Magufuli ni nani

Friday October 30 2015

Rais Jakaya Kikwete akikumbatiana na Rais

Rais Jakaya Kikwete akikumbatiana na Rais Mteule, Dk John Magufuli alipokuwa akimpongeza baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu Damian Lubuva kutangaza rasmi matokeo ya Uchaguzi Mkuu,  ambako walifuatilia kwa pamoja matangazo hayo ya moja kwa moja kupitia vituo vya televisheni wakiwa Ikulu, Dar es Salaam jana. Picha na Ikulu 

Mbio za urais za Dk John Magufuli zilianza Juni 5, 2015 alipochukua fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kupitia CCM katika Makao Makuu chama hicho mkoani Dodoma, baada ya kuteuliwa na chama chake na baadaye Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Alizindua kampeni Agosti 23, kwenye Viwanja vya Jangwani.

Dk Magufuli alionyesha ujasiri mkubwa wa kampeni kwakuwa mgombea pekee wa urais aliyesafiri kwa kilomita nyingi kwa njia ya barabara, akiomba ridhaa ya wananchi kuwa Rais wa Awamu ya Tano. Moja ya ajenda kubwa iliyombeba Dk Magufuli kwenye mikutano yake ya kampeni ni uadilifu wake, ikiwamo mwenendo alioonyesha katika nafasi yake ya waziri katika Wizara ya Ujenzi, iliyokuwa ya kipaumbele kibajeti.

Mbali na uadilifu, ajenda nyingine iliyombeba Dk Magufuli na kusababisha awe kivutio kikubwa kwa maelfu ya wananchi waliojitokeza katika mikutano yake, ni sifa ya uchapakazi wake. Mbali na watumishi, ukali wake pia umejidhihirisha mara kwa mara alipozungumzia Baraza la Mawaziri atakalounda na hasa Waziri wa Ujenzi, akisema huyo waziri atakayemteua, kama hawezi kazi aseme mwenyewe kabla ya kutimuliwa.

Dk Magufuli pia katika kampeni zake alionyesha umahiri mkubwa wa kutawala majukwaa kwa mbinu mbalimbali, ikiwamo uwezo wa kutoa salamu na vionjo vya makabila zaidi ya kumi jambo lililokuwa likiwavutia wananchi wengi katika mikutano ambayo ilikuwa ikifikia mpaka 15 kwa siku.

Baada ya kutoa salamu hizo, Dk Magufuli pia amekuwa akiomba kura kutoka kwa vyama vyote, kuanzia CCM, Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi, ACT na kwa watu wasio na vyama, huku akiwaambia kuwa kazi yake itakuwa kuwaletea maendeleo na kwa kuwa maendeleo hayabagui, ndiyo maana anaomba kura za vyama vyote.

Ahadi zake

Advertisement

Dk Magufuli katika mikutano hiyo, amekuwa akiahidi kushusha bei ya vifaa vya ujenzi hasa saruji, mabati na misumari ili wananchi wanaofanya kazi wajenge nyumba bora. Katika kuongeza idadi ya Watanzania wanaofanya kazi ili kufikia lengo hilo, Dk Magufuli alisema katika kila mtaa na kijiji, Serikali yake itatoa Sh 50 milioni kwa ajili ya kuanzisha na kukuza biashara ndogo za wanawake na vijana.

Alisema atataka kila anayefanya kazi apate kipato kizuri kitakachomsaidia kukabiliana na mahitaji ya maisha yake, ikiwamo kujenga nyumba bora kutokana na kushushwa kwa bei za bidhaa za ujenzi. Pia amekuwa akitamba ‘Mimi hapa kazi tu’ Tanzania ya Magufuli ni ya viwanda, viwanda kwa ajili ya wakulima namaji safi na salama vijijini. Pia kwenye kampeni zake amekutana na changamoto kadhaa ikiwamo kukabiliana na mashabiki wa Ukawa eneo la Soweto na Uyole mkoani Mbeya. Pia Dk Magufuli ambaye alijambulisha kwa kibwagizo cha ‘hapa kazi tu’ pia alipata umaarufu kwa staili yake ya kuonyesha uimara wa afya yake jukwaani kwa kupiga ‘push up’. Aliweza kuiga staili ya Chadema ya M4C, yaani Movement for Change na kuiita Magufuli for Change, kuwavutia wana-Chadema na wanaotaka mabadiliko.

Magufuli ni nani?

Jana ilikuwa siku ya kuzaliwa kwake. Alizaliwa Oktoba 29, 1959 wilayani Chato Mkoa wa Kagera (sasa ni wilaya ndani ya Mkoa wa Geita). Alianza elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Chato mwaka 1967 na akahitimu mwaka 1974. Alifaulu na kujiunga na Shule ya Seminari Katoke, iliyoko Biharamulo ambako alisoma Kidato cha Kwanza na cha Pili kati ya mwaka 1975 na 1977, akahamishiwa Shule ya Sekondari Lake, Mwanza ambako alisoma kidato cha Tatu na Nne kati ya mwaka 1977 na 1978.

