa na ofisa tume hiyo, Peter Mwezi ambaye alisaini kitabu cha kumbukumbu na uthibitisho wa kupokea barua hiyo. Alipomaliza kuikabidhi, Duni alisema: “Hata kama tume haitachukua hatua yoyote, ulimwengu umeona msimamo wa chama changu na Watanzania wanafahamu jinsi haki ilivyopindishwa. Tumeleta malalamiko yetu leo (jana) baada ya kukusanya ushahidi wa kutosha tangu matokeo ya kura za urais yalipoanza kukusanywa na kutangazwa.”

Tamko la Lowassa

Baada ya kuwasilisha malalamiko hayo, Lowassa alikutana na wanahabari, akiwa na Duni na viongozi wakuu wa Ukawa, kueleza kile alichokiita “kuporwa kura zake”.

Lowassa, aliyeonekana kukasirishwa na matokeo yaliyokuwa yanatangazwa kwa kutokuwa na tabasamu kama ilivyo kawaida yake, alitaja malalamiko hayo kuwa ni kupunguzwa kwa kura zake, kuongezewa kura kwa mgombea wa CCM, kutangazwa matokeo batili na kutotoa nafasi ya kuulizwa maswali na wanahabari.

Wakati Lowassa akitoa kauli hiyo, jana saa 8:00 mchana, NEC ilimtangaza Dk Magufuli kuwa mshindi wa kiti cha urais baada ya kupata kura 8,882,935 huku Lowassa akitajwa kupata kura 6,072,848.

Juzi, waziri huyo mkuu wa zamani aliitaka NEC kusitisha kutangaza matokeo ya kura za urais wa Muungano na kuanza upya uhakiki wa matokeo inayopokea kutoka majimbo mbalimbali nchini, ombi ambalo tume hiyo haikulizingatia.

“Tumeainisha kwenye malalamiko yetu, kutoridhishwa kwetu na mwenendo na matukio mbalimbali, hususani utangazaji wa matokeo batili, yasiyoakisi matokeo halisi yaliyopatikana kwenye vituo vya kupiga kura,” alisema.

“Tunaendelea kukataa dhuluma hii dhidi ya matakwa ya wananchi na jaribio la kutaka kubakwa kwa demokrasia kunakoonekana wazi kutokana na mwenendo wa Tume kuendelea kutangaza matokeo ya kura yasiyo ya kweli kwa kupoka ushindi wetu,” alisema Lowassa.

“Pia kumekuwapo na uporaji wa ushindi kwa wagombea wa vyama vya Ukawa kwenye ngazi ya ubunge na udiwani.”

Lowassa aliwashukuru wananchi kwa imani yao ya kumchagua pamoja na viongozi wengine wa Ukawa waliogombea majimbo mbalimbali nchini.

“Tunaamini kuwa kuchezea demokrasia ni kuvunja amani, lakini sote tunatambua ni nyie Watanzania ndio mnaoporwa haki yenu ya kupata mabadiliko, na viongozi mnaowahitaji. Hivyo nitaendelea kuwa pamoja na Watanzania wote kudai haki yenu kwa nguvu zote,” alisema.

Alisema kwa miaka mingi Tanzania imefahamika kama kisiwa cha amani katika Afrika, lakini Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu hali imekuwa tofauti kutokana na vyombo vya dola kutanda kila kona vikiwa na silaha, hali ambayo alidai ilijenga hofu.

“Kufanya hivi ni kuwatisha wananchi ili wakubali kunyang’anywa haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi wanaowataka,” alisema.

Serikali yavionya vyama

Wakati huohuo, Serikali imevipiga marufuku vyama vya siasa vinavyoingilia jukumu la NEC na kujitangazia matokeo ya kura za urais.

Kauli hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari, Assah Mwambene imekuja siku chache baada ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad kujitangazia ushindi wa kiti cha urais Zanzibar, jukumu ambalo Mwambene alisema linapaswa kufanywa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

“Tumepata tetesi kwamba kuna chama cha siasa na mgombea wake wanataka wajitangazie kuwa wameshinda urais kwa takwimu zao za kupikwa, hivyo kama Serikali tunatahadharisha mapema wasifanye hivyo,” alisema.

Alisema NEC ndiyo ina jukumu la kisheria la kutangaza matokeo ya urais wa Jamhuri ya Muungano na si chama chochote cha siasa.

Mwambene alisema matokeo ya udiwani na ubunge yatatangazwa katika maeneo husika kama ilivyosema NEC, lakini kwa matokeo ya urais ni lazima yatangazwe na tume hiyo.

Imeandikwa na Fidelis Butahe, Julius Mathias, Florid Mapunda.