Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Asimulia jinsi mtoto wa aliyeuawa Uingereza alivyopambana kuokoa uhai wa mama yake

Muktasari:

Akizungumza na Mwananchi ameeleza namna Tyrese Mahmoud (12), ambaye ni mtoto wa Leyla alivyopambana kuokoa uhai wa mama.

Arusha/Dar. Ndugu wa Leyla Mtumwa (36), Mtanzania aliyeuawa nchini Uingereza kwa kuchomwa kisu na mumewe, amesimulia namna mtoto wa miaka 12 alivyopambana kuokoa uhai wa mama yake.

Akizungumza na Mwananchi ameeleza namna Tyrese Mahmoud (12), ambaye ni mtoto wa Leyla alivyopambana kuokoa uhai wa mama.

Abdulkarimu Mtumwa ambaye ni mdogo wa Leyla anayeishi Arusha alisema hayo akikariri maelezo aliyopewa na Tyrese kuhusu tukio hilo.

Mtumwa alisema mtoto huyo bila mafanikio aliingilia kati kujaribu kuzuia ugomvi kati ya mama na baba yake, Kema Kasambula (38).

Alisema Kasambula ambaye pia ni Mtanzania waligombana na Leyla usiku wa Machi 30 eneo la Haringey Kirkstall Avenue, London N17 jijini London.

Mtumwa alimkariri Tyrese akisema kwamba kushindwa kuamua ugomvi huo, alitoka nyumbani na kwenda kupiga simu kitengo maalumu cha polisi cha makosa ya jinai.

“Hadi alipoondoka kwenda kupiga simu Leyla alikuwa bado hajachomwa visu na mumuwe. Aliporudi alikuta tayari amechomwa visu na muda mfupi polisi walifika,” alisema.

Mtumwa alisema baada ya tukio hilo, Kasambula hakuondoka nyumbani na polisi walipofika walimchukua.

Alisema Tyrese alizaliwa na Leyla kabla ya kuoana na Kasambula mwaka jana.

Akizungumzia ndoa ya ndugu yake, alisema ilifungwa mwanzoni mwa mwaka jana na Desemba waliondoka kwenda kuishi Uingereza.

Mtumwa alisema kabla ya kuondoka nchini, Leyla alifanya kazi katika kampuni za simu za Zantel na Airtel jijini Dar es Salaam.

Kuhusu utaratibu wa mazishi, alisema familia inaomba kusaidiwa ili Leyla azikwe nchini.

“Tunasubiri kupata mrejesho kutoka Uingereza lakini familia tunaomba sana aje kuzikwa Arusha. Kutokana na sikukuu hatujapata uhakika lini utaratibu wa mazishi utakamilika,” alisema.

Mwenyekiti wa Jumuiya Kuu ya Watanzania inayotambuliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza, Joe Warioba alisema jana kuwa mwili wa Leyla utasafirishwa kurejeshwa nchini uchunguzi utakapokamilika.

Warioba alisema ni mapema kutaja siku ambayo mwili huo utasafirishwa kutokana na utaratibu ulivyo kwa matukio ya mauaji.

“Jambo hili mpaka sasa bado liko chini ya polisi ambao wanaendelea na utaratibu wa kawaida, ikiwamo uchunguzi na upelelezi ili kujiridhisha na tukio hilo. Wakimaliza watatukabidhi mwili wa mpendwa wetu,” alisema Warioba.

Alisema hivi sasa Watanzania waishio Uingereza wanachangishana fedha kwa ajili ya kusafirisha mwili wa Leyla kuurejesha nchini.

Warioba alisema hawajajua ni gharama kiasi gani zitatumika kufanikisha jambo hilo kwa sababu bei kwa usafiri wa ndege hubadilika.

Hidaya Mtumwa ambaye ni mama wa Leyla ni maarufu jijini Arusha aliyewahi kuimbwa katika moja ya nyimbo za mwanamuziki Pepe Kale.

Juzi, Hidaya alisema muda mfupi kabla ya kifo cha mtoto wake, walizungumza akijiandaa kurejea nyumbani akiwa na rafiki zake na neno lake la mwisho aliahidi angempigia simu baadaye kwa kuwa alikuwa akiwahi teksi.

Mtumwa alisema katika familia yao, Leyla alikuwa mtoto wa kwanza kati ya watano na sasa wamebaki watatu.