Sunday, October 7, 2018

Mbunge wa saba upinzani ahamia CCMMbunge wa Simanjiro (Chadema), James Millya.

Mbunge wa Simanjiro (Chadema), James Millya. 

By Bakari Kiango, Mwananchi bkiango@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mbunge wa Simanjiro (Chadema), James Millya amejiuzulu nafasi hiyo na uanachama wa chama hicho kikuu cha upinzani huku akitangaza kurejea CCM.

Millya ambaye alimshinda Christopher Ole Sendeka (CCM) katika uchaguzi mkuu mwaka 2015 ametangaza uamuzi huo leo, Jumapili Oktoba 7, 2018 katika barua yake kwenda kwa Spika wa Bunge Job Ndugai.

Katika barua hiyo, Millya amesema amekuwa mwanachama wa Chadema kwa miaka sita baada ya kuhama CCM uamuzi aliouchukua kutokana na kiu ya kuitafuta haki wakati huo na jukwaa ambalo angeweza kupaza sauti kwa misingi ya hoja na kupambana na rushwa na ufisadi.

“Naandika barua hii nikiwa na uhalisia mwingine kabisa, kila mtu atakuwa shuhuda nimekuwa si mtu wa siasa za jukwaani kwa miaka hii mitatu.”

“Ni dhahiri kwamba nimepoteza imani na kukosa amani, mahali nilipo sipaoni tena kama ni jukwaa la kunituma na kuhamasisha kuwaletea maendeleo wana Simanjiro,” amesema Millya.

Amesema chama cha siasa kinapaswa kuwa taasisi yenye mwelekeo wa kiitikadi na inayowatuma wawakilishi akiwemo yeye kuwahamasisha wananchi kushirikiana na Serikali kutafuta na kuleta maendeleo na si vinginevyo.

“Ukweli ambao nimeuishi umekuwa mchungu na kinyume na matarajio yangu. Najua siasa za siku hizi msingi wake si siasa safi na zinatufanya ukiwa mbunge wa upinzani kila jambo unapinga hata pale kazi nzuri imefanyika ni dhambi kuunga mkono na kutoa hamasa ya kuongeza juhudi.”

“Siasa hizi hazina afya kwa Taifa letu na wananchi wa Simanjiro, licha ya changamoto za hapa na pale lakini ukweli usiopingika Serikali ya CCM imefanya kazi kubwa sana chini ya Rais John Magufuli,” amesema Millya.

Millya amesema kinachosikitisha badala ya kusimama pamoja katika mafanikio ya Rais Magufuli na kumsaidia kwa kumpa mbadala wa hoja na mipango, matokeo yake upinzani umekuwa na kazi ya kubeza na kuponda chochote kinachofanyika.

Ameongeza bahati mbaya hata pale yanayofanyika na kugusa na kubadilisha maisha ya Watanzania, alisema hizo si siasa alizokuwa akizitarajia upinzani izifanye katika Taifa ambalo lina kazi kubwa la kukombolewa kiuchumi.

“Kipindi hiki nikiwa huru nimejipanga kufanya kazi na wadau mbalimbali wakiwemo wabunge wa maeneo ya wafugaji na viongozi wa Serikali ili kutoka na mapendekezo ya utatuzi wa kudumu wa changamoto za wavuvi, wakulima na wafugaji na namna ya kuratibu matumizi bora ya ardhi na maeneo yao,” amesema.

Wabunge wengine sita wa upinzani waliohamia CCM ni; Maulid Mtulia (Kinondoni-CUF), Dk Godwin Mollel (Siha- Chadema), Julius Kalanga (Monduli- Chadema), Mwita Waitara (Ukonga- Chadema), Zuberi Kuchauka (Liwale- CUF), Marwa Chacha (Serengeti) huku Lazaro Nyalandu (Singida Kaskazini) akitoka CCM kwenda Chadema.

-->