Kamanda awataadharisha wapiga kura Kilimanjaro

Muktasari:

Amesema jeshi hilo halitasita kuwachukulia hatua kali watakaobainika kuingia katika viashiria vya uvunjifu wa amani

Moshi. Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro Hamis Issah amesema jeshi hilo halitasita kuwachukulia hatua kali watakaobainika kuingia katika viashiria vya uvunjifu wa amani katika uchaguzi mdogo wa madiwani unaoendelea.

Issah akizungumza na Mwananchi leo Jumapili amewatahadharisha wapiga kura kuondoka katika eneo la kituo cha kupigia kura mara moja baada ya kumaliza kufanya upigaji kura.

Amesema wananchi wanapaswa kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima vinginevyo watashughulikiwa.

Licha ya Mbunge wa Moshi Mjini(Chadema), Jafary Michael kusema kuwa kuna viashiria vya uvunjifu wa amani, lakini kamanda huyo amesema hali iko shwari mpaka sasa.

Mkoa wa Kilimanjaro una kata nne ambazo zinafanya uchaguzi mdogo wa madiwani kutokana na sababu mbalimbali zilizofanya uchaguzi huo kurudiwa.