NSSF sasa yaliwa mchana kweupe

Muktasari:

Habari za uhakika kutoka serikalini zinasema ripoti ya ukaguzi wa miradi kujua thamani ya fedha uliofanywa na ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa ushirikiano na taasisi binafsi ya Ernst & Young umebaini uzembe na ukiukwaji wa taratibu kwa makusudi uliochangia kuwapo ufisadi huo.

Dar es Salaam. Miradi ya ujenzi iliyoanzishwa na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) miaka ya hivi karibuni imebainika kuwa na harufu ya ufisadi ikiwamo ya Mzizima na hoteli ya kitalii Mwanza ambayo makandarasi walizidishiwa zaidi ya Sh16.9 bilioni bila sababu za msingi.

Habari za uhakika kutoka serikalini zinasema ripoti ya ukaguzi wa miradi kujua thamani ya fedha uliofanywa na ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa ushirikiano na taasisi binafsi ya Ernst & Young umebaini uzembe na ukiukwaji wa taratibu kwa makusudi uliochangia kuwapo ufisadi huo.

Ofisa mmoja wa Serikali ameliambia Mwananchi kwamba miongoni mwa taratibu ambazo zilikiukwa ni kutozingatiwa kanuni wakati wa kuidhinisha miradi na mwanasheria mkuu wa serikali kutoarifiwa ili aweze kufanya ukaguzi wa kitaalamu.

Kwa mujibu wa ofisa huyo, NSSF ilitangaza zabuni kwa ajili ya ujenzi wa jengo la biashara la Mzizima Tower, Dar es Salaam, ambapo kampuni tatu ziliomba. Kampuni hizo ni Atlas, Ginde, na Jandu ambayo ilishinda.

Wakati wa kuwasilisha maombi zabuni ya Jandu ilikuwa Sh 8,346,155,654 lakini Kamati ya Tathmini iliketi na kupitia upya mkataba ilibainika makosa hivyo ilirekebisha zabuni hiyo isomeke Sh 8,340,700,710.94 pamoja na Ongezeko la Thamani (VAT). Jandu iliridhia marekebisho hayo ya hesabu.

“Kitu cha ajabu ni kwamba pamoja na marekebisho hayo, mkataba waliosainiana kati ya NSSF na Jandu ulikuwa wa kiwango kilekile kilichokosewa cha Sh8,346,155,654 chenye ziada ya Sh5,454,943. Kwa maneno mengine hasara iliyoingiwa kwa kutia saini mkataba wa awali ni Sh5.45 milioni,” alisema ofisa huyo.

Kuhusu ujenzi wa hoteli ya kitalii ya Mwanza, taarifa zinasema kampuni tatu ziliomba kazi hiyo mwaka 2013 lakini iliyoshinda zabuni ilikuwa China Railway Jianchang Engineering Co. (T). Mradi huo uliokuwa wa thamani ya Sh 72.85 bilioni ulijumuisha pia uwekaji wa umeme, viyoyozi, vifaa vya usalama, mabomba ya maji na mawasiliano ya simu.

Ofisa wa serikali alisema ukaguzi wa mradi huo uliofanywa na CAG na Ernst & Young umegundua kuwa NSSF iliingia mkataba mwingine na kampuni nyingine kwa ajili ya uwekaji wa umeme, viyoyozi, vifaa vya usalama, mabomba ya maji na mawasiliano ya simu, kazi zilizomo kwenye mkataba iliopewa kampuni ya Kichina. Mkataba huo mpya ni wa thamani ya Sh16.98 bilioni sawa na asilimia 23 ya mradi wote.

“Mradi wa Mzizima ulitakiwa uwe wa gharama pungufu kwa Sh5.45 milioni, lakini NSSF wakasaini mkataba wa bei ya juu, huu wa Mwanza kila kitu kilikuwamo kwenye mkataba wa mkandarasi wa Kichina lakini ukatiwa saini mkataba mpya wa zaidi ya Sh 16.9 bilioni. Miradi hii imeongezewa takriban Sh16,986,295,752; kama huu si ufisadi ni nini,” alisema ofisa huyo.

“Kama nilivyosema awali hili ni kosa kubwa na kwa vile walijua kwamba wamefanya kosa NSSF hawakumshirikisha kabisa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili afanye uchunguzi wa kitaalamu kwenye miradi yake kwa mujibu wa sheria.”

Ofisa huyo alizungumzia mkataba mwingine uliofanywa kifisadi kuwa ni wa Sh 1.078 bilioni wa manunizi ya sare za wafanyakazi ambao NSSF iliingia na kampuni ya Pink Diamond.

Hata kabla ya mkataba kusainiwa, ripoti inasema NSSF iliilipa Pink Diamond Sh 215.4 milioni sawa na asilimia 20 ya thamani ya mkataba. Hatua ya NSSF kufanya malipo hayo kabla ya mkataba ni uvunjaji wa sheria ya manunuzi, kwani malipo ya awali kwa ajili ya kazi serikalini, yanapaswa kufanywa baada ya mkataba kusainiwa.

Ripoti inaonyesha kuwa mkataba wenyewe ulisema baada ya kusaini ndipo Pink Diamond wangestahili kulipwa asilimia 20 ya zabuni lakini walilipwa kabla ya kusainiwa kwa mkataba. Baada ya mkataba kusainiwa Machi 4, 2015, Pink Diamond waliandika barua kwenda NSSF wakiomba nyongeza ya asilimia 20 ya zabuni ili waweze kufanya kazi na katika hali ya kushangaza Machi 13, 2015 NSSF iliidhinisha malipo mengine ya Sh 215.4 milioni. Hatua ya Pink Diamond kulipwa Sh 431 milioni sawa na asilimia 40 kabla ya kazi kufanyika ni ukiukwaji wa kanuni.

Mkataba uliitaka Pink Diamond kukabidhi sare hizo katika muda wa siku 90 yaani kabla ya Aprili 23, 2015 lakini ilikabidhi nje ya muda yaani Julai 21, 2015 na hawakuadhibiwa.

Katika toleo la jana Mwananchi liliripotiwa kuwa mradi mkubwa wa ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni jijini Dar es Salaam uitwao Dege Eco Village, ulioanzishwa pia na NSSF umesimama huku ikiripotiwa kuwapo kwa ufisadi wa zaidi ya Sh179 bilioni. Hii inatokana na NSSF “kununua” kutoka kwa mbia mwenzake Azimio Housing Estate ekari moja kwa Sh800 milioni huku ikikubali pia ‘kuuziwa’ ardhi Arumeru-Arusha kwa Sh 1.8 biloni kwa ekari kinyume cha thamani halisi ambacho ni Sh 500,000 mpaka Sh 1 milioni..

Mwananchi lilifanya juhudi kupata ufafanuzi kutoka NSSF. Kwanza liliambiwa shirika hilo halikuwa na Mkurugenzi Mkuu tangu Februari 15 baada ya Dk Dau kuteuliwa kuwa balozi.

Alipofuatwa Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji wa Miradi wa NSSF, Yacoub Kidula alitaka apelekewe maswali ili ajibu kwa maandishi. Alipopelekewa maswali kwa maandishi alitaka yaandikwe kwenye karatasi yenye jina la kampuni na namba ya kumbukumbu.

Baada ya wiki kadhaa za kufuatilia majibu, baadaye barua ilipelekwa kwa Mkurugenzi wa Mawasiliano, Eunice Chiume ambaye alisema hawezi kuijibu kwa kuwa bado ofisi hiyo haikuwa na mkurugenzi mkuu.

“Endeleeni kuwa wavumilivu kwa sababu sisi hatuwezi kuzungumza chochote bila kuwa na mkurugenzi mkuu. Tukimpata atajibu kwa sababu taratibu za ofisi zetu ni kuwa mkurugenzi mkuu ndiye mwenye majibu ya kila kitu,” alisema Chiume.

Rais John Magufuli alipomteua, Profesa Godius Kahyarara kuwa Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, bado majibu hayakutolewa. Chiume alisema Profesa Kahyarara bado anajifunza mazingira ya shirika.