Sh1 bilioni kutekwa Mo Dewji zakosa mtu




Muktasari:

  • Familia ya mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo’ imesema donge nono la Sh1bilioni iliyoahidi kwa yeyote atakayefanikisha kupatikana kwa bilionea huyo haitatolewa kwa kuwa mfanyabiashara huyo ndiye aliyempiga simu baba yake kumueleza mahali alipo baada ya kutelekezwa na waliomteka katika viwanja vya Gymkhana

Dar es Salaam. Gullam Hussein Dewji, baba wa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo’ amesema Sh1 bilioni ambazo familia yake iliahidi kumpatia mtu ambaye angefanikisha kupatikana kwa mwanaye hazitatolewa.

Akizungumza na Mwananchi jana Gullam alisema hakuna aliyefanikiwa kupata fedha hizo kwa kuwa Mo alipoachiwa na watekaji, ni yeye mwenyewe ambaye aliomba msaada wa simu katika Hoteli ya Southern Sun jijini hapa.

Alisema hakuna aliyewasiliana na familia hiyo na kutoa maelezo yaliyosaidia kupatikana kwake.

Oktoba 11, Mo alitekwa na watu wasiojulikana katika Hoteli ya Colosseum alipokuwa amekwenda kufanya mazoezi na kupatikana juzi saa 7:30 usiku baada ya watekaji hao kumtelekeza katika Viwanja vya Gymkhana.

Jumatatu iliyopita, familia hiyo ilitangaza dau la Sh1 bilioni kwa mtu yeyote ambaye angewezesha kupatikana kwa bilionea huyo kijana.

Taarifa ya familia ilisomwa mbele ya wanahabari na Azim Dewji ilisema ambaye angetoa taarifa hizo zingekuwa za siri.

Jana, Gullam mbali na kuzungumzia afya ya mwanaye kuzidi kuimarika, alitoa ufafanuzi kuhusu fedha hizo, “Nilikwenda kumchukua mwanangu katika Hoteli ya Southern Sun iliyopo umbali mfupi kutoka eneo la Gymkhana ambako alikwenda kuomba msaada.”

Kwa hiyo hakuna aliyefanikiwa kuipata kwa kuwa Mo mwenyewe ndiye aliyepiga simu kwa baba yake baada ya kufika katika hoteli hiyo na kuomba kuwasiliana naye.

“Alipopata ile nafasi alitembea umbali mfupi mpaka pale Southern Sun na alipofika pale akaomba msaada wa kupiga simu ili awasiliane na mimi, alinipigia nikamfuata.

“Ndugu yangu hiyo zawadi kama nilivyokwambia simu alipiga Mohammed mwenyewe akinipigia mimi sio kwamba mtu alinipigia akaniambia kwamba mwanangu yuko wapi,” alisisitiza.

Afya ya Mo

Kuhusu afya ya mwanaye alisema, “Mohamed anaendelea vizuri mpaka sasa tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kweli. Unajua sisi kama familia hatuwezi kusema zaidi mambo ya kiuchunguzi yapo chini ya Jeshi la Polisi wao ndiyo wenye mamlaka hayo.”

Alipoulizwa kuhusu kusambaa kwa taarifa za kupatikana kwa Mo mitandaoni, zikiwamo zilizotolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, Gullum alisema, “Baada ya kupatikana (Mo) watu wengi walijua na yeye pia (Makamba) alijua. Mtu wa kwanza kujua nilikuwa ni mimi hakuna mtu mwingine.”

Alishokisema Makamba

Alipoulizwa kuhusu kuwa mtu wa kwanza kusambaza taarifa za kupatikana kwa Mo katika ukurasa wake wa Twitter, Makamba alisema ilitokana na ukaribu aliokuwa nao na familia hiyo baada ya bilionea huyo kutekwa.

Katika ukurasa huo wa Twitter Makamba ameandika, “Mohammed Dewji amerudi nyumbani salama. Nimezungumza naye kwa simu dakika 20 zilizopita. Sauti yake inaonyesha yu mzima bukheri wa afya. Shukrani kwa wote kwa dua na sala. Naenda nyumbani kwake kumuona muda huu.”

Kitendo hicho kiliibua maswali mengi mitandaoni, watu wa kada mbalimbali wakihoji nani alianza kuwasiliana na mwenzake, kati ya Makamba na Mo.

“Tangu kutekwa kwa Mo mimi nimekuwa karibu sana na familia yake, katika kipindi chote alichotekwa nilikuwa nawatembelea. Lakini mimi ni mtu wa karibu sana na Mo, tumejuana zaidi ya miaka 10.

“Kwa hiyo alipopatikana baba yake (Gullam) alinipigia simu na kuniambia kuna jambo la furaha kwamba amepatikana na akampa simu azungumze na mimi. Nakumbuka ilikuwa saa 9.09 usiku.”

Aliongeza, “Kwa kuwa hapa ninapoishi na kwa Mo ni kama dakika tano, nikasema siwezi kulala acha niende kumwona. Nilipofika ilikuwa furaha tulisalimiana na tukazungumza.”

Alisema wakati anakwenda kumuona mfanyabiashara huyo, polisi walikuwa hajafika nyumba kwa mfanyabiashara huyo.

Mchungaji aitaka Sh1bilioni

Lakini wakati Gullam akisema hakuna anayestahili Sh1 bilioni kwa kuwa hakuna aliyetoa taarifa zilizowezesha kupatikana kwa mtoto wake, jana mchungaji wa mitume, manabii na maaskofu Tanzania wa Kanisa la Emmaus Bible Church Pentecostal lililopo Mbezi Kibanda cha Mkaa, Dar es Salaam, Komando Mashimo alisema anapaswa kupewa yeye.

Akizungumza katika ibada ya kumshuruku Mungu baada ya kupatikana kwa bilionea huyo alisema, “Naweza kusema hiyo fedha ni yangu kama ataamua kutoa maana nimetabiri ataonekana na ameonekana. Ikitokea amekubali kunipa nitamuomba anijengee kanisa.”

Askofu Gwajima anena

Pia, Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima jana alizungumzia tukio hilo akiwataka waumini wake kuendelea kuliombea Taifa kwa sababu Mungu anasikiliza maombi yao ikiwamo kupatikana kwa Mo.

Alitoa kauli hiyo katika ibada kanisani hapo na kusema wiki iliyopita walimwombea kama ambavyo wamekuwa wakiliombea Taifa na viongozi wake, kama walivyoomba wakati wa mauaji yaliyotikisa Mkoa wa Pwani, hasa Kibiti, Mkuranga na Rufiji.

“Tuendelee kuwa watiifu katika kuliombea Taifa letu. Mungu wetu anasikia,” alisema Gwajima huku waumini wake wakipiga makofi na kushangilia.

Wafanyabiashara na usalama

Baadhi ya wafanyabiashara wamezungumzia kupatikana kwa mfanyabiashara huyo na kulishauri Jeshi la Polisi kuimarisha ulinzi ili kujenga imani kwa wawekezaji.

Wafanyabiashara hao pia walikosoa kauli ya Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro kwamba wenye uwezo wa kifedha wachukue tahadhari kwa kuwa na silaha ili kujihakikishia ulinzi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye alisema utekaji wa mwekezaji huyo ulijenga hofu.

“Kwa niaba ya sekta binafsi tumefurahi amepatikana akiwa salama. Tulikuwa na wasiwasi maana utekaji huu ungeweza kuleta sintofahamu kwa wawekezaji wengine,” alisema Simbeye.

Kuhusu kumiliki silaha, alisema ni pendekezo zuri lakini Polisi pia wanatakiwa kujiimarisha kimfumo katika kukabiliana na uhalifu.

“Watu wanaweza kujilinda wenyewe lakini ni lazima tuimarishe mifumo yetu ya ulinzi wa raia na mali zao, watu wanatumia mitandao sana kwa sasa kwa hiyo Polisi nao wajiongeze ili kukabiliana na hilo,” alisema.

Mwenyekiti mstaafu wa Umoja wa Maofisa Watendaji wakuu wa Kampuni Binafsi (CEO’s Roundtable), Ali Mufuruki alishauri polisi kutimiza wajibu katika kuimarisha ulinzi wa raia na mali zao.

Alisema Serikali inatakiwa kuwekeza kikamilifu katika kuimarisha usalama nchini vinginevyo inaweza kuharibu taswira ya Taifa na kuvuruga mipango ya ushawishi wa uwekezaji katika sekta ya viwanda nchini.

Mwenyekiti wa zamani wa Jumuiya ya Wafanyabiashara nchini (JWT), Johnson Minja alisema, “Nashauri Polisi wajitathmini wenyewe katika utekelezaji wa majukumu yao. Ni muhimu watekaji wakawa wanakamatwa na kuchukuliwa hatua ili Polisi iwe na jambo la kujivunia.

“Kutembea na silaha inaweza kumsaidia mtu kukabiliana na matukio madogo lakini haiwezi kusaidia katika matukio makubwa ya uhalifu kama lile la Mo Dewji, tunahitaji ulinzi unaoweza kumhakikishia usalama kila mmoja wetu bila kuwa na silaha, “ alisema.

Imeandikwa na Khatimu Naheka na Peter Elias na Kelvin Matandiko.