Wachezaji wa Tanzania kusukiwa mipango England, Finland

Muktasari:

  • Asema kuwa atafanya mazungumzo na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia Benki ya Standard Chartered ili kuona wanafanya jitihada ili kuwawezesha wachezaji wa Tanzania kucheza soka nchini Uiengereza na nchi nyingine kama Finland.

Dar es Salaam. Gwiji la soka la klabu kongwe barani Ulaya, Liverpool, Sami Hyypia amesema wachezaji wenye vipaji wa Afrika pamoja na Tanzania wana fursa kubwa kucheza soka la kulipwa nchini Uingereza na nchi nyingine endapo wataongeza bidii.

Hyypia ambaye Jumamosi atazindua mashindano ya Standard Chartered Cup pamoja na Waziri wa Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo kwenye viwanja vya Dar es Salaam Gymkhana amesema kuwa kwa sasa kuna wachezaji wengi wenye vipaji ambao wanatamba Uingereza kutokana na kuongeza bidii.

Amesema kuwa tangu enzi ya Tony Yeboah ambaye alicheza naye, kwa sasa kuna wachezaji kama Sadio Mane, Mohamed Salah na wengine wengi wanaotamba katika ligi mbalimbali barani Ulaya na mabara mengine.

Amesema kuwa atafanya mazungumzo na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia Benki ya Standard Chartered ili kuona wanafanya jitihada ili kuwawezesha wachezaji wa Tanzania kucheza soka nchini Uiengereza na nchi nyingine kama Finland.

“Kwa sasa nipo nchini na bahati nimekutana na viongozi wa TFF hasa kocha wa Serengeti Boys, Oscar Mirambo na Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Salum Madadi, pia nitakutana na Waziri wa Michezo, nini kitafanyika, naomba msubiri,” alisema Hyypia.

Awali, Mkurugenzi wa benki ya Standard Chartered, Sanjay Rughani alisema kuwa wamefarijika sana kwa ujio wa Hyypia na mbali ya kuzindua mashindano Standard Chartered Cup Jumamosi, pia atakutana na watoto mbalimbali ambao wazazi wao wana akaunti kwenye benki yao na pia mashabiki wa timu wa Liverpool.

Rughani alisema kuwa Hyypia pia atakutana na wachezaji 224 kutoka timu 32 zitakazoshiriki katika mashindano ya mwaka huu ambapo mshindi atapata fursa ya kwenda Liverpool, mwezi  Septemba.

“Maandalizi yamekamilika na timu zote zipo tayari kwa mashindano, ili kuonyesha kuwa tupo katika jamii, Hyypia pia atakutana na watoto yatima na kushiriki nao katika shughuli maalum,” alisema Rughani.