Masomo ya kidato cha Tano na Sita aliyapata mkoani Iringa katika Shule ya Sekondari Mkwawa kuanzia mwaka 1979 hadi 1981. Baadaye akarudi Chuo cha Ualimu Mkwawa kusomea Stashahada ya Elimu ya Sayansi akibobea kwenye masomo ya Kemia, Hisabati na Elimu. Hii ilikuwa kati ya mwaka 1981 na 1982.

Baada ya kuhitimu akaenda kuanza kazi ya ualimu katika Shule ya Sekondari Sengerema, akifundisha masomo ya Kemia na Hisabati.

Ajira hii aliifanya kati ya mwaka 1982 na 1983, kisha akajiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria akianzia Makutupora, Dodoma (Julai - Desemba 1983), na kambi ya Makuyuni, Arusha (Januari hadi Machi 1984) na akamalizia katika kambi ya Mpwapwa mkoani Dodoma (Machi – Juni,1984).

Mwaka 1985 alijiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akisomea Shahada ya Sayansi ya Elimu akibobea kwenye masomo ya Kemia na Hisabati na alihitimu mwaka 1988.

Mwaka 1989 - 1995 alifanya kazi katika kiwanda cha Nyanza Cooperative Union (Ltd.) akiwa mkemia na wakati huohuo alianza masomo ya shahada ya uzamili ya Sayansi katika Chuo Kikuu cha Salford nchini Uingereza, kikishirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako alisoma kati ya mwaka 1991 na 1994.

Magufuli aliendelea na elimu ya juu zaidi kwa maana ya Shahada ya Uzamivu ya Kemia kuanzia mwaka 2000 hadi 2009 ambayo aliihitimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuwa mhitimu wa shahada ya udaktari. Dk Magufuli ana mke na watoto.

Safari yake kisiasa

Dk Magufuli alianza mbio za ubunge mwaka 1995, alipojitosa katika jimbo la Chato kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na kushinda wakati akiwa na miaka 36.

Rais Benjamin Mkapa akamteua kuwa Naibu Waziri katikaWizara ya Miundombinu. Kazi ya ubunge na unaibu waziri ilimpeleka salama hadi mwaka 2000.

Uchaguzi wa mwaka 2000 ulipoitishwa, Dk Magufuli aligombea na kushinda kwa mara ya pili. Rais Mkapa akamteua kuwa Waziri wa Wizara ya Miundombinu na akakaa hapo hadi kipindi cha uongozi wa Mkapa kilipokamilika.

Mwaka 2005 aliendelea kutupa karata jimboni kwake kuwania ubunge kwa kipindi cha tatu. Akaingia kwenye orodha ya wabunge waliopita bila kupingwa. Lakini safari hii, Rais Jakaya Kikwete alimteua kuongoza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi hadi mwaka 2008 alipohamishiwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ambayo aliiongoza hadi mwaka 2010.

Mwaka 2010 wana CCM wa Chato hawakuchoka kumpa ridhaa Dk Magufuli, hii ikiwa mara ya nne. Mara hii hakupita bila kupingwa, alipambana na mgombea kutoka Chadema, Rukumbuza Vedastus Albogast ambaye alifanikiwa kumtoa jasho Magufuli.

Katika uchaguzi ule alipata ushindi wa asilimia 66.39 dhidi ya asilimia 26.55 za mgombea wa Chadema. Na baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge kwa mara ya nne, Rais Kikwete alimrudisha katika Wizara ya Ujenzi.

Mwanasiasa huyu ni mwanataaluma mbobezi, akiwa tayari ni mwanachama wa vyama vya kitaaluma kama Chama cha Wakemia wa Tanzania na kile cha Wataalamu wa Hisabati Tanzania.

Magufuli ana mahaba na namba. Si kwamba amesoma hisabati kama somo lakini amekuwa akipenda masuala ya namba na moja ya alama yake kubwa ya kiutendaji ni uwezo wake mkubwa wa kukariri takwimu mbalimbali kuhusu masuala anayoyafanyia kazi.

Kama msomi, Dk. Magufuli ameandika machapisho mbalimbali yakiwamo; “A New Rate Equation for Solid State Decomposition and its Application to the Decomposition of Calcium Carbon Trioxide, The Control and Management of Heat as Challenge and Opportunity to Engineers, Funding for the EAC Road Network Project na The Potential of Anacardic Acid Self-Assembled Monolayer From Cashew Nut Shell Liquid As Corrosion Protection Coating (2009).

Mke wa Magufuli, Janet ni Mwalimu wa Shule ya Msingii Mbuyuni, shule aliyokuwa akifundisha Salma, mke wa Rais Jakaya Kikwete.

Sifa nyingine ya ziada ya John Pombe Magufuli ni kwamba hanywi pombe wala havuti sigara.