Uchaguzi Mkuu DRC palepale

Muktasari:

Licha ya kuteketea kwa moto ghala la kuhifadhia vifaa vya uchaguzi mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya nchi hiyo (CENI) imesema uchaguzi mkuu uliocheleweshwa tangu Desemba 2016 utafanyika Desemba 23 kama ilivyopangwa.

 


Kinshasa, DR Congo. Licha ya kuteketea kwa moto ghala la kuhifadhia vifaa vya uchaguzi mkuu, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya DRC (CENI) imesisitiza kuwa upigaji kura utaendelea kama ilivyopangwa Desemba 23.

Taarifa iliyotolewa na CENI baada ya kufanya tathmini ya awali ya uharibifu huo imesema vifaa vya uchaguzi vilivyoteketea kwa moto ni vile ambavyo vilikuwa vimeandaliwa kwa wapiga kura wa jiji la Kinshasa.

Msemaji wa CENI, Jean-Pierre Kalamba amethibitisha tukio hilo la moto kwenye moja ya ofisi za tume hiyo Alhamisi asubuhi.

Kalamba alisema tume hiyo itatoa tathmini kamili baadaye lakini kwa makadirio ya sasa kilichoteketezwa hakiwezi kusitisha mchakato wa uchaguzi.

Alisema vifaa vya uchaguzi wa majimbo mengine 25 havikuwapo Kinshasa wakati wa moto huo kwani vilishahamishiwa majimboni.

Alipoulizwa kisa cha ghala kuchomwa moto na watu wasiojulikana, Felix Tshisekedi mmoja wa wagombea wa kiti cha urais kupitia chama cha upinzani cha Democracy and Social Progress (UDPS) alilaani akidai kuwa hofu yake ni kwamba Serikali ya DRC itahusisha moto huo na wapinzani wake.

Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani wa DRC, Emmanuel Ramazan Shadary  anawania urais kupitia muungano unaotawala unaoongozwa na Rais Joseph Kabila, wakati upinzani una wagombea kadhaa wakiwamo Tshisekedi na Martin Fayulu.