Tatizo la kukatika umeme Dar kumalizika Mei
Muktasari:
- Akizungumza jana baada ya kutembelea vituo vya Mbagala, Kurasini na Kariakoo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dk Tito Mwinuka alisema tatizo hilo linatokana na miundombinu kuzidiwa na watumiaji.
Dar es Salaam. Uongozi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), umesema tatizo la kukatika kwa nishati hiyo mara kwa mara jijini hapa litamalizika kabla ya Mei, baada ya ujenzi wa vituo vya kusafirisha na kupooza umeme kukamilika.
Akizungumza jana baada ya kutembelea vituo vya Mbagala, Kurasini na Kariakoo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dk Tito Mwinuka alisema tatizo hilo linatokana na miundombinu kuzidiwa na watumiaji.
“Kama mnavyofahamu, Jiji la Dar es Salaam linakua kwa kasi, tunahitaji miundombinu itakayohimili ongezeko kubwa la watu na viwanda,” alisema.
Mwinuka aliyefanya ziara hiyo ya kwanza tangu ateuliwe na Rais John Magufuli mwezi uliopita, alisema kukamilika kwa vituo vya kusafirisha na kupooza umeme vya Mbagala, Kurasini na Kariakoo, kutamaliza tatizo hilo.