Rita yapata dawa ya watoto wenye ‘baba wawili’

Muktasari:

Majibu ya swali hilo yalikuja baada ya ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Bukoba, Vivian Roland kutaka suala la namna hiyo lipatiwe ufumbuzi.

Bukoba. Swali lililoulizwa kutaka kujua hatima ya watoto wanaosajiliwa na kupewa vyeti vya kuzaliwa, lakini baadaye inathibitika kuwa kuna baba mwingine ambaye hakutajwa kwenye cheti, limetoa suluhu ya matukio ya namna hiyo.

Majibu ya swali hilo yalikuja baada ya ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Bukoba, Vivian Roland kutaka suala la namna hiyo lipatiwe ufumbuzi.

Kaimu meneja wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), Patricia Mputa alikuwa na jibu ambapo alisema wataanza upimaji wa vinasaba (DNA) katika kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wanaodhaniwa kuwa na baba zaidi ya mmoja.

Patricia alitoa kauli hiyo wakati wa mkutano baina ya watendaji wa Rita na viongozi wa Mkoa wa Kagera jana.

Alisema utata wa nani ni baba halisi wa mtoto utamalizwa na vipimo vya vinasaba kwa kuwa baadhi ya wanawake huandikisha majina ya baba wasio sahihi kwenye vyeti vya watoto.

“Kwa sababu wanazozijua wenyewe, wakati mwingine wanawake huandikisha majina ya baba mwingine ambaye si halisi kwenye cheti, lakini hilo huthibitishwa kwa DNA,” alisema Patricia.

Kadhalika, alisema wataanza kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto chini ya miaka mitano mkoani Kagera kupitia kwenye ofisi za kata na vituo vya tiba, huku akisisitiza kuwa visitiliwe shaka kwa kuwa vitaandikwa kwa mkono.

Alisema vyeti vilivyoandikwa kwa mkono hukataliwa katika baadhi ya maeneo na baadhi ya mamlaka, lakini ni halali na vinatakiwa kutambuliwa kama vile vinavyopitia kwenye mfumo wa kielektroniki.

“Utoaji wa vyeti hivyo unatarajiwa kuanza Oktoba kwa mkoa wa Kagera,” alisema.

Kaimu ofisa mtendaji mkuu wa Rita, Emmy Hudson alisema mpango huo utawawezesha watoto walio chini ya umri wa miaka mitano kusajiliwa na kupatiwa vyeti papo hapo ambapo awali huduma hiyo ilipatikana kwenye ofisi za wakuu wa wilaya.

“Tayari watoto milioni 2.7 wamesajiliwa na kupata vyeti kupitia mpango huu katika mikoa sita nchini na vituo vyote vya usajili vitapewa simu za kiganjani kwa ajili ya kutuma taarifa za waliosajiliwa ambazo zitaingizwa kwenye kanzidata ya wakala,” alisema.

Pia alisema hata watoto ambao si raia wanaozaliwa kwenye kambi za wakimbizi wana haki kupata vyeti.