Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maudhui ya ndani ajenda muhimu sekta ya madini

Picha ikionesha madini. Picha na Mtandao

Muktasari:

  • Kongamano la mwaka la uzingatiaji wa maudhui ya ndani linafanyika jijini Mwanza, likiwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya madini.

Mwanza. Wadau wa sekta ya madini watakutana jijini Mwanza kujadili namna ya kuongeza ushiriki wa Watanzania katika shughuli za uchimbaji, ununuzi wa bidhaa na huduma, ajira, pamoja na uongozi wa kampuni zinazofanya kazi katika sekta hiyo.

Majadiliano hayo yatafanyika kuanzia kesho, Jumatano, Julai 22 hadi 24, 2026, katika kongamano la mwaka la uzingatiaji wa maudhui ya ndani (LCCF), lililoandaliwa na Tume ya Madini kwa lengo la kutathmini hatua zilizofikiwa na changamoto zilizopo katika utekelezaji wa sera hiyo.

Kongamano hilo litawakutanisha viongozi wa Serikali, kampuni za madini, wakandarasi, wasambazaji wa bidhaa na huduma, pamoja na wataalamu wa sekta hiyo kujadili namna ya kuongeza manufaa ya rasilimali madini kwa wananchi.

Ajenda ya maudhui ya ndani imeendelea kupata uzito nchini katika miaka ya karibuni, huku Serikali ikiimarisha sheria na kanuni zinazolenga kuongeza ushiriki wa Watanzania katika mnyororo mzima wa thamani wa madini.

Kanuni za Madini (Maudhui ya Ndani) za mwaka 2018, pamoja na marekebisho yaliyofanyika mwaka 2025, zimeweka masharti yanayotaka kampuni za madini kutoa kipaumbele kwa bidhaa, huduma na wataalamu wa Kitanzania pale inapowezekana.

Marekebisho hayo pia yameongeza wajibu wa kampuni kuwasilisha mipango ya ununuzi, matumizi ya huduma za kifedha na kushirikisha wazawa kupitia ubia katika baadhi ya shughuli za biashara zinazohusiana na madini.

Katika kongamano hilo, kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) itashiriki kama mdhamini wa ngazi ya Gold, huku ikitaja hatua mbalimbali ilizochukua katika kuendeleza ushiriki wa Watanzania katika shughuli zake.

Kwa mujibu wa takwimu za kampuni hiyo, zaidi ya watu 7,000 wameajiriwa katika shughuli zake, na asilimia 98 ni Watanzania. Kampuni hiyo pia imeeleza kuwa zaidi ya asilimia 80 ya nafasi za juu za uongozi zinashikiliwa na wazawa.

Mbali na ajira, kampuni hiyo imekuwa ikifanya kazi na zaidi ya biashara ndogo na za kati 600 za Kitanzania zinazoshiriki katika ugavi wa bidhaa na huduma kwa shughuli zake za uzalishaji.

Akizungumzia kongamano hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Ashraf Suryaningrat, amesema maendeleo ya kampuni hiyo yamejengwa juu ya uwekezaji wa muda mrefu katika kukuza uwezo wa wafanyakazi wa Kitanzania.

Amesema katika kipindi cha zaidi ya miaka 25, kampuni imeendelea kuwekeza katika mafunzo, ukuzaji wa taaluma na uhamishaji wa ujuzi ili kuhakikisha Watanzania wanashiriki kikamilifu katika nafasi za kiufundi na kiutawala.

Wakati huohuo, Tume ya Madini, katika taarifa yake, imesisitiza umuhimu wa kampuni zote zinazofanya shughuli za madini kuzingatia kikamilifu matakwa ya maudhui ya ndani kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo.

Tume hiyo imeeleza kuwa itaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa mikataba ya wakandarasi, wasambazaji na mipango ya kampuni ili kuhakikisha fursa zinazotokana na sekta ya madini zinawanufaisha Watanzania kwa kiwango kikubwa zaidi.