Mbunge CCM anaswa kwa tuhuma za rushwa

Mbunge wa Kishapu (CCM), Suleiman Nchambi 

Muktasari:

Mbunge huyo na viongozi wengine wa mgodi wa Stamigold leo wanatarajia kufikishwa mahakamani


Biharamulo. Mbunge wa Kishapu (CCM), Suleiman Nchambi na viongozi watatu wa mgodi wa Stamigold ulioko Tulawaka wilayani Biharamulo mkoani Kagera, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Wilaya ya Biharamulo, Hassan Mosi amesema mbunge huyo na wenzake walikamatwa na kuwekwa rumande katika gereza la wilaya hiyo Jumamosi Agosti 4, 2018.

Amesema leo Jumatatu Agosti 6, 2018 watafikishwa mahakama ya wilaya ya Biharamulo kwa kosa la kufanya miamala ya kupokea rushwa.

Mosi amesema kitendo hicho ni kinyume na  kifungu cha15 cha  sheria namba 11 ya mwaka 2007 ya kupambana na kuzuia rushwa.

"Wakifikishwa mahakamani watasomewa mashtaka yanayowakabili. Wanaweza kukiri au kukanusha na sheria itachukua mkondo wake,” amesema.

Ndugu, jamaa na marafiki leo wamejitokeza kwa wingi katika mahakama hiyo, huku wengi wakionekana kuwa na shauku ya kujua hatima ya viongozi hao.