Ukijisikiliza, utajenga msingi wa maendeleo yako kiuchumi

Muktasari:

  • Hifadhi hii ya kumbukumbu inafanana na kiboksi cheusi kwenye ndege au black box, yenye mtandao wa mishipa ya fahamu kwa kila binadamu. Kila utazamacho, usikiacho hata unusacho inatengeneza sehemu ya nafsi ya ndani, kuwa makini na madirisha ya ufahamu wako, yaani nafsi iliyo wazi

Kila mtu au mazingira unayokutana nayo yanatengeneza nafsi. Kitaalamu inajulikana kama liwazo au solar plexus. Hifadhi ya solar plexus ipo nyuma ya mgongo wa binadamu unaofanya kazi kwa saa 24.

Hifadhi hii ya kumbukumbu inafanana na kiboksi cheusi kwenye ndege au black box, yenye mtandao wa mishipa ya fahamu kwa kila binadamu. Kila utazamacho, usikiacho hata unusacho inatengeneza sehemu ya nafsi ya ndani, kuwa makini na madirisha ya ufahamu wako, yaani nafsi iliyo wazi.

Nafsi au akili iliyofichika ni kumbukumbu ya mambo mbalimbali kama vile matukio, mafunzo, uzoefu au ujuzi itokanayo na watu au mazingira yanayomzunguka mtu.

Hapana shaka katika maisha yako kuna mambo ambayo huwa unayafanya kila siku. Vilevile kuna ambayo hufanywa na rafiki na jamaa zako. Lakini pamoja na yote haya, unatakiwa kufahamu kwa nini watu hufanya wanayoyafanya; kwa kupenda au kutopenda, kufahamu au kutofahamu.

Kwa mfano, ni nini humfanya mtu apige mswaki, kutabasamu, kupanga maneno wakati wa kuongea, kusalimia kwa kushikana mikono, kutembea, kujituma au kukumbuka?

Kama umewahi kujiuliza na ukashindwa kupata jibu usisikitike kwa sababu ni swali ambalo wanasaikolojia wamelifanyia utafiti kwa miaka mingi na kuandika maelfu ya vitabu.

Kwa hakika, kwa nini watu wanafanya wanayoyafanya ni moja kati ya maswali tata ambayo saikolojia imeyafanyia kazi kubwa kutafuta majibu yake. Hii ni kwa sababu kadri unavyozifahamu sababu zinazokufanya ufanye mambo fulani ndivyo unavyokuwa na uwezo mkubwa wa kudhibiti vitendo vyako hivyo, hata mienendo ya maisha yako.

Kuna mambo mengi ambayo humfanya mtu afanye vitendo fulani katika maisha yake, lakini sababu kubwa ni nafsi ya binadamu inayoambatanishwa na mazingira au watu wanaomzunguka.

Upo mfano hai. Mwaka 1994 yupo mkulima alinunua miche ya miti aina ya girevelia ipatayo 60; miche 56 aliiotesha na minne iliyobaki aliipanda kwenye ndoo. Yote alikuwa akiinyunyizia maji kwa mwezi mmoja ila aliyoipanda shambani iliendelea kukua, baada ya miaka 13 ilikuwa mikubwa. Aliivuna na akapasua mbao, alipata 688 za tatu kwa mbili.

Japo ile ya kwenye ndoo nayo ilikaa kwa miaka 13 ila haikuongezeka kimo. Na ingawa alikuwa na uwezo wa kuihamisha kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine, hakufanya hivyo.

Kuna kitu cha kujifunza kutokana na kitendo hiki. Miti yote ilikuwa na uwezo kutoa mbao lakini kufanikiwa kufanya hivyo ilitegemea nafasi iliyopandwa. Ile ya kwenye ndoo ilishindwa kufikia mafanikio ya kutoa mbao kwa sababu ilibanwa na mizizi yake haipata nafasi ya kutambaa na kufika mbali kuchukua virutubisho vyote muhimu vya kuufanya mti uwe mkubwa kiasi cha kuchanwa.

Pia, unapaswa kujifunza. Yawezekana kabisa una uwezo wa kufanya makubwa lakini mazingira unayoishi au mazingira unayofanyia kazi yanakubana na kukufanya usisogee kiroho, kiuchumi, kielimu, kiafya hata kiakili.

Yapo mambo ya kuzingatia kuondoka kwenye changamoto hii. Kwanza angalia namna unavyoutumia muda wako, ni kwa kiasi gani unauelekeza kwenye mambo yenye tija? Marafiki zako wa karibu wanakufanya ustawi au wanazuia ustawi wa maisha yako?

Ipo dhana kwamba; wewe ni mfano wa watu watano wanaokuzunguka. Pia, kazi unayoifanya sasa ina nafasi ya kukufanya ustawi au inakudumaza. Watu wanaokuzunguka pia uchangia kwa asilimia fulani katika mafanikio yako.

Hili linajumuisha elimu uliyonayo ambayo inapaswa kukupa uwanja wa kufanikiwa. Hii siyo lazima iwe ya darasani yenye vyeti na majina mkubwa kama udaktari au uprofesa, bali yaweza kuwa katika eneo unalojishughulisha nalo.

Mwisho ni tabia na mwenendo wako. Mafanikio yako huenda yakawa yanatokana na sifa hii kwa kiasi kikubwa. Ni kama ile miti iliyopandwa kwenye ndoo, ikihamishiwa shambani itakuwa na uwezo wa kukua hatimaye kuchanwa mbao.

Upo uwezo ndani yako ambao unaweza kukufanya ukawa wa tofauti ambao huenda unakandamizwa na nafasi uliyopo kwa sasa. Unachotakiwa kufanya ni kutambua kinachokukwamisha ili uchukue hatua za kufanya mabadiliko katika kujenga uchumi imara na kuondoka kwenye kundi la wasio na uhakika wa fedha.