Namba za Yanga zilivyotawala Ligi Kuu Bara

Muktasari:

  • Yanga inapewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu ikiwa na pointi 68 baada ya kucheza michezo 26, ikiwa imebakiza michezo minne tu ili imalize msimu wa ligi lakini inatakiwa kupata pointi nne tu kati ya 12 itangazwe kuwa mabingwa msimu hii.

Dar es Salaam. Ushindi wa bao 1-0 ambao Yanga iliupata juzi Jumatano dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi, ulikifanya kikosi hicho cha Miguel Gamondi kuweka rekodi tatu tofauti huku wakiendelea kuunyemelea ubingwa wa 30 wa Ligi Kuu Bara.

 Yanga inapewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu ikiwa na pointi 68 baada ya kucheza michezo 26, ikiwa imebakiza michezo minne tu ili imalize msimu wa ligi lakini inatakiwa kupata pointi nne tu kati ya 12 itangazwe kuwa mabingwa msimu hii.

Timu hiyo iliyo chini ya kocha Miguel Gamondi imekuwa ikionyesha kiwango cha juu na inaongoza kwenye asilimia 90 ya takwimu za ligi msimu huu hadi sasa.

Mchezo wa juzi ambao Yanga ilishinda bao 1-0 dhidi ya Kagera kwenye Uwanja wa Chamazi umeifanya kuwa timu pekee msimu huu wa 2023/24, iliyoshinda dhidi ya wapinzani wote 15, wanazoshiriki Ligi Kuu Bara.

Kagera Sugar inayonolewa na Fred Felix Minziro ndio timu pekee ambayo ilikuwa imeiwekea ngumu Yanga kutokana na mchezo wa kwanza kule Kagera kwenye Uwanja wa Kaitaba kumalizika kwa suluhu, hivyo Gamondi na vijana wake ilibidi watumie nguvu ya ziada ili kuweka rekodi hiyo.

Kwenye michezo hiyo, Yanga imekusanya pointi 68 ikifunga mabao 57 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 12 tu, ikiwa ndiyo timu iliyofunga mabao mengi hadi sasa msimu huu ikifuatiwa na Azam iliyofunga 52 na Simba 50, lakini ikiwa imepoteza michezo miwili tu dhidi ya Ihefu na Azam.

Rekodi nyingine iliyoweka Yanga ni kushinda michezo 25 mfululizo katika ligi tangu msimu uliopita, mara ya mwisho kwa Wananchi kudondosha pointi nyumbani ilikuwa Oktoba 23, 2022 ambapo ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi wa watani zao Simba mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa.

Kwa hesabu za msimu huu wa 2023/24, Yanga ina rekodi ya ushindi kwa asilimia 100 ikiwa nyumbani kuliko timu nyingine yoyote, imeshinda mechi zote 13, ikifuatiwa na Azam FC ambao katika michezo 13, imeshinda 10, sare mbili na kupoteza mara moja.

Watani wao Simba wenyewe inashika nafasi ya tatu katika michezo 12 imeshinda mara nane, sare mbili na kupoteza mara mbili.

Rekodi nyingine ambayo Yanga imeweka msimu huu baada ya kuibuka na ushindi dhidi ya Kagera Sugar ni kufikisha michezo mitano mfululizo katika mashindano yote  bila kuruhusu bao ambapo hakuna timu iliyofanya hivyo msimu huu. Michezo hiyo ni dhidi ya JKT Tanzania (0-0), Coastal Union (1-0), Tabora United (3-0), Mashujaa (1-0) na Kagera Sugar (1-0).

Katika michezo 10, iliyopita ya mashindano yote ikiwemo miwili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns, Yanga imeruhusu bao moja tu ambalo ni dhidi ya Simba lililofungwa na Freddy Michael wakati ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1 kwenye ligi.

Msimu uliopita:

Msimu uliopita wa 2022/23, Yanga na Simba hazikupoteza mchezo wowote nyumbani katika ligi, kila mmoja alishinda mechi 13, sare mbili kati ya mechi 15 hivyo zilivuna  pointi 41, Azam yenyewe ilishinda 12, sare moja huku ikipoteza mechi mbili ilikusanya pointi 37.

Hata hivyo, wachezaji wa timu hiyo wameonekana kutawala maeneo mengi muhimu kwenye ligi hadi sasa kwenye eneo la wafungaji, anaongoza Aziz Ki mwenye mabao 15 sawa na Feisal Salum Fei Toto, vinara wa pasi za mabao kwa upande wa mabao anaongoza beki wa Yanga, Koussi Yao mwenye pasi saba, kwa ujumla akiongoza Kipre Junior wa Azam, lakini kwa upande wa makipa Djigui Diarra wa timu hiyo anaongozo kwa clean Sheet akiwa nazo 13 mbele ya Ley Matampi wa Coastal Union  mwenye kumi.

Gamondi atoa neno

Licha ya ugumu wa michezo ambayo wamekumbana nayo, Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi ambaye alionekana katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar akigeuka mbogo kwa mwamuzi Abdallah Mwinyimkuu, amewapongeza wachezaji wake kwa namna ambavyo wamekuwa wakijitoa kuhakikisha wanafanya vizuri.

"Japo yapo matukio ambayo yamekuwa yakituumiza lakini lazima tukubali kwamba wachezaji wangu wamekuwa wakifanya kazi kubwa, tunatakiwa kuendelea na mapambano bila ya kuchoka na kuangali vikwazo vilivyopo," alisema.


Mechi zilizobaki:

Timu hiyo ina michezo minne iliyobaki kumaliza msimu huu katika ligi ambayo miwili ni ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar na Dodoma Jiji huku ikimalizia msimu nyumbani kwa kukabiliana dhidi ya Tabora United na Tanzania Prisons.