Mgogoro wa Loliondo wamsubiri Kigwangala

Muktasari:

Wamemtaka Dk Kigwangala akutane na wakazi wa eneo hilo ili waweze kumweleza kiini cha mgogoro wa eneo la pori tengefu.

Loliondo. Wananchi pamoja na viongozi wa maeneo mbalimbali katika tarafa ya Loliondo wamefurahia kupigwa chini aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe huku wakimsubiri kwa hamu waziri mpya Dk Hamis Kingwangala.

Wamemtaka Dk Kigwangala akutane na wakazi wa eneo hilo ili waweze kumweleza kiini cha mgogoro wa eneo la pori tengefu.

Wananchi hao wamesema kupigwa chini Profesa Maghembe kimewapa faraja na matumaini ya kubaki katika ardhi wanayoipigania.

Wakizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana Jumatano katika eneo la Ololosokwan baadhi ya wakazi wa tarafa hiyo walimshauri Dk Kingwangala kutosikiliza majungu bali anapaswa kufika eneo la mgogoro na kupata ukweli.

Diwani wa Kata ya Ololosokwani, Yannick Ndoinyo amesema kwamba Dk Kingwangala anapaswa kukutana na wakazi wa eneo hilo ili waweze kumweleza kiini cha mgogoro unaofukuta mpaka sasa huku akimshauri ajiepushe na wapiga majungu.

“Waziri Kingwangala tunaomba akutane na sisi aje tumweleze kiini cha mgogoro na akitusikiliza hapa nawahakikishia hakuna mgogoro,” alisema Ndoinyo.

Hata hivyo, alisisitiza kwamba wateule katika wizara ya maliasili na utalii wanapaswa kutambua ya kwamba ardhi wanayoipigania ni mali yao kisheria na kusema kwamba kinachofanyika kwa sasa ni uvamizi na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Diwani wa Kata ya Soitsambu, Boniphace Kanjwel alisema wanamshukuru Rais Magufuli kusikia kilio cha wakazi wa eneo hilo kupitia ujumbe wa mabango mbalimbali waliyomwonyesha wakati akiwa katika uwanja wa michezo wa Sheikh Amri Abeid.

Kanjwel amesema Dk Kingwangala anapaswa kutambua kwamba jamii ya wamasai ni wahifadhi wazuri wa mazingira tofauti na uvumi unaoenezwa kwa sasa kwamba wao ndio chanzo cha uharibifu wa mazingira katika eneo la Loliondo.

“Baada ya kubeba mabango tunamshukuru Rais Magufuli alisikia kilio chetu lakini tunaomba kumwambia waziri Kingwangala kwamba jamii ya wamasai ni wahifadhi wazuri wa mazingira,” amesema Kanjwel

Kwa upande wake diwani wa viti maalumu kupitia CCM wilayani Ngorongoro, Tina Timan alipinga baadhi ya propaganda zinazoenezwa kwamba wakazi wa eneo hilo ni raia kutoka nchini Kenya na kusisitiza kwamba wao ni Watanzania halali na kumwomba Dk Kingwangala kukutana nao.

Katibu wa CCM Kata ya Ololosokwan, Saibulu Letama amesema kwamba wao kama chama tawala wanampongeza Rais Magufuli kwa mabadiliko ya baraza la mawaziri aliyofanya na kudai kwamba wananchi wa eneo hilo wamekuwa wakitegemea shughuli za ufugaji kama njia mojawapo ya kuwaingizia kipato kiuchumi.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Olorien, Nektayo Ledidi kwa upande wake amesema wao kama jamii ya wamasai wanaiomba Serikali kutambua ya kwamba wao ni Watanzania wanaostahili haki ya kupatiwa makazi na sio kunyanyaswa.

Katika operesheni ya kuwaondoa wakazi wanaoishi katika  eneo la pori tengefu iliyoendeshwa na Serikali  hivi karibuni  jumla ya maboma 463 yameteketezwa kwa moto, mifugo 300 imefariki kwa kukosa chakula baada ya kukamatwa, mifugo 618 imetaifishwa baada ya kukamatwa na mifugo 590 inashikiliwa kizuizini kwa muda wa miezi mwili mpaka sasa.