Mama asimulia mwanaye alivyoishi kabatini miezi 5

Muktasari:

  • Mama huyo amesema alilazimika kutumia mbinu mbalimbali ili kunusuru maisha ya mtoto wake ikiwamo kumnyonyeshea katika tundu alilotoboa kabatini

Dodoma. Licha ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto kudai kwamba madai ya mtoto wa miezi mitano kufungiwa kabatini sio ya kweli, mama mzazi wa kichanga hicho amesimulia jinsi alivyotumia mbinu kuokoa maisha ya mwanaye kabatini.

Katika tukio hilo ambalo linafanana na lile la mwaka 2014 la Mariamu Said wa Morogoro kumficha mtoto wa marehemu mdogo wake kwenye boksi kwa miaka minne, mama wa mtoto huyo amedai kuwa alikuwa akitakiwa kufanya hivyo na mwajiri wake ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi jijini Dodoma.

Akizungumza na Mwananchi jana, mzazi huyo mwenye umri wa miaka 15 alisimulia jinsi alivyolazimika kuvunja sehemu ya nyuma ya kabati ili mwanaye aweze kupata hewa bila mwajiri wake kujua.

Binti huyo na mwanaye ambao wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Dodoma alisema alivunja mbao katika kabati hilo ili mwanaye apate hewa, wakati mwingine alikuwa akitumia upenyo huo kumnyonyesha kwa siri anapokuwa mwenyewe nyumbani hasa mchana.

“Hakujua kama nilivunja mbao nyepesi nyuma ya kabati lake lakini angejua sijui ingekuwaje maana asingekubali kilichofanyika,” alisema.

Binti huyo alidai kuwa ameishi kwa mwajiri wake zaidi ya mwaka mmoja na nusu baada ya kumchukua kutoka Kijiji cha Kigwe, Bahi. “Ila tangu aliponichukua hakuwahi kunilipa mshahara, alikuwa akinipa chakula tu,” alidai. “Mwanzoni aliniambia atakuwa akinilipa Sh30,000 kwa mwezi lakini sijawahi kupewa hata mia. Nilipata ujauzito nikiwa kwake na aliyenipa ni (anamtaja jina), ila tangu nimejifungua huyu mama amekuwa akinipiga.

“Asiponipiga yeye basi nitapigwa na mtoto wake wa kiume. Huyu mtoto wangu sijawahi kumnyonyesha mchana. Alikuwa akimuweka kwenye kabati lake la nguo lakini ikifika saa nane usiku ndipo ananipa nimnyonyeshe halafu asubuhi anamchukua tena.”

Polisi wakana kabati

Wakati mzazi huyo akisema hayo, Kamanda Muroto alisema wanamshikilia mwalimu huyo lakini amekanusha kukifungia kichanga hicho kabatini.

Alisema polisi walifika nyumbani kwa mwalimu huyo lakini hawakukuta kabati la aina yoyote.

“Ni kweli tulimshikilia kisha tukamwachia, lakini jana (juzi) tulimkamata tena. Awali tulimuachia kwa sababu aliyejeruhiwa hakuwa na maumivu makali wala hakulazwa na huyu kichanga hakufungiwa kabatini,” alisema Muroto.

Majirani wasimulia

Wakati binti huyo akisimulia hayo, majirani walipigwa na butwaa kwani hawakuwahi kujua kama mtoto huyo alikuwa na kichanga licha ya nyakati fulani kuhisi kuwa ni mjamzito.

Amina Asheri alisema ilikuwa ni vigumu kugundua kama mwalimu huyo alikuwa anamnyanyasa msichana wake wa kazi kwa kuwa hana ushirikiano na majirani zake.

“Mimi namuonaga huyu mwalimu anaingia na kutoka hana mpango na mtu, lakini siku ya tukio nikiwa na mwenyekiti wetu wa mtaa, Zena Chiuja tuliletewa taarifa binti amepigwa hadi hawezi kutembea wala kuinama,” alisema Amina.

Alisema baada ya mahojiano, binti huyo alisema alipigwa na bosi wake kwa kutumia fimbo ya Kimasai kwa kushirikiana na kijana wake mkubwa kwa kosa la kuchelewa kuamka na kumchemshia maji ya kuoga ndipo wakashauriana kumpeleka Polisi.

Aisha Othman alisema mateso aliyokuwa anayapata mtoto huyo yamemuathiri kisaikolojia na kusisitiza kuwa ni binti anayejitambua na anaweza kujieleza vizuri na alikuwa tegemeo kwa kazi zote za ndani.

Chiuja alisema mwalimu huyo aliwahi kumpiga mfanyakazi wake mwingine wa ndani na kufikishwa kwake ambako alimuonya na kuahidi kujirekebisha.

“Sasa lilipotokea hili nikaona si la kukanywa, bali liende polisi kwa kuwa huyu binti alikuwa hawezi hata kukaa chini kutokana na maumivu ya majeraha aliyonayo kutokana na kipigo,” alisema Chiuja.

Taarifa ya hospitali

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Dodoma, Ernest Ibenzi alisema binti huyo alilazwa kwa siku mbili na kufuatiwa na mwanaye ambaye alikuwa na utapiamlo.

“Tulimpokea Desemba 27 alikuwa na maumivu makali na majeraha sehemu za mwili wake, tulimpumzisha hadi Desemba 29 tulipoona hali yake imetengemaa na tukamlaza mtoto wake sasa,” alisema Dk Ibenzi.

Kuhusu mtoto wake, Dk Ibenzi alisema anaendelea vizuri ingawa bado anatakiwa kuwa chini ya uangalizi wa madaktari.