Ndege nyingine ya Serikali kuwasili Tanzania

Muktasari:

Msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abbas amesema Serikali itapokea ndege yake nyingine mpya toleo la Airbus A220-300  Jumapili Desemba 23, 2018.

Dar es Salaam. Msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abbas amesema Serikali itapokea ndege yake nyingine mpya toleo la Airbus A220-300  Jumapili Desemba 23, 2018.

Abbas ameeleza hayo leo Ijumaa Desemba 21, 2018 katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter.

“Ungana nasi kuipokea ndege ya kwanza kununuliwa na Serikali kwa toleo la Airbus A220-300. Ni Tanzania pekee.’Ngorongoro-Hapa kazi Tu’, itawasili nchini Jumapili hii na siku chache baadaye ndege nyingine kama hiyo itawasili Dodoma-Hapa Kazi Tu,” ameandika Dk Abbas.

Julai, 2018 Rais John Magufuli aliwaongoza Watanzania katika sherehe ya mapokezi ya ndege mpya aina ya Boeing 787-8 Dreamliner.

Ndege hiyo ilitua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) ikitokea mjini Seattle Marekani.

Kabla ya tukio hilo, Septemba 28, 2016, kiongozi huyo wa nchi pia alizindua ndege mbili mpya aina ya Bombardier Q 400 zilizonunuliwa na Serikali.

Ndege hizo zenye uwezo wa kubeba abiria 76 kila moja zimetengenezwa nchini Canada na zinahudumia soko la ndani.