Mchango wa wazazi katika mafanikio ya elimu kwa watoto

Mzazi anayefuatilia maendeleo ya mtoto wake,ana nafasi kubwa ya kumsaidia kufanya vizuri shuleni. Picha ya maktaba

Muktasari:

Katika waraka huo Serikali ilisisitiza kuwa kuanzia mwaka 2016 ingetoa elimu bure kuanzia ngazi ya awali hadi kidato cha nne, ikiwa pia ni azma ya kutekeleza sera mpya ya elimu ya mwaka 2014.

Januari 27 mwaka 2015 iliyokuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, ilitoa Waraka wa Elimu Na 5 wa mwaka 2015 kuhusu kufuta ada na michango yote katika elimumsingi.

Katika waraka huo Serikali ilisisitiza kuwa kuanzia mwaka 2016 ingetoa elimu bure kuanzia ngazi ya awali hadi kidato cha nne, ikiwa pia ni azma ya kutekeleza sera mpya ya elimu ya mwaka 2014.

Kimsingi, suala la elimu bure si geni kwa Watanzania wengi waliosoma miaka ya nyuma hadi mwanzoni mwa miaka ya 1990 kabla ya sera ya kuchangia gharama ilipoanzishwa nchini.

Tofauti iliyopo ni kwamba sasa hivi Tanzania imepanuka ikiwa na ongezeko kubwa la watu na uwezo wa Serikali kuhudumia watu wake ipasavyo umepungua.

Hata hivyo, utararibu huu wa elimu bure kuanzia awali hadi kidato cha nne unaonekana haujaeleweka vizuri kwa wazazi wengi. Sasa hivi maelekezo yaliyopo ni kuhakikisha kila mtoto mwenye umri wa kusoma shule ya msingi anatakiwa kuwa shuleni.

Hivyo, walimu wakuu wamekuwa wakipata shida kuwarejesha watoto ambao walikuwa tayari wameacha shule, kutokana na utoro na kukosa uwezo wa kuchangia gharama za masomo.

Bado wazazi hawaelewi wajibu wao

Nikiwa najiandaa kuandika makala haya, niliamua kufanya uchunguzi mdogo kwa kutembelea baadhi ya shule zilizoko mkoani Dar es Salaam na kuzungumza na wakuu wa shule.

Nilikutana na masimulizi mengi kuhusiana na changamoto za elimu nchini, kubwa zaidi nililoliona ni la wazazi wengi wa Dar es Salaam kutojali kabisa elimu ya watoto wao.

Katika shule mojawapo ya sekondari ya kata katika Manispaa ya Ilala, nilikutana na Mkuu wa Shule aliyenieleza kuwa siku moja walikuja wazazi shuleni hapo wakidai mahitaji ya watoto wao kama vile vitabu, sare, kalamu, madaftari na chakula.

Walikuwa wakiamini kuwa Serikali ilishatangaza kuwa elimu ni bure, hivyo walitegemea watoto wao watapata mahitaji hayo shuleni kwani Serikali ilikuwa imeshatuma shuleni fedha kwa ajili ya mahitaji ya watoto wao. Ndivyo walivyodai wazazi wale.

Tangu kutangazwa kwa mpango wa elimu bure kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha nne, tumeona kuwa kulihitajika elimu ya kutosha kwa wazazi, wanafunzi na jamii kwa jumla kuhusu ukweli halisi wa elimu bure.

Walimu wengi niliozungumza nao wanasema kuwa matatizo makubwa yako kwa wanafunzi ambao wazazi wao wametengana na kila mmoja anategea jukumu la malezi kwa mwenzake. Wanashindwa kufuatilia maendeleo ya watoto wao kwa sababu mbalimbali kama madai ya kuchoshwa na shughuli za kimaisha na uzembe unaosababishwa na ulevi wa kupindukia.

Kero za wanafunzi

Nikiwa Kimara – Mbezi nakutana mwanafunzi wa kike mdogo kabisa ananiambia yuko kidato cha pili anasoma shule moja ya kata iliyoko maeneo ya Kiluvya. Alikuwa amesimama anasubiri usafiri wa kwenda shuleni; anasema wakati mwingine hupanda malori ya mchanga kwenda shuleni kwake.

Binti yule anasema huamka saa kumi na nusu kila siku na kabla ya kwenda shule hufanya usafi wa ndani ya nyumba yao. Anaishi na shangazi yake anayefanya biashara ndogondogo, kwani wazazi wake walitengana miaka mingi iliyopita

Hutoka kwao Kimara Bonyokwa asubuhi saa kumi na mbili na akifika Kimara mwisho huhangaika kupata usafiri. Hufika shuleni saa mbili au wakati mwingine saa tatu kasoro akiwa amechoka. Na nyumbani hurejea jioni na hukutana na kazi mbalimbali za nyumbani.

Mwanafunzi huyu anawakilisha kundi kubwa la wanafunzi wa Dar es Salaam wanaosoma mbali na nyumbani kwao kutokana na sababu mbalimbali. Huwa wanapata changamoto nyingi za kimasomo. Hawana muda wa kujisomea; hushindwa kufuatilia masomo darasani kutokana na uchovu; huwa dhaifu kutokana na wazazi wengi kutomudu kuwapa pesa ya chakula cha mchana wawapo shuleni.

Uhusiano wao na walimu unakuwa mbaya kwa sababu mara nyingi hawafanyi mazoezi wanayopewa darasani kutokana na mazingira ya nyumbani kutokuwa rafiki kwao kufanya mazoezi ya nyumbani; na baadhi yao kushawishika kujiunga na makundi mabaya au kudhalilishwa kingono na madereva bodoboda, makondokta wa daladala, walimu wasio na maadili pamoja na watu wengine.

Tufanyeje?

Baada ya kuangalia hali ilivyo baada ya kuanza kwa mpango wa elimu bure nchini, nadhani ipo haja sasa kwa Serikali kutoa ruzuku ya chakula kwa shule za kata ili watoto waweze kupata huduma ya chakula shuleni.

Kama inawezekana, Serikali iridhie bodi za shule kuzungumza na wazazi wanaoweza kuchangia huduma ya chakula kwa ajili ya watoto wao wafanye hivyo, ili wanafunzi wapate huduma ya chakula wawapo shuleni.

Hili la chakula shuleni litaepusha mambo mengi hasa kuwapa nguvu wanafunzi wanaoondoka nyumbani, bila ya kupata chakula na wale wanaotoka katika familia zenye wazazi wasiopatikana nyumbani. Mtoto anayepata chakula shuleni atakuwa na afya njema na utulivu wa akili kuweza kufuatilia masomo yake.

Jambo jingine ambalo viongozi wa halmashauri wanaweza kulifanya kwa kushirikiana na wakuu wa shule ni pamoja na kuhakikisha wanafunzi wanapangiwa shule zilizo jirani.

Aidha, iko haja ya kuwa na mpango endelevu wa kutoa elimu kwa wazazi na jamii kwa jumla kuhusu umuhimu wa kuwa karibu na watoto, walimu na viongozi wa shule.

0787525396