Hoja nzito tano wiki ya kwanza ndani ya Bunge

Dodoma. Hoja tano zilizoibuka ndani ya Bunge tangu lilipoanza mwanzoni mwa wiki, ziliutikisa mhimili huo wa kutunga sheria na kusababisha mijadala mizito kutoka kwa wabunge wa CCM na upinzani.

Katika mkutano huo wa 13 wa Bunge ulioanza Novemba 6, wabunge walitumia fursa hiyo kujadili masuala mbalimbali yaliyomo na yasiyokuwamo ndani ya Mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa 2019/2020.

Hadi juzi, mkutano huo ulikuwa umekaa vikao vinne na kuibuka kwa hoja hizo ambazo ni sakata la korosho; matukio ya utekaji hasa lililomtokea mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji ‘Mo’ na mdahalo wa uchumi na siasa uliofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Novemba Mosi.

Zingine ni suala la mazingira ya biashara kutokuwa rafiki kwa wafanyabiashara na la Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isaack Kamwelwe kunyooshewa kidole na wabunge kwamba ana majibu ya jeuri na dharau.

Kati ya mambo yaliyojadiliwa zaidi ndani ya siku hizo ni la korosho ambalo wabunge wengi waliitaka Serikali kutotumia nguvu na kuacha soko litawale.

Miongoni mwa wabunge waliozungumzia suala hilo ni Tulia Malapo (viti maalum-Chadema), Katani Katani (Tandahimba-CUF), Abdallah Chikota (Nanyamba-CCM), Peter Serukamba (Kigoma Kaskazini-CCM), Ahmed Shabiby (Gairo-CCM) na Hamidu Bobali (Mchinga-CUF).

Hoja nyingine ni ya mazingira ya biashara ambapo wabunge waliitaka Serikali kuyaangalia upya kwa sababu yamekuwa yakiwafanya baadhi ya wafanyabiashara kukimbia nchini. Baadhi ya wabunge waliochangia suala hilo ni Mussa Zungu (Ilala-CCM), Hussein Bashe (Nzega Mjini-CCM) na Lucy Mayenga (viti maalumu-CCM) ambao walisema bila kufanya hivyo wafanyabiashara wataendelea kukimbia.

Matukio ya utekaji ni miongoni mwa hoja zilizozungumzwa na mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa aliyeibua hoja ya kutekwa kwa ‘Mo’. Mfanyabiashara huyo alitekwa Oktoba 11 na kupatikana Oktoba 20 jijini Dar es Salaam.

Katika hoja hiyo, mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche aliigusia akisema matukio hayo yamekuwa yakiwafanya watu kupoteza imani na Serikali, huku akiitaka kuwaeleza Watanzania imewasaidiaje wanyonge kuondokana na umaskini.

Ndani ya siku hizo nne, hazikumuacha salama Waziri Kamwelwe ambaye alijikuta akinyooshewa kidole na wabunge waliodai kuwa huwatolea majibu ya dharau ambayo hata Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa hayatoi.

Wabunge hao ni Seleman Bungara ‘Bwege’ (Kilwa Kusini-CUF), Ramadhan Dau (Mafia-CCM) na Mohamed Mchengerwa (Rufiji-CCM). Bwege alisema majibu ya waziri huyo yanaonyesha dharau kwa Waziri Mkuu, Majaliwa ambaye ameteuliwa na Rais Magufuli kisha kuthibitishwa na Bunge. Hata hivyo, Kamwelwe alijibu moja ya tuhuma hizo akisema hazina ukweli wowote.

Sugu, Msukuma

Wabunge Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ (Mbeya Mjini–Chadema) na Joseph Kasheku ‘Msukuma’ (Geita-CCM) ndiyo pekee ambao waliwakosoa maprofesa walioshiriki mdahalo wa siasa na uchumi wa miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Tano ulioandaliwa na UDSM.

Wabunge hao walisema maprofesa hao hawakuwatendea haki Watanzania kwa sababu hoja zao zilikuwa za kusifia na kurudia hotuba zinazotolewa na Rais Magufuli.

Hata hivyo, alipoulizwa na Mwananchi, mwenyekiti wa mdahalo huo, Profesa William Anangisye aliwatetea akisema hakuna profesa wala mtu aliyepangiwa jambo la kuzungumza.