#WC2018: Javier Mascherano aongoza kwa kutoa pasi nyingi Russia

Muktasari:

  • Mascherano alicheza kwa kiwango bora mchezo dhidi ya Iceland waliotoka sare ya bao 1-1 ambapo alitoa pasi 141.

Moscow, Russia. Kiungo nguli wa Argentina, Javier Mascherano anaongoza kwa kutoa pasi nyingi katika Fainali za Kombe la Dunia nchini Russia.

Mascherano alicheza kwa kiwango bora mchezo dhidi ya Iceland waliotoka sare ya bao 1-1 ambapo alitoa pasi 141.

Licha ya mechi za mashindano hayo kuanza katika mzunguko wa pili jana, hakuna mchezaji aliyemfikia Mascherano kwa kutoa pasi nyingi katika mchezo mmoja.

Mascherano ambaye muda mrefu amekuwa akicheza nafasi ya beki wa kati katika kikosi cha Barcelona, mchezo dhidi ya Iceland alipangwa nafasi ya kiungo mkabaji (namba sita).

Kiwango bora cha Mascherano kimeibua mjadala baada ya kuonyesha uwezo mkubwa ingawa tayari ametangaza kuihama klabu yake ya Barcelona.

Nguli huyo anatarajiwa kucheza ligi ya nyumbani Argentina anakotarajiwa kumalizia soka kabla ya kutundika daluga.

Nafasi ya pili kwa mchezaji aliyetoa pasi nyingi ni nahodha wa Hispania na beki wa kati Sergio Ramos aliyetoa pasi 118 katika mchezo waliotoka sare ya mabao 3-3 dhidi ya Ureno.

Nafasi ya tatu inashikwa na beki wa Ubelgiji Toby Aldeweireld aliyetoa pasi 102 katika mchezo wa juzi walioshinda mabao 3-0 dhidi ya Panama.

Kiungo nyota mkabaji wa Ujerumani aliyetegemea kung’ara katika fainali hizo, Toni Kross anayecheza klabu ya Real Madrid, anashika nafasi ya 10 katika orodha ya wachezaji wenye majina makubwa waliotoa pasi nyingi hadi sasa katika fainali hizo.