Kauli za Kinana zaacha wosia mzito

Muktasari:

  • Kauli hizo sasa zimekuwa gumzo na kuibua mijadala

Mara baada ya kujiuzulu Abdulrahman Kinana kujiuzulu wadhifa wa katibu Mkuu wa CCM, kauli zake mbalimbali alizowahi kutoa akiwa kazini zimetawala mijadala kuhusu maisha na utendaji wake.

Mbali na hilo, picha zikimwonyesha akiwa kwenye majumuku ya kueneza chama, mfano akilima, akibeba madumu ya maji, akijenga madarasa na nyinginezo zimesambaa kwenye mitando ya kijamii.

Akiwa katika mikutano yake ya hadhara na hata kwenye makongamano, Kinana hakuacha kuikosoa Serikali huku pia akitaka viongozi kuwasikiliza wananchi.

Katika moja ya mikutano alipata kusema mwaka 2015: “Nitapeleka mapendekezo, lazima ifike mahali NEC iseme, Serikali inavyoendesha mambo yake si sawa. Watendaji hawako sawa, mawaziri wavivu, tunataka muwabadilishe mawaziri na Serikali isikie, asubuhi tukute mabadiliko,” alisema Kinana.

Alieleza pia kukerwa na tabia ya wabunge wa CCM kusifia na kuunga mkono kila kitu kinachopelekwa na Serikali bungeni.

“Mambo ya Wabunge wa CCM kuunga mkono kila kinacholetwa na Serikali iwe mwisho. Nataka niwaambie wabunge wa CCM, jambo jema likiletwa lipitisheni, jambo la hovyo likiletwa, kataeni. Si kila kinacholetwa na Serikali ya CCM mnakiunga mkono, hata kama cha hovyo,”  alisema Kinana.

Akizungumza katika kongamano la Kigoda cha Mwalimu Nyerere katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Juni 2016, Kinana aliwataka viongozi kuwa na tabia ya kuwasikiliza wale wanaowaongoza.

“Jambo muhimu sana kwa kiongozi ni kuwasikiliza wale wanaowaongoza. Kwamba kiongozi hana ‘monopoly of truth’ (umiliki wa ukweli). Mara nyingi unapokuwa kiongozi ‘you claim to have the monopoly of truth, wisdom and right and this is wrong (unadai kuwa na umiliki wa ukweli, hekima na haki na hiyo si sahihi),” alisema Kinana.

Huku akitoa mfano wa Mwalimu Julius Nyerere, Kinana aliwataka viongozi kuwa tayari kuomba radhi.   

“Alipokuwa anaondoka Novemba 1985 pale Diamond Jubilee (Mwalimu Nyerere) alitoa kauli nzito sana. Alisema ‘Watanzania mmeniamini kwa miaka 24, lakini nina hakika nimefanya makosa mengi, ama kwa hakika au kwa kushauriwa vibaya, ninawaomba radhi kwa kuwa naondoka. Sasa viongozi inabidi tuwe na ujasiri wa kuomba radhi tunapokosea.”