Askofu ajitoa mhanga kilio cha Katiba mpya

Askofu wa Jimbo la Katoliki, Rulenge Wilaya ya Ngara mkoani Kagera, Severine Niwemugizi akizungumza wakati wa mkutano wa asasi za kiraia uliofanyika jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa na kulia ni Mwenyekiti wa mtandao huo, Martina Kabisa. Picha na Ericky Boniphace.

Muktasari:

  • Askofu Niwemugizi, ambaye alikuwa akizungumza katika mkutano wa zaidi ya asasi 80 za kiraia, ametoa kauli hiyo siku moja baada ya Jukwaa la Katiba kusema linaandaa maandamano ya amani kumueleza Rais John Magufuli umuhimu wa kuandika Katiba Mpya.

Dar es Salaam. Wakati mjadala wa kufufua mchakato wa Katiba Mpya ukionekana kuanza kushika kasi, Askofu Severin Niwemugizi wa Kanisa Katoliki Ngara, ameongeza uzito, akisema yuko tayari “kuitwa mchochezi” endapo juhudi za kudai nyaraka hiyo zitatafsiriwa tofauti.

Askofu Niwemugizi, ambaye alikuwa akizungumza katika mkutano wa zaidi ya asasi 80 za kiraia, ametoa kauli hiyo siku moja baada ya Jukwaa la Katiba kusema linaandaa maandamano ya amani kumueleza Rais John Magufuli umuhimu wa kuandika Katiba Mpya.

Huku vuguvugu hilo likiendelea kushika kasi, mbunge wa Singida Kaskazini (CCM), Lazaro Nyalandu jana alidokeza katika ukurasa wake wa Twitter kuwa suluhisho la Tanzania kwa sasa ni Katiba Mpya pekee.

Katika mkutano huo, asasi hizo zilisema umefika wakati mwafaka wa mchakato wa Katiba kuanza upya ili ifikapo 2020  iwe imepatikana.

Rais Magufuli ameshasema kuwa Katiba Mpya si kipaumbele chake na wala hakutaja suala hilo wakati wa kampeni zake na hakuna mtu ambaye ameshtakiwa au kukamatwa kwa kuzungumzia suala hilo.

Lakini jana, Askofu Niwemugizi alisema ili mambo mazuri anayofanya Rais yaweze kuendelezwa, ni muhimu kuwa na Katiba Mpya itakayoweka mwongozo.

Alisema akiwa kiongozi wa dini anaongozwa na maadili, haki na ukweli, hivyo hajali namna wengine watakavyomchukulia.

Akifungua mkutano wa asasi hizo uliolenga kujadili Katiba Mpya jijini Dar es Salaam jana, Askofu Niwemugizi alisema imefika wakati nchi inahitaji kuwa na dira nzuri.

Alisema hakuna mtetezi wa haki za binadamu anayetaka nchi iingie kwenye machafuko kwa kuwa lengo lao wote ni kuchochea maendeleo, amani na utulivu.

Askofu huyo alisema kuibuka kwa matukio ya kuteka watoto, vifo katika mazingira ya kutatanisha na ongezeko la watu wasiojulikana kushambulia wananchi, ni ishara mbaya.

“Hizi si dalili nzuri kwa Taifa lenye afya njema. Ni vielelezo vyenye dira mbaya. Imefika wakati tukae kama Taifa tukubaliane kuwa tunataka dira njema ambayo ni Katiba,” alisema kiongozi huyo wa kidini.

Alisema anatambua jitihada anazofanya Rais John Magufuli katika kupambana na ufisadi na kutaka rasilimali ziwanufaishe wanyonge, lakini ni muhimu juhudi hizo zilindwe na Katiba nzuri.

“Rais anafanya mengi mazuri na alipoanza kila mmoja aliona dalili za matumaini lakini juhudi hizo zinaweza zisiwe endelevu kama hakuna ulinzi wa Katiba,” alisema.

“Tunahitaji Katiba tena Katiba nzuri ambayo haitaruhusu kuchezewa na yeyote kwa masilahi au matakwa yake binafsi.

“Namshauri Rais achunguze kwa makini yatakayozungumzwa kwenye mkutano huu, ayaone kuwa yana nia njema na ayafanyie kazi.”

Askofu Niwemugizi alisema yeye ni miongoni mwa watu wa kwanza kusikia kuhusu azma ya Serikali ya Awamu ya Nne kuanzisha mchakato wa kuandika Katiba Mpya.

“Nakumbuka siku hiyo nilikuwa nyumbani kwa Waziri Mkuu (wa awamu hiyo, Mizengo) Pinda, nikiwa pale Rais Jakaya Kikwete alimpigia simu,” alisema.

“Walikuwa wakiongea na kuweka mipango ya namna ya kutekeleza azma hiyo. Nikaona ni jambo jema na hatimaye mchakato ukaanza.

“Lakini pia mimi nikawa miongoni mwa watu waliokuwa wakipinga mwenendo wa mchakato huo na namna ulivyokuwa ukiendeshwa hadi tukaonekana watu wasiofaa.”

Alisema akiwa kiongozi wa dini, ilifika wakati alitamani mchakato huo usifanikiwe na ikawa hivyo.

Alidai kuwa kuna wakati pia alikutana na kiongozi mmoja wa juu wa CCM ambaye alimwambia kuwa mchakato wa Katiba umewagawa Watanzania.

“Alionyesha kuwa na hamu ya kulirudisha Taifa katika mwafaka wa kitaifa, nami nikamwambia namuunga mkono kwa asilimia 200,” alisema akimtaja kigogo huyo ambaye tumemsitiri jina kwa sababu za kimaadili.

“Nikamwambia yaani hivi unavyoniona hapa naonekana ni mtu ninayepinga mchakato wa Katiba, napinga Serikali. Hiyo ni kwa sababu niliweka wazi kuwa endapo Bunge la Katiba litachakachua mchakato wa kupata Katiba, nitakuwa wa kwanza kusimama na kuwaambia watu waikatae. Basi tangu hapo nikaonekana mpinzani.”

Mchakato wa Katiba Mpya ulikwama katika hatua ya kupiga kura ya maoni kupitisha Pendekezo la Katiba Mpya baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kueleza kuwa haingeweza kuandaa kwa wakati mmoja na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Hata hivyo, mchakato huo uliingia dosari baada ya kundi la wajumbe wa Bunge la Katiba, wakiongozwa na vyama vinne vya upinzani, kususia vikao kwa madai kuwa wenzao waliacha mapendekezo ya wananchi yaliyokuwa katika Rasimu ya Katiba na kuingiza utashi wa chama tawala.

Katika mkutano wa jana, mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Olengurumwa alisema Serikali ifufue mchakato huo wakati huu.

“Tunataka tunapokwenda kwenye uchaguzi (2020) tayari tuwe na Katiba. Maandalizi hayo yanatakiwa kuanza sasa tusisubiri,” alisema.

“Kama Rais anavyotaka tumuombee, basi aweke mbele Katiba kama silaha yake. Hiyo ndiyo itatupa mwanga wa masuala yote mazuri anayoyapenda. Ndani yake yatakuwepo masuala ya viwanda, hapa kazi na maendeleo kwa ujumla.

“Kuna nchi zimeandika Katiba Mpya baada ya kuingia kwenye machafuko. Sisi hatutaki tufike huko,  nimsihi Rais asimamie.”

Mwanasheria wa kujitegemea, Harold Sungusia alisema ni muhimu Katiba ipatikane ili kusimamia mambo yanayoonekana kwenda mrama